Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyekata rufaa afungwa maisha

Muktasari:

Kabla ya kukata rufaa, hukumu iliyotolewa katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela

Dar es Salaam. Kwa kawaida kukata rufaa ni haki ya upande usioridhika na hukumu katika kesi yoyote kwa lengo la kupata nafuu, lakini wakati mwingine huambulia machungu anapoongezewa adhabu kama ilivyotokea kwa mfungwa Paul Dioniz.

Awali, Dioniz ambaye ni fundi viatu alikata rufaa Mahakama ya Rufani akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyounga mkono hukumu ya Mahakama ya Wilaya Kinondoni iliyomhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumnajisi mwanafunzi mwenye umri wa miaka minane.

Dioniz alikuwa akitarajia mahakama hiyo igeuze hukumu ya awali kwa kumuondolea hatia na kumfutia adhabu hiyo, hivyo kumwachilia huru.

Pamoja na mambo mengime katika rufaa hiyo alikuwa akidai kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake bila kuacha shaka.

Hata hivyo, matokeo ya rufaa yake hiyo yamekuwa kinyume cha matarajio badala yake imemponza kwa kuwa alijikuta akiongezewa adhabu kutoka kifungo cha miaka 30 hadi kifungo cha maisha jela.

Uamuzi huo wa kumpa adhabu hiyo ya juu kabisa umetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Rehema Mkuye (kiongozi wa jopo), Ferdinand Wambali na Ignas Kitusi, lililosikiliza rufaa yake.

Katika hukumu yake, kwanza Mahakama ilieleza kuwa imeridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha mashtaka dhidi yake bila kuacha shaka lolote.

Pili, Mahakama ilisema inakubalina na wakili wa Serikali, (Gloria Mwenda aliyeiwakilisha Serikali wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo) kuwa adhabu hiyo aliyopewa mrufani ya kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kunajisi mtoto haikuwa sahihi.

Ilielezwa kuwa kifungu cha 131 (2) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code-PC) kiko wazi kabisa kwa kuwa kinaweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mtu anayetiwa hatiani kwa kosa la unajisi wa mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 10.

“Hivyo kwa kuzingatia kufungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Sura 141, marekebisho ya mwaka 2019, tunabadili adhabu kutoka kifungo cha miaka 30 jela kuwa kifungo cha maisha jela,” Ilisema Mahakama hiyo katika hukumu hiyo.

Katika kesi ya msingi, kwa mujibu wa kumbukumbu za Mahakama, Agosti 6, 2016, asubuhi, baba wa mtoto huyo alimuona mtoto kama amekojolewa katika nguo yake na alipomuuliza mkewe kuhusu hali hiyo, alimjibu kuwa hali hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa mtoto huyo.

Mama huyo alisema katika siku za karibuni mtoto huyo amekuwa akichelewa kurudi kutoka shule na wakati mwingine hata chakula alikuwa hali.

Baba alitoa taarifa kwa mwalimu wake na alipohojiwa mtoto huyo alisema fundi viatu huyo, amekuwa akimpa fedha na chipsi.

Pia, alimweleza baba yake kuwa Dioniz amekuwa akimpeleka katika pagale ambamo hutunzia vifaa vyake vya kazi na kumbaka (kunajisi).

Baba aliripoti polisi, mtoto huyo akapelekwa katika Hospitali ya Palestina Sinza kwa vipimo, ingawa hakukutwa na michubuke katika sehemu zake za siri wala manii, lakini ilibainika kwa hakuwa na kizinda (bikira), jambo ambalo halikuwa la kawaida kwa mtoto mwenye umri huo.

Hata hivyo, Dioniz alikana mashtaka na katika utetezi wake alidai kuwa alikamatwa katika eneo lake la kazi na akapelekwa mahabusu bila kuambiwa kosa lake .

Septemba 2,2016 alipandishwa kizimbani (katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni) na kusomewa shtaka la ubakaji (kunajisi).

Licha ya kuita mashahidi wengine wawili kumtetea, lakini Mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu adhabu hiyo ya kifungo cha miaka 30 jela.

Alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini haikukubalina na sababu na hoja zake za rufaa, badala yake ilikubaliana na hukumu ya Mahakama ya Kinondoni pamoja na adhabu hiyo, ndipo akakata tena rufaa hii Mahakama ya Rufani.