Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahadi ya gridi ya taifa ya maji ilivyoanza kutekelezwa siku 100 za Rais Samia

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Mradi huo unalenga kuunganisha vyanzo vikubwa vya maji na kusambaza maji nchi nzima. Hatua za awali zimefikiwa ikiwemo kukamilika kwa usanifu wa mradi wa Ziwa Victoria–Dodoma, huku wananchi wakionesha matumaini na wasiwasi kuhusu mwendelezo wake.

Dar es Salaam. Wakati siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani zikikaribia kutimia, sekta ya maji nchini imeanza kuonesha mwelekeo mpya, kutokana na ahadi ya mkuu huyo wa nchi ya kuanzisha utekelezaji wa gridi ya taifa ya maji.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Rais Samia aliahidi kuanzisha gridi ya taifa ya maji. Gridi hiyo ni jambo jipya hapa nchini, kwani Tanzania ina vyanzo tofauti vya maji ambavyo vinahudumia maeneo husika, lakini hakuna mfumo mmoja wa kusambaza maji nchi nzima kama ilivyo kwenye Gridi ya Taifa ya Umeme.

Gridi ya taifa ya maji ni mpango wa Serikali wa kuunganisha vyanzo vikubwa vya maji (mito, maziwa, mabwawa, visima vikubwa) na kuyasambaza kwenda mikoa, wilaya na miji mingi kwa mfumo mmoja, badala ya kila eneo kujitegemea chanzo chake pekee.

Mradi huo unaolenga kusambaza maji kutoka vyanzo vikubwa na vya uhakika kwenda maeneo yenye uhaba wa maji nchini, huku ikitarajiwa kuwa na mfumo wa pamoja wa usambazaji maji nchi nzima.

Itakumbukwa kwamba baada ya kuingia madarakani, Novemba 3, 2025, miongoni mwa mambo aliyoahidi Rais Samia kuyafanya katika siku 100 za kwanza ni kuanza utekelezaji wa mradi wa gridi hiyo.

Alisema wataanza utekelezaji huo ndani ya siku 100 kwa lengo la kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kilimo, mifugo na biashara.

Alisisitiza kwamba gridi hiyo itahusisha vyanzo vikubwa kutoka Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa pamoja na mito mikubwa nchini.


Utekelezaji ulipofika

Mpaka sasa, moja ya hatua muhimu zilizofikiwa ni kukamilika kwa usanifu wa mradi wa kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida, unaojulikana kama Lake Victoria–Dodoma (LVD) Project.

Malengo mahsusi ni kupunguza uhaba wa maji, kuwezesha miji kukua bila kukosa maji, na kuhakikisha maji yanapatikana hata wakati wa ukame.

Utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa awamu kadhaa, kwa mujibu wa Serikali, awamu ya kwanza ni kujenga na kukarabati vyanzo vikubwa vya maji, kujenga mabomba makuu na kuunganisha miradi iliyokuwa imekwama.

Awamu ya pili itahusisha kuunganisha miji na wilaya jirani kutoka chanzo kimoja, kusambaza maji kutoka mijini kwenda vijijini, na awamu ya tatu (inaendelea) itahusisha kupanua mtandao ili kufikia maeneo zaidi.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, anasema wizara hiyo imeanza utekelezaji wa gridi ya taifa ya maji kwa kuandaa miradi mikubwa ya kuchukua maji kutoka maziwa makuu na mito mikubwa, na kuyasambaza kwa mabomba makuu kwenda maeneo yenye ukame na yale yenye uhaba wa maji.

“Usanifu wa mradi huu umekamilika na kwa sasa taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea. Huu ni mradi mkubwa utakaosaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa adha ya maji katika Kanda ya Kati,” anasema Aweso.

Anaongeza kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi mingine mikubwa inayohusisha Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa pamoja na mito mikuu kama Rufiji na Ruvuma umefanyika katika hatua mbalimbali, hatua inayoweka msingi wa utekelezaji wa gridi kwa awamu.


Maeneo yanayonufaika

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, anasema, “Kama alivyosema Waziri (Aweso), lengo ni kuhakikisha hakuna mkoa unaoachwa nyuma katika upatikanaji wa maji safi na salama.”

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mradi huo unatarajiwa kusaidia pia vijiji vya mbali ambavyo havijafikiwa na mtandao wa kawaida wa maji, kwa kuweka mabomba makuu yatakayounganishwa na mifumo ya usambazaji ya ndani.


Mwelekeo wa kitaifa

Wakizungumzia mradi huo, baadhi ya wananchi wameonesha mtazamo tofauti juu ya kuanza kwa gridi ya taifa, baadhi wakieleza kwamba utakuwa mwarobaini wa tatizo la maji nchini, huku wengine wakidhani hautasaidia kama hakuna utashi wa kumaliza changamoto hiyo.

Mkazi wa Kimara, Dar es Salaam, Nelson Jumanne, anasema kuanza kwa utekelezaji wa gridi ya taifa ya maji ndani ya siku 100 za Rais Samia ni ishara kuwa mkakati huo si wazo la kisiasa bali ni ajenda ya kitaifa.

“Utekelezaji usiishie njiani au ukawa na nguvu ya soda, usimamiwe ipasavyo na ufanyike na kumalizika kwa wakati, hapo ndipo utakuwa na impact (matokeo). Wananchi tunataka maji saa 24,” anasema kijana huyo.

Anaongeza kuwa vijijini wana changamoto kubwa zaidi ya maji kuliko mijini, hivyo nao wakumbukwe kwenye mradi huu ili kila Mtanzania, popote alipo, apate uhakika wa maji safi ya kunywa na matumizi mengine ya nyumbani.

Kwa upande wake, mkazi wa Dodoma, Jane Jerome, anasema kama mradi huo utafanyika bila urasimu, utapunguza adha ya maji kwenye maeneo mengi nchini na kuboresha maisha ya wananchi.

“Natamani kuona Serikali inaweka mifumo ya kisheria, kiutawala na kifedha ili kuhakikisha gridi hiyo inakuwa mradi wa taifa, unaoendelea hata pale uongozi unapobadilika,” anasema mwanamke huyo.

Naye, Anita Sumi, mkazi wa Kisarawe mkoani Pwani, anasema kuanza kwa utekelezaji wa gridi ya taifa ya maji ndani ya siku 100 ni hatua, japo wasiwasi wake ni namna mwendelezo wake utakavyokuwa.

“Tunatamani kuona lini maji ya gridi yataanza kutiririka kwenye mabomba yetu. Kero ya maji imekuwa kubwa na hatujui kama hiyo gridi itakuwa mwarobaini au la,” anasema mkazi huyo wa Kisarawe.


Fundi bomba afafanua

Mmoja wa mafundi bomba nchini, Albert Makasi, anasema ujenzi wa gridi ya taifa ya maji, mbali na kuwapatia Watanzania uhakika wa maji, pia utachochea fursa ya ajira kwa mafundi hao ambao wengi wao ni vijana.

“Siku hizi ajira hakuna na sisi mafundi bomba tunatafuta kazi za kufanya lakini hakuna. Hii itakuwa ni fursa kwetu kupata kazi za kufanya ili tupate fedha za kuendesha maisha yetu ya kila siku,” anabainisha kijana huyo mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es Salaam.