Ajali ya lori, bodaboda ilivyopoteza maisha ya watoto watatu

Lori la mizigo aina ya Faw, mali ya kampuni ya TransAfrica lililogonga bodaboda iliyowabeba watoto watatu na wote kufariki dunia papo hapo.

Muktasari:

  • Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Alfred Mbena amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema ilitokea usiku wa Juni 28, 2024 saa 1 usiku katika eneo la Mlima Ipogoro, kata ya Kitanzini, kwenye barabara kuu ya Iringa – Dodoma.

Iringa. Watu wanne, wakiwamo watoto watatu na dereva wa bodaboda, wamefariki dunia papo hapo mjini Iringa baada bodaboda iliyowabeba watoto hao kugonga lori la mizigo aina ya Faw, mali ya kampuni ya TransAfrica.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 29, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Alfred Mbena amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema ilitokea usiku wa Juni 28, 2024 saa 1 usiku katika eneo la Mlima Ipogoro, kata ya Kitanzini, kwenye barabara kuu ya Iringa – Dodoma.

Kamanda Mbena amesema pikipiki ambayo ilisabisha ajali hiyo, iliyokuwa ikiendeshwa na Hassan Burhan (17), ilitoroshwa muda mfupi mara baada ya ajali hiyo kutokea.

Amesema abiria waliokuwa wamebebwa katika pikipiki hiyo ni Helena Thomas (12), Ally Tenywa (9) na Gabriel Gongo (5), wote wakiwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Ipogoro.

Amesema pikipiki hiyo iligonga ubavuni upande wa kushoto wa gari lenye namba za usajili RAG450N/RL 5167.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa nje ya jengo la kuhifadhia maiti lililopo katika Hospital ya Rufaa Mjini Iringa.

Amesema lori hilo lilikuwa ikitokea Ruvuma kuelekea Dodoma, likiendeshwa na Said Rashid (27), mkazi wa Dar es Salaam na kusabisha vifo kwa watu wanne akiwemo dereva pikipiki na abiria wake wote watatu.

Kamanda huyo ameongeza kuwa kutokana uchunguzi uliofanyika, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa pikipiki kujaribu kulipita lori hilo upande wa kushoto na kuligonga ubavuni na kuanguka na kisha kukanyagwa na magurudumu ya nyuma.

Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, wamesema imetokea baada ya bodaboda huyo kujaribu kupita kwenye upande usio wake na baada kupoteza mwelekeo ndipo lori hilo lilipowagonga.