AI isitumike kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, Rodney Mbuya, akizungumza na wandishi wa Habari
Muktasari:
- Akili Mnemba ni mifumo ya kompyuta yenye uwezo wa kutekeleza kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili ya binadamu
Dar es Salaam. Vyombo vya habari vimetakiwa kuwa makini na kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (AI) kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo, Rodney Mbuya alipokuwa akizungumzia maadhimisho Siku ya Uhuru wa Vyombo ya Habari yanayotarajiwa kuadhimishwa Aprili 29, 2025.
Maadhimisho hayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika jijini Arusha huku kaulimbiu yake ikiwa ni 'Uhabarishaji kwenye dunia mpya: Mchango wa akili mnemba kwenye uhuru wa vyombo vya habari'.
Mbuya amesema kutokana na kaulimbiu hiyo inafundisha kuhusu ulimwengu mpya unaoendeshwa na AI ambapo vyombo vya habari vinatakiwa kuwa makini kwa kutumia teknolojia hiyo.
"Kaulimbiu hii inatoa changamoto kwa waandishi ,wamiliki wa vyombo vya habari na serikali kuhakikisha kwamba AI inasaidia badala ya kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya watu kupata habari sahihi,amesema Rodney ambaye katika mkutano alikuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo, Mkurugenzi huyo amesema yanatoa nafasi kwa wadau sekta ya habari,mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia kujadili masuala muhimu yanayohusu habari na changamoto zinazohusiana na teknolojia.
Kwa upande wake Ofisa Programu wa taasisi ya Jamii Africa, Melba Sandi, ambao ndio mwenyekiti wa maadhimisho hayo kwa mwaka huu, amesema mikutano itaanza Aprili 27 hadi 28 ikiwa ni utangulizi kuelekea kilele cha maadhimisho hayo itakayokuwa Aprili 29,2025.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na katika siku zote hizo kutakuwepo na utoaji wa mada mbalimbali,majadiliano na maonyesho kuhusu tasnia ya habari na teknolojia.
Naye Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa, Susan Namondo, amesema maadhimisho hayo yatatumika kama fursa ya kuweka mkazo mkubwa katika uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binadamu.
"Siku hii itatumika pia k kuangazia uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki zingine,"amesema Susan ambaye alikuwa pia akiwakilisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).