Vilio vyatawala maziko ya baba, wanawe watatu waliofariki kwa ajali ya moto

Sheikh wa mkoa wa Arusha, Shaaban Bin Juma (aliyeshika kipaza sauti), leo Juni 24, 2024  akiongoza ibada ya kuaga miili ya watu wanne akiwemo Zuberi Msemo na watoto wake watatu waliofariki kwa ajili ya moto juzi, wakiagwa katika eneo la Ol Matejoo, Arusha kabla ya kwenda kuwazika kijijini kwao wilayani Mwanga, Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Ajali hiyo ya moto ilitokea Jumamosi, Juni 22, 2024 eneo la Olmatejoo, Mkoani Arusha na kusababisha vifo vya watoto watatu na baba yao.

Arusha. Simanzi na majonzi vimetawala katika Kijiji cha Shighatini, Wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya miili minne ukiwemo wa aliyekuwa mtumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Zuberi Msemo ilipowasili nyumbani kwao kwa ajili ya maziko.

Zuberi na wanawe watatu, Mariam (9), Salma (7) na Bisma (3), walifariki dunia baada ya ajali ya moto iliyotokea Jumamosi, Juni 22, 2024 jijini Arusha.

Ajali hiyo ilitokea Mtaa wa Olmatejoo na ilisababishwa na kompyuta mpakato iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme kushika moto na kuunguza kochi.

Leo Jumatatu Juni 24,2024 miili ya marehemu hao iliwasili kijijini hapo saa sita mchana kwa magari maalum ya Tanapa na kuzikwa saa 10 jioni katika makaburi ya familia yaliyopo Kitongoji cha Lomboni.

Marehemu Msemo alikuwa anafanya kazi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika kitengo cha Tehama (ICT) na alirejea mkoani Arusha ilikokuwa familia yake kwa ajili ya kumpongeza mke wake aliyekuwa amejifungua siku chache zilizopita.

Watoto wake watatu walipoteza maisha papo hapo wakati moto ukiendelea kuteketeza nyumba yao, huku Msemo akifariki dunia Juni 23, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, Mkoani Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya aliyeongoza mamia ya waombolezaji katika maziko hayo, aliomba wananchi kuendelea kuwaombea majeruhi na zaidi mke wa marehemu aliyesema anapitia kipindi kigumu.

Katika tukio hilo mke wa marehemu Jasmine Khatibu ambaye ana mtoto mchanga aliyejifungua hivi karibuni,  ni miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo.

Wengine ambao wamelazwa hospitali wakiendelea kupatiwa matibabu ni mama mzazi wa Msemo, Mariam Mussa, Mwanaidi Aldina (dada wa marehemu), Mussa Msemo (mdogo wa marehemu), AbdulKarim Ramadhan (mtoto wa kaka wa marehemu) na mfanyakazi wa ndani aliyefahamika kwa jina moja la Ester.

Akizungumza na Mwananchi mapema asubuhi leo, msemaji wa familia, Yahya Msemo alisema Jasmine na mama mkwe wake wameruhusiwa kuhudhuria maziko na wanatakiwa kurudi hospitali baada ya kumalizika maziko hayo.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mount Meru, Dk Kipapi Mlambu, alisema mke na mama wa marehemu wanahitajika kukaa kwa muda hospitali kwa ajili ya tiba ya akili.

"Msiba huu umewashtua, hivyo wanahitaji huduma ya ushauri, ili kuwarudisha katika hali zao za kawaida," amesema.


Miili yaagwa Arusha

Awali,  Kamishna mstaafu wa Uhifadhi wa Tanapa, Dk Allan Kijazi na Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Shaban Bin Juma, waliongoza mamia ya waombolezaji kuaga miili hiyo katika ibada fupi iliyofanyika nyumbani kwao eneo la Olmatejoo.

Akitoa salamu kwa niaba ya Tanapa, Dk Kijazi amesema Shirika limepoteza nguvu kazi kubwa kwa sababu marehemu alifanya kazi kwa kipindi kirefu na kuwa kupitia tukio hilo, kuna mengi ya kujifunza kwake.

“Nikiwa kiongozi wao mstaafu, wameniomba kwa heshima kubwa nitoe salamu kwa niaba ya shirika.Tulipokea taarifa hizi kwa mshtuko mkubwa, mimi niliona mara ya kwanza  jana asubuhi kwenye mitandao na nikawa siamini kilichotokea,” amesema Dk Kijazi.

Amesema tukio hilo ambalo si la kawaida kutokea, limeacha pengo kubwa kwa wafanyakazi wa shirika hilo ambao marehemu amekuwa akifanya nao kazi, huku akifariki na watoto wake watatu.

“Hakika ni tukio la kuhuzunisha lakini haya yote nadhani sisi kama binadamu tumtegemee Mwenyezi Mungu na liwe fundisho kwetu tuna mengi ya kujifunza kutokana na tukio hili, kikubwa tutaendelea kuwa karibu na wanafamilia,” amesema Dk Kijazi.

Diwani wa Kata ya Sombetini, jijini Arusha ambaye pia ni mwanafamilia, Bakari Msangi, ameishukuru Serikali na wananchi waliojitolea tangu tukio hilo lilivyotokea.

“Tunaishukuru Serikali, Tanapa na wananchi kwa kiasi kikubwa walivyojitolea kushiriki nasi katika msiba huu ambao umekuwa mkubwa mno kwa familia, kwa kweli imetuumiza ila  kazi ya Mungu tunaamini haina makosa,” amesema Msangi.

Juzi, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji mkoani Arusha, Jeradi Nonkwe, alisema chanzo cha moto huo uliosababisha vifo na majeruhi ni kompyuta mpakato iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme kushika moto na kuunguza kochi.

Amesema moto huo ulisababisha vifo vitatu vya papo hapo vya watoto hao na kujeruhi watu wengine wanane kabla ya baba naye kufariki dunia jana alfajiri.