Ajali ya basi Kibaha manusura wasimulia hofu kabla ya ajali
Basi la kampuni ya A.M lililokuwa likitoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam likiwa limepinduka maeneo ya Mailimoja, Kibaha, leo Jumamosi Mei 23, 2026, na kusababisha majeruhi wawili. Picha na Sanjito Msafiri.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika huku dereva wa basi hilo akitoroka eneo la tukio na msako wake ukiendelea.
Kibaha. Baadhi ya abiria walionusurika katika ajali ya basi la kampuni ya A.M wamesema walisafiri kwa hofu na mashaka baada ya magari waliyopanda kuonyesha hitilafu mara kwa mara kabla ya ajali kutokea.
Ajali hiyo imetokea leo Mei 23, 2026 maeneo ya Njuweni, wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Ajali hiyo iliyohusisha basi aina ya Yutong lililokuwa likitoka Kigoma kwenda Dar es Salaam, imesababisha majeruhi wawili ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika huku dereva wa basi hilo akitoroka eneo la tukio na msako wake ukiendelea.
Akizungumza baada ya ajali, mmoja wa abiria walionusurika, Bakari Athumani, amesema safari yao ilianza Kigoma jana lakini tayari walikumbana na changamoto njiani baada ya basi la awali kuharibika mara kwa mara kabla ya kuhamishiwa kwenye lingine Dodoma.
“Tulitoka Kigoma jana, gari tulilopanda lilikuwa linaharibika kila mara njiani. Tulipofika Dodoma tukabadilishiwa na kupanda hili ambalo leo limepata ajali,” amesema Bakari.
Naye manusura mwingine, Faraji Juma, amesema hata basi walilohamishiwa lilikuwa na hitilafu za kiufundi na lilisafiri likiyumba na kudunda, hali iliyowapa hofu abiria wote.
“Hata hili tulilopata ajali nalo lilikuwa linatusumbua njiani, lilikuwa linadunda dunda na kuyumba yumba. Tumesafiri kwa mashaka sana,” amesema Faraji.
Kwa mujibu wa polisi, majeruhi wa ajali hiyo ni Mashaka Kitundu (53), mkazi wa Dodoma aliyepata maumivu ya tumbo na mbavu, pamoja na Anna Mashamva (30), mkazi wa Itigi mkoani Singida aliyepata maumivu ya bega la mkono wa kushoto.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo huku msako wa dereva aliyekimbia ukikiendelea.