Wanne wa familia moja wafariki dunia kwa ajali ya gari Korogwe

Ndugu wa familia moja ambao ni wakazi wa Wilaya ya Rombo, waliofariki kwa ajali ya gari walilokuwa wakisafiria wakitokea Harusini mkoani Dar es salaam. Ajali hiyo waliipatia eneo la Bwiko, Korogwe, mkoani Tanga wakienda mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Wanafamilia hao walikuwa wametoka Dar es Salaam kwenye harusi ya ndugu yao, wakirejea nyumbani Rombo mkoani Kilimanjaro, kabla ya kupata ajali katika eneo la Bwiko, Korogwe mkoani Tanga na wanne kupoteza maisha.

Moshi. Watu wanne wa familia moja, akiwemo mama wa bwana harusi, wamefariki dunia kwa ajali ya gari wakitokea harusini jijini Dar es Salaam kuelekea Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia Jumatatu Juni 24, 2024 katika eneo la Bwiko, Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga baada ya gari walilokuwa wakisafiria, aina ya Toyota Noah, kuacha njia na kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa waliokuwemo ndani ya gari hilo.

Alipotafutwa kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi kuzungumzia ajali hiyo, amesema yupo kwenye kikao atafutwe baadaye.

“Nipo kwenye kikao, naomba unitafute baadaye,” amesema Kamanda Mchunguzi.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu hao, Fredrick Michael amesema wanafamilia hao walifariki kwa ajali njiani  wakati wakitoka Dar es Salaam kwenye harusi ya ndugu yao ambayo ilifanyika Jumamosi Juni 22, 2024.

Amewaja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni mama mzazi wa bwana harusi, Cecilia Luka na dada yake, Antonio Luka pamoja na ndugu wawili wa bwana harusi ambao ni Godfrey Michael na Judith Michael.

“Hawa ndugu zangu, walikuwa kwenye harusi ya mdogo wetu, Dar es Salaam, ambayo ilifanyika Jumamosi na baada ya kumalizika kwa harusi, kesho yake walianza safari ya kurejea nyumbani Rombo mkoani Kilimanjaro, lakini walipofika eneo la Bwiko, Korogwe, walipata ajali mbaya baada ya gari walilokuwa nalo kupinduka.

“Na katika ajali hiyo, nimempoteza mama yangu mzazi, mama mkubwa, dada yangu na kaka yangu. Kwa kweli huu ni msiba mzito ambao umetuumiza sana, tunaomba Mungu atutie nguvu na kutufariji,” amesema Michael.

Amesema tayari wamemzika dada yao katika eneo la Kileo wilayani Mwanga alikoolewa na kwamba mama yao mzazi na ndugu hao wengine wawili watazikwa katika makaburi ya familia, yaliyopo katika kijiji cha Samanga, Kata ya Kirongo Samanga, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro.

Diwani wa Kata ya Kirongo Samanga, Prisila Shayo amesema wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za vifo vya wanafamilia hao kwa kuwa ndugu hao waliondoka kwa pamoja kwenda kwenye sherehe ya harusi ya ndugu yao.

“Hapa kwetu tumepata msiba mzito, ndugu wanne wa familia moja wote wamefariki wakitoka kwenye harusi, yaani mama wa bwana harusi na dada yake pamoja na watoto wake wawili wamefariki, ni pigo kubwa kwa familia hii,” amesema.