Aina za mabosi na namna ya kuendana nao kazini

Muktasari:
- Moja ya vitu vinavyowapa shida waajiriwa ni mabosi wao hasa pale ambapo matarajio yao hayaendani na tabia za mabosi wao. Hiki ni chanzo cha msongo wa mawazo katika maeneo ya kazi kinachosababisha wengi kushindwa kufurahia maisha yao kazini.
Moja ya vitu vinavyowapa shida waajiriwa ni mabosi wao hasa pale ambapo matarajio yao hayaendani na tabia za mabosi wao. Hiki ni chanzo cha msongo wa mawazo katika maeneo ya kazi kinachosababisha wengi kushindwa kufurahia maisha yao kazini. Kwa upande mwingine wapo ambao wanaishi vyema na mabosi wao kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa katika maeneo ya kazi. Leo tutaangalia aina za mabosi na jinsi unavyoanaweza kuendana nao:
Wapenda madaraka
Mabosi wapenda madaraka hujawa kiburi na dharau na kuwaona wengine hasa wanaowaongoza si lolote si chochote. Wapo radhi kutoa maneno ya kuwadharirisha wengine mbele ya watu bila kujali chochote. Njia bora ya kuepuka madhara yatokanayo na maneno na matendo yao ni kufuata kanuni na taratibu huku busara ya kiwango cha juu ikitumika katika kuhusiana nao.
Watafuta ukamilifu
Mara nyingi hawa hawana shida ya moja kwa moja kimahusiano ndani ya maofisi lakini shida yao moja ni kutaka kila kitu kiende kama kilivyo pangwa. Hukerwa sana na watu wasiofuata utaratibu, wasiotunza muda na wanaofanya mambo bila maandalizi ya kutosha. Mabosi hawa hutamani kila mtu afuate sheria, miongozo, kanuni na taratibu. Ili kuzuia migogoro isiyo ya lazima ni lazima kuhakikisha unafuata taratibu na kanuni za kazi yako.
Walalamishi
Hawa ni wale wenye sifa za kulalamika sana. Muda wote wao ni kupiga kelele na kutafuta nani wa kumlaumu hata kwa makosa yao wenyewe. Wakikuita ofisini lazima ujiulize kwanza hivi ni kosa gani umefanya, unaweza hata kujitathmini namna ulivyo vaa kabla ya kwenda kuwaona. Kwa sababu hawanaga dogo hakikisha unajiridhisha kwa kila unachotaka kufanya na hata kwa kwa kuuliza wengine.
Wahamasishaji
Hawa wanaimani kuwa mafanikio ya taasisi ni matokeo ya ushawishi wao na uwezo wa wafanyakazi kufanya majukumu yao ipasavyo. Hivyo hutumia muda mwingi kuwatia moyo watu na kuwakumbusha majukumu yao. Ni watu wanaopenda kujua maendeleo ya kila shughuli inayofanyanyika ili kuweka chachu ya hamasa katika kufanikisha malengo ya taasisi. Kwa sababu ni watu wanaopenda kufuatilia mambo, ili kuepuka migogoro ni vyema kuwapa taarifa za maendeleo ya kazi mara kwa mara.
Watu wa watu
Hawa ni wale ambao kila mtu angependa kufanya kazi nao. Wanachukulia taasisi kama familia na wanafanya jitihada kuhakikisha hakuna mwanafamilia yoyote anayekuwa na shida na isipewe uzito. Hawapendi kuona migogoro ikiendelea ndani ya taasisi na ni watu wa kujichanganya. Kuendana na watu wa aina hii ni rahisi lakini mtu akitumia sifa zao njema kama kigezo cha kufanya anavyotaka haimaanishi kuwa watamchekea hivyo ni vyema kufurahia mazingira haya mazuri huku ukiwajibika na kujua mipaka yako.