Rais Samia kushiriki mkutano wa Dunia Dubai
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiagana na viongozi wakati akiondoka nchini kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) leo Februari 2, 2026.
Muktasari:
- Ziara hii inalenga kuvutia mitaji, kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, na kuendeleza miradi ya kimkakati katika sekta za nishati, miundombinu, kilimo, viwanda, teknolojia na usafirishaji.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Dunia wa Serikali (World Governments Summit – WGS) 2026 pamoja na uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), itakayofanyika Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
Mkutano wa WGS 2026, unaobeba kaulimbiu ‘Kutengeneza Serikali zijazo (Shaping Future Governments)”, ni jukwaa la kimataifa linalowakutanisha wakuu wa nchi na serikali, watunga sera, viongozi wa taasisi za kimataifa, sekta binafsi na wawekezaji wakubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Ushiriki wa Rais Samia katika mkutano huo unaweka mkazo katika diplomasia ya uchumi, huku lengo kuu likiwa ni kuoanisha sera za maendeleo ya Tanzania na mwelekeo wa mitaji ya kimataifa na kuharakisha uwekezaji unaochochea ajira na ukuaji wa uchumi.
Sambamba na WGS, Rais Samia atashiriki uzinduzi wa Global Africa Investment Summit (GAIS), jukwaa la kimkakati la uwekezaji lililoanzishwa na Rais mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina, kwa kushirikiana na wadau wa kimataifa.
GAIS inalenga kuunganisha miradi yenye tija barani Afrika na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha.
Katika kipindi cha mkutano huo, Rais Samia anatarajiwa kufanya mazungumzo ya kiserikali na viongozi wa nchi mwenyeji, Falme za Kiarabu, na kukutana na viongozi wa taasisi za fedha za kimataifa na wawekezaji wakubwa, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja nchini.
Ushiriki wake huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) pamoja na Sera Mpya ya Mambo ya Nje, ambazo zinatilia mkazo diplomasia ya kiuchumi kama nguzo kuu ya mahusiano ya kimataifa ya Tanzania.
Ziara hii ya kimataifa ya Rais Samia ni ya kwanza tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, na inatoa ujumbe wa uthabiti wa kisiasa, mwendelezo wa sera, na dhamira ya Tanzania katika kuvutia mitaji ya uwekezaji kutoka nje.
Katika WGS 2026, Rais Samia anatarajiwa kushiriki mjadala wa wakuu wa nchi na serikali wenye mada “Serikali na mustakabali wa uwekezaji: Mtazamo wa Afrika”, pamoja na Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, João Lourenço; Rais wa Ghana, John Dramani Mahama; na Dk Akinwumi Adesina.
Mjadala huo unalenga kujadili mwelekeo mpya wa maendeleo ya kiuchumi barani Afrika, namna ya kuhamasisha uwekezaji wa kimataifa na kuharakisha mabadiliko ya bara kutoka utegemezi wa misaada kwenda ukuaji unaoongozwa na uwekezaji.
Kwa Tanzania, majukwaa ya WGS na GAIS yanatoa fursa ya kuwasilisha miradi ya kimkakati katika sekta za nishati, miundombinu, kilimo-biashara, viwanda, teknolojia na usafirishaji, kwa lengo la kupata matokeo ya haraka yanayochangia ajira, mapato na maendeleo endelevu.