Alivyoponyoka kifo cha kinyama kwa muda -3

Muktasari:

Katika matoleo mawili yaliyopita, tuliona jinsi mtoto George Stinney mwenye umri wa miaka 14 alivyonyongwa hadi kufa Juni 16, 1944. Tukio hilo limeweka kumbukumbu mbaya kwa kuwa mwanadamu wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kukutana na adhabu hiyo katika karne ya 20.

Katika matoleo mawili yaliyopita, tuliona jinsi mtoto George Stinney mwenye umri wa miaka 14 alivyonyongwa hadi kufa Juni 16, 1944. Tukio hilo limeweka kumbukumbu mbaya kwa kuwa mwanadamu wa kwanza mwenye umri mdogo zaidi kukutana na adhabu hiyo katika karne ya 20.

Udogo wake ulifanya iwe vigumu kumfunga kwenye kiti cha umeme cha kumnyongea kiasi kwamba, alianguka sakafuni wakati mnyongaji alipogeuza swichi. Hukumu hiyo ni baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua watoto wawili--Betty June Binnicker (11) na mwenzake Mary Emma Thames (7).

Wakati wa kukamatwa kwake na upelelezi kudai kuwa aliwabaka wasichana hao kabla ya kuwaua, wakazi wengi wa eneo hilo walitaka kumkamata na kumuua mara moja. Lakini, aliponyokaje mauaji hayo wakati wako wengi waliuawa kwa njia hiyo?

Kihistoria katika miaka ya 1930 na 1940, Wamarekani weusi, hasa wenye asili ya Afrika, walikuwa wakipitia mateso ya ubaguzi wa rangi kiasi cha yeyote anayetuhumiwa kumdhulumu mtu mweupe, ilitosha kupata hukumu ya kifo au kuchukuliwa sheria mkononi.

Mmoja wa watu walioponyoka kwenye mateso hayo ni mama mzazi wa George, ambaye alihukumiwa kunyongwa, lakini baada ya kunyongwa kwa kutumia kiti cha umeme, ilikuja kubainika baadaye kwamba hakuwa na hatia.

Takriban watu 4,000 waliuawa nchini Marekani kati ya mwaka 1880 na 1940, kulingana na uchunguzi wa kihistoria wa Gunnar Myrdal kuhusu Wamarekani weusi, uliochapishwa mwaka huo. Asilimia 80 ya waliouawa kwa kuchukuliwa sheria mkononi walikuwa weusi.

Hali hii ilitokea kwenye maeneo mbalimbali nchini Marekani katika karne ya 19. Kati ya mwaka 1880 na 1940, mauaji ya aina hiyo yalikuwa ni asilimia 90 Kusini mwa Marekani na zaidi ya theluthi mbili ya asilimia 10 iliyobaki ya mauaji hayo ilitokea Maryland, West Virginia, Ohio, Indiana, Illinois na Kansas, majimbo sita ambayo yamepakana na Kusini.

Mauaji yangeweza kufanywa kwa kupigwa risasi, kunyongwa au kuchoma moto. Kuuawa kwa kupigwa risasi kunaweza kusisababishe uchungu sana, ingawa wakati mwingine wauaji walichakaza miili kwa wingi wa risasi. Kifo kwa kuchomwa moto, kutundikwa juu ya mti au juu ya moto, ndicho kilisababisha machungu zaidi.

Kuuawa kwa kuchinjwa nako kulifanyika na kusababisha mateso ya kutisha kwa anayeuawa. Wakati mwingine wauaji walikuwa wakimburuta mtu kwa farasi au gari hadi umauti umfike.

Kati ya 1907, mwaka mama yake George Stinney alipozaliwa, na Machi 25, 1944 siku ambayo mtoto wake alikamatwa, angalau mauaji 49 yaliyothibitishwa yalifanyika katika Jimbo la South Carolina. Mwaka 1911, mtoto wa miaka 17 aliyeshtakiwa kwa kumbaka mwanamke mzungu alivutwa juu ya nguzo ya simu, akasimamishwa kwa muda kichwa chini, kisha akapigwa risasi. Miaka mitano baadaye, Anthony Crawford, mkulima wa Kiafrika ambaye alikuwa na mafanikio, alipozozana na mfanyabiashara mwenye ngozi nyeupe, ilimtosha kumfanya auawe kwa kutundikwa juu ya mti na kuchomwa kwa vijiti mwilini hadi alipofariki.

Tuhuma za kubaka zilichukuliwa kwa uzito na jamii ya Wamarekani wa Kusini huko South Carolina. Jamii hiyo ilikuwa na hoja mbili ambazo waliona ni za msingi kwao: Kwanza, wanawake wa kizungu walipaswa kulindwa wasijamiiane na wanaume weusi.

Pili ni kwa sababu waliamini kuwa kulikuwa na kasoro nyingi katika mfumo wa sheria jinai nchini Marekani. Kasoro hizi, walidai zilichelewesha kutoa hukumu. Hata Kardinali wa Boston, Kadinali J. Gibbons, ambaye kwa ujumla alipinga mauaji ya aina hiyo, alikubaliana na wanaoyatetea akidai sheria hizo zilitoa mwanya kwa wabakaji wengi kuponyoka adhabu.

Jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya Alabama aliona kwamba: “Kitendo cha kuchelewa kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria ... kunaonekana kutumika kama ‘msamaha unaowezekana’ kwa wahalifu.”

Sababu zote mbili zilikaribia kutumiwa katika matukio ya Alcolu siku iliyofuata baada ya wapelelezi kudai kuwa George aliwabaka watoto wawili wa kizungu na kisha kuwaua.

Baada ya tuhuma hizo, baadhi ya wanaume walijiandaa hata kumfanyia vitendo vya ulawiti George wakiamini shambulio la mwanamume mweusi dhidi ya wanawake weupe lazima lishughulikiwe kwa njia ya haraka bila kuchelewesha.

Kuponyoka kwa George Stinney kwenye kitanzi cha kuuawa na watu waliokuwa tayari kujichukulia sheria mikononi haikuwa kawaida. Ingawa kulikuwa na mauaji 762 kati ya mwaka 1915 na mwaka 1941 yaliyofanywa na waliojichukulia sheria mikononi, zaidi ya mara mbili ya matukio kama hayo yalizuiwa. George alinusurika kifo mikononi mwa umati, lakini hakunusurika kunyongwa kwenye kiti cha umeme.

Maofisa wa polisi walijitahidi kuwahakikishia watu waliokuwa na hasira kuwa George atashtakiwa na hukumu yake itapatikana haraka iwezekanavyo. Hayo ndiyo makubaliano yaliyofanywa kati ya maofisa wa polisi na wanaume wenye hasira waliokusanyika kumshambulia George Stinney. Ingawa hakukuwa na uhakika au ahadi iliyotolewa kwamba angepatikana na hatia mahakamani.

Miaka 39 baada ya mauaji ya wasichana hao, Roston Stukes ambaye alijieleza kama mmoja wa viongozi wa umati wa watu waliokusanyika kumuua George, alikaririwa na jarida la ‘North American Review’ akizungumzia mpango huo:

“Tulikuwa tumejiandaa kumuua ... Ilikuwa afe. Nilishiriki kwenye mpango huo na nilikuwa kiongozi wa mpango huo. Sijali kukiri hilo... huo ndio ulikuwa mpango wetu. Baadaye tukasema waache wamshtaki na walituhakikishia kwamba tungeweza kumwona akikutwa na hatia.

“Hawakusema kwamba angehukumiwa, tungeweza kumwona kama asingenyongwa kwenye kiti cha umeme ... Tulikwenda Columbia [kwenye gereza] ... na tukaingia mle na tukaona akinyongwa hadi kufa.”

Stukes hakutambua ni nani alitoa ahadi hiyo, lakini kuna uwezekano walikuwa ni wale maofisa wa polisi ambao ni Huger Newman na Sidney Pratt katika jela ya Manning walimokuwa wamemshikilia George Stinney. Maofisa hawa ndio waliodai kuwa George alikiri kuwaua wasichana wawili na aliwabaka, ingawa madaktari walioichunguza miili hiyo walidai kuwa “...Sehemu za siri na kizinda zilikuwa shwari.”

‘Upelelezi’ wa maofisa hao ndio uliopandisha hasira za watu kiasi cha kutaka kujichukulia sheria mkononi na kumuua kijana mdogo, ambaye miaka 70 baadaye ilikuja kuonekana kuwa hana hatia ya si tu mauaji, bali hata kubaka alikodaiwa kuwa alifanya.

Hata hivyo, wakati watu wenye hasira wakiwa wamejiandaa kuvunja gereza la Kaunti ya Clarendon; maofisa walifanikiwa kumsafirisha George kwa siri hadi jela ya Sumter County kulikokuwa salama zaidi kwake.

Wazazi wake na nduguze nao walifanikiwa kuondoka Alcolu ambako wakazi wengi wa eneo hilo walitishia uhai wao kwa sababu ya mauaji ya wasichana wawili yaliyodhaniwa tu kuwa yalifanywa na mtoto wao.

George Stinney na baba yake walikuwa salama kwa hiyo, lakini kwa muda mfupi. Mauaji ya George Stinney yalikuwa yameahirishwa kwa muda. Mwezi mmoja baadaye, wangehudhuria kesi ya George wakiwa na silaha zilizofichwa kwenye mifuko yao, ili ikiwa mtoto huyo mwenye umri wa miaka 14 hatahukumiwa kifo, basi wamkamate na kumuua hapo hapo.


Je, hii ndiyo sababu ilitengeneza mwelekeo wa kesi hadi akahukumiwa kama alivyohukumiwa? Tukutane toleo lijalo.