Mwanamke aliyefiwa na mumewe, watoto watatu ajali ya moto Arusha atoka hospitali

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa (mwenye kofia) akiwa amem'beba mtoto mchanga aliyenusurika kwenye ajali ya moto, iliyoua watu wanne akiwemo baba na watoto watatu. Pembeni aliyelala ni mke wa marehemu, Jasmine Khatibu.

Muktasari:

  • Watu saba walinusurika, akiwemo mama wa marehemu na kaka yake ambaye bado anaendelea na matibabu.

Arusha. Hatimaye Jasmine Khatibu na mtoto wake mchanga mwenye umri wa wiki moja, wameruhusiwa kutoka hospitali baada ya kupata nafuu.

Jasmine pamoja na mtoto wake mchanga wameruhusiwa kurudi nyumbani kutoka Hospitali ya Rufaa Mount Meru walikokuwa wakipatiwa matibabu baada ya kunusurika katika ajali ya moto iliyotokea Juni 22, 2024 ambayo ilisababisha kifo cha mumewe Zuberi Msemo pamoja na watoto wake watatu--- Mariam, Salma na Bisma.

Chanzo cha moto huo ulitokea nyumbani kwake Olmatejoo jijini Arusha, kimetajwa kuwa ni kompyuta mpakato (laptop) iliyokuwa imechomekwa kwenye soketi ya umeme kushika moto na kuunguza kochi.

Katika ajali hiyo, watu saba walinusurika akiwemo mke wa marehemu (Jasmine) na mwanawe mchanga. Pia mama wa marehemu, Mariam Mussa, dada, kaka na mfanyakazi wa nyumbani.

Akizungumzia leo Jumatano Juni 26, 2024. msemaji wa familia, Yahya Msemo amesema wanamshukuru Mungu mke wa marehemu  ameruhusiwa kutoka hospitali na mtoto wake wakiambatana  pia na dada wa marehemu (Mwanaidi) na mfanyakazi wa nyumbani, Esta Yohana.

"Kwa sasa mama wa marehemu (Mariam) anaendelea na matibabu kutokana na shinikizo la damu kupanda, lakini pia anahitaji zaidi huduma za ushauri (cancelling) kutokana na mshtuko wa ajali hiyo," amesema Msemo.

Amesema pia kaka wa marehemu, Mussa Msemo bado anaendelea na matibabu kutokana na majeraha ya kuungua moto maeneo mbalimbali mwilini, ikiwemo paji la uso, mikono na muguu.