Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kisa kuua watoto watatu

Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyofanya kikao chake mkoani Njombe imemuhukumu Joel Nziku kunyongwa hadi kufa, kwa kosa la kuwaua watoto watatu wa baba yake mdogo.
Muktasari:
- Jaji Mrisha amesema mshitakiwa huyo alikwenda nyumbani kwa baba yake mdogo na kuwachukua watoto watatu ambao aliwapakia kwenye lori na baadae aliwaua kwa kuwapiga na kitu kizito na kisha kuitelekeza miili katika maeneo tofauti.
Njombe. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa iliyofanya kikao chake mkoani Njombe imemuhukumu Joel Nziku kunyongwa hadi kufa, kwa kosa la kuwaua watoto watatu wa baba yake mdogo.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Aboubakar Mrisha amesema mshitakiwa huyo alitekeleza mauaji hayo mwezi Januari mwaka 2019 katika Kijiji cha Ikando, Kata ya Kichiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Jaji Mrisha amesema mshitakiwa huyo alikwenda nyumbani kwa baba yake mdogo na kuwachukua watoto watatu ambao aliwapakia kwenye lori na baadae aliwaua kwa kuwapiga na kitu kizito na kisha kuitelekeza miili katika maeneo tofauti.
Amebainisha kuwa katika maelezo yaliyotolewa na mshitakiwa yameeleza kuwa alikuwa na mgogoro na baba yake mdogo Danford Nziku ambaye ndiye baba mzazi wa watoto watatu waliouawa ambao ni Giliad Nziku, Gaspa Nziku pamoja na Godliver Nziku.
Amesema pamoja na mshtakiwa kukana kuhusika na mauaji pamoja na kukana kutowafahamu watoto waliouawa, mahakama imesema kupitia vielelezo na mashahidi tisa walioapa na kutoa ushahidi mahakamani hapo, mahakama hiyo imemkuta mshitakiwa na hatia ya mauaji.
"Kosa lililofanywa na mshtakiwa huyo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022," amesema Mrisha.
Jaji Mrisha amesema mahakama hiyo imemuhukumu Joel Nziku kunyongwa hadi kufa na gari lililotumika katika mauaji hayo litaifishwe na kuuzwa kupitia mnada na pesa ziwekwe kwenye akaunti ya Serikali.
Kesi hiyo namba 108 ya mwaka 2021 imesimamiwa na mawakili wa serikali ambao ni Pienzie Nichombe, Magdalena Whero pamoja na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Dhamiri Masinde wakati upande wa utetezi ukisimamiwa na Wakili Alex Mgani.