Ajira chanzo wanafunzi kukimbia baadhi ya kozi vyuoni

Muktasari:

  • Ripoti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ya mwaka 2023 inaonyesha jinsi baadhi ya kozi mathalan za madini na sayansi ya dunia, sayansi ya maisha zikiwa na wanafunzi wachache.

Dar es Salaam. Wakati idadi ya udahili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza ngazi mbalimbali vyuoni mwaka 2023/2024 ukishuka kwa asilimia 22.3 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, madini na sayansi ya dunia, sayansi ya maisha, utalii na ukarimu zinaongoza kwa kukimbiwa na wanafunzi.

Hiyo ni baada ya takwimu kuonyesha kuwapo idadi ndogo ya wanafunzi wanaochagua kusoma kozi hizo, huku wadau wa elimu wakitaja ufinyu wa soko la ajira, kutokuwapo kwa msingi mzuri tangu ngazi ya chini na kukosekana kwa unasihi kama sababu.

Hayo yanasemwa wakati ambao Ripoti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ya mwaka 2023 inaonyesha jumla ya wanafunzi 106,570 walidahiliwa kuanza mwaka wa kwanza 2023/2024 katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pungufu kutoka wanafunzi 137,272 mwaka uliotangulia.

Wakati anguko hilo likitajwa, ripoti hiyo inaonyesha ni wanafunzi 589 pekee ndiyo walichagua kozi ya madini na sayansi ya dunia, 743 wakisomea sayansi ya maisha, 972 wakisoma maktaba, kumbukumbu na makumbusho (Library, Archive and Museum Studies), 1,081 usanifu na mipango huku 1,326 wakichagua masomo ya sayansi ya kifizikia na hesabu (Physical Sciences and Mathematics).

Kozi ya elimu na ile ya biashara ndizo zinazoongoza kwa kubeba idadi kubwa ya wanafunzi vyuoni.

Katika mwaka 2023/2024 wanafunzi 20,271 walichagua masomo ya biashara huku 27,731 wakisomea elimu. Kwa pamoja fani hizo zinabeba asilimia 45.03 ya wanafunzi wote waliodahiliwa mwaka huo wa masomo.

Pamoja na wingi huo, idadi ya waliochagua kozi ya biashara ni pungufu kwa asilimia 54.12 ya wanafunzi waliochagua fani hiyo mwaka uliotangulia.

“Kukosekana kwa ajira ya uhakika kwa watu wanaohitimu baadhi ya fani ni moja ya kigezo kinachofifisha tija ya kozi hiyo,” anasema mdau wa elimu, Catherine Sekwao alipozungumza na Mwananchi.

Anasema kuna baadhi ya fani nafasi za ajira ni chache, wakati ambao aina ya masomo yaliyotolewa pia hayamwezeshi mtu kujiajiri.

Hali hiyo ndiyo inafanya watu kukimbilia kozi ambazo wanaweza kuajiriwa au ufundi ambao wanaweza kujiajiri baadaye.

Moja ya sababu ya kukosekana kwa ajira ni kuwapo kwa mtindo wa kuwaongezea muda wastaafu baada ya umri wa kufanya kazi kumalizika, hali inayowanyima fursa wahitimu.

“Sisi wastaafu tukubali kustaafu, hii mikataba ya miaka miwili miwili inakosesha watoto wetu fursa ya kuajiriwa, mtu wa madini akikosa ajira hana mahali pa kwenda labda na yeye awe mchimbaji,” anasema Sekwao.

Katika hili, mwanasaikolojia, John Ambrose aliwahi kuliambia Mwananchi kuwa baadhi ya watu wanaoajiriwa wanashindwa kutambua kustaafu ni mchakato wanaopaswa kufanya kuanzia miaka 10 hadi 15 wakiwa bado kazini na bila kufanya hivyo inamfanya mtu kujikuta katika wakati mgumu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya funguo, Nicodemus Shauri anatilia mkazo suala la ajira kwa wahitimu, huku akitolea mfano wa fizikia na hisabati kuwa ni ngumu kujiajiri wakihitimu.

“Walimu wa fizikia na hesabu ni wachache sana shuleni, lakini wanaoajiriwa kwa mwaka ni wachache sana, hali hii inafanya watu wasione umuhimu wa kusoma kozi hizo kwa sababu hawaajiriwi,” anasema Shauri huku akitolea mfano:“Mimi nawajua vijana wamemaliza shahada ya hesabu, lakini hajawahi kuajiriwa tangu mwaka 2016 hadi walipobahatika kupata shule binafsi.

Hata hivyo, anaeleza wakati mwingine hali hiyo huchangiwa na kutokuwapo kwa msingi mzuri wa masomo hayo tangu ngazi za chini, jambo linalowafanya wanafunzi kuchagua masomo ambayo si ya kuwaumiza kichwa.

“Somo kama fizikia na hisabati ni lazima ujue njia za kufanya tofauti na masomo mengine ambayo mtu anaweza kukariri na akafaulu, sasa kama hakuna msingi mzuri ni tatizo,” anasema Shauri.

Kukosekana kwa unasihi nayo inatajwa kuwa moja ya kukosa mvuto kwa baadhi ya kozi kwa wanafunzi, huku akitaja kuwa hali hii inachochewa na walimu kukosa motisha na kufanya kazi kwa kutimiza wajibu na si wito.

“Walimu wenyewe siku hizi hawajitumi, wanafunzi wanamaliza shule hawajui wanakwenda wapi, hajui anataka kufanya nini, analiza masomo atakapopangiwa ndiyo huko atakwenda. Hii ni tofauti na zamani, wanafunzi walikuwa wanaambiwa ukisoma hivi itakuwa mtu fulani, hivyo kulingana na malengo yake anaweka mkazo huko,” anasema Shauri.

Kwa mujibu wa ripoti za matokeo ya kidato cha nne yanayotolewa na Baraza la Mitihani a Taifa (Necta), hisabati bado ni somo linaloshika mkia kwa kuwa na ufaulu ambao si mzuri.

Mfano, ni asilimia 25.42 pekee ya wanafunzi ndiyo valiopata daraja A hadi D katika mtihani wa hisabati mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko kidogo kutoka asilimia 20.08 mwaka ulitangulia.

Somo la fizikia pia asilimia 71.85 walipata daraja A hadi D katika mtihani wa mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 63.34.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa wachimbaji wa madini mkoani Manyara, Lesebius Msangi anasema mara nyingi ufanyaji kazi na wataalamu wa madini ni gharama na ili kufanya nao kazi ni lazima kuwa na mikataba.

“Kuna wengine mnaingia mkataba kuwa kitakachopatikana mtagawana asilimia ngapi zitakuwa za kwake, lakini kwa wamiliki wakubwa wa migodi wanaajiri watu wao. Ni gharama, si rahisi kwa watu wa chini kumudu gharama hizo kutumia wataalamu.

“Mara nyingi wanaotumika ni watu walewale, ni vigumu kukuta wapya, hasa vijana maana wengi wanataka wenye ujuzi tayari na wanaoweza kuwaamini kwa sababu wamekaa muda mrefu katika nafasi zao,” anasema.

Kinachoweza kufanyika kwa mujibu wa Sekwao ni kufanya mapitio kwa baadhi ya kozi kwa kuangalia ni kitu gani kinaweza kuleta ubora na mvuto ambacho pia kinaweza kuongeza thamani ya wahitimu katika soko la ajira na kujiajiri.

“Mfano wa kozi kama ya biashara watu wanakimbilia kwa sababu wanajua wanaweza kufanya biashara na haina kikomo, wanaweza kutafuta biashara akafanya baada ya kumaliza chuo,” anasema Sekwao na kuongeza;

“Pia kubakisha wastaafu kazini tukiendelea hivi fani itaendelea kudidimia na tunaweza kukosa watu wa madini watabaki wazee. Waliofikia umri wa ustaafu, basi wastaafu ili watoto wetu nao waajiriwe. Mtu umeshafikia umri wanakuonea huruma kwa kukuongeza mkataba,” anaeleza.

Shauri, anatoa rai kwa Serikali kuangalia namna inayoweza kutoa motisha, ikiwemo ajira kwa walimu wa masomo ambayo yana uhaba wa walimu, ili kuchochea ari ya wanafunzi kuweka nguvu kujifunza baadhi ya masomo kuanzia ngazi ya sekondari.