Ajiua baada ya kutengana na mkewe

Muktasari:
- Mkazi wa mtaa wa Tushikamane kata ya Lukobe Wailaya ya Morogoro, Wiliam Emily (45) amejinyonga hadi kufa kwa kutumia shuka huku sababu zikidaiwa kuwa ni mgogoro wa ndoa na mke wake.
Morogoro. Mkazi wa mtaa wa Tushikamane kata ya Lukobe Wailaya ya Morogoro, Wiliam Emily (45) amejinyonga hadi kufa kwa kutumia shuka huku sababu zikidaiwa kuwa ni mgogoro wa ndoa na mke wake.
Tukio hilo ni la pili kutokea katika mtaa huo ndani ya mwezi mmoja ambapo la kwanza lilitokea Novemba 15 mwaka huu baada ya mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Lukobe mwenye umri wa miaka 13 kujinyonga kwa kutumia kamba ya Manila na kufariki dunia.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba 10, 2021Mwenyekiti wa mtaa huo, Omary Hassan amesema kuwa Wiliam amejinyonga usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake alikokuwa akiishi na watoto wake wawili baada ya kutengana na mke wake kufuatia migogoro wa ndoa yao.
Amesema kuwa kabla ya kujinyonga Wiliam aliwaambia watoto wake wawili ambaye mmoja anamaliza darasa la saba mwaka huu kuwa waende wakacheze na baadaye aliingia ndani na kujinyonga hadi kufa.
Amesema marehemu alitengana na mke wake ambaye wamezaa watoto wanne ambapo watoto wawili walikuwa wakiishi na mama yao ambaye amepanga mtaa wa jirani huku watoto wengine wawili walikuwa wakiishi na baba yao.
Mwemyekiti huyo amesema tayari mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi wa kidaktari na ndugu wameshakabidhiwa kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho Jumamosi katika kijiji cha Kisaki wilaya ya Morogoro.
"Kwa sasa ndugu wapo kwenye vikao ili kuhakikisha mwili wa marehemu unafika Kijiji kwao, kuhusu masuala mengine ya kiuchunguzi tunaliachia Jeshi la Polisi ambalo ndio lenye mamlaka ya kuchunguza," amesema Hassan.