Prime
Agizo la polisi lazua maswali

Moshi/Dar. Nini kipo nyuma ya kuitwa na kuhojiwa kwa mawakili, wanaharakati na watu wengine maarufu waliokosoa kwa hisia kali mkataba kati ya Tanzania na Dubai juu ya uwekezaji na uendelezaji bandari nchini?
Hili ndilo swali linalogonga vichwa vya watu wengi, huku Jeshi la Polisi likifafanua sababu za kuchukua hatua ambazo pia zinakosolewa kwa ukiukaji uhuru wa kujieleza.
Kufuatia hatua hiyo, mawakili, wanaharakati na wananchi wa kawaida waliozungumza na Mwananchi wameonya kama mijadala kuhusu uwekezaji huo haitafanyika kwa staha na kuvumiliana, inaweza kutishia umoja na mshikamano wa Watanzania.
Katikati ya mjadala huo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Ramadhan Kingai amefafanua kuwa wanaoitwa kuhojiwa na polisi “ni wale ambao matamshi yao yana viashiria vya uchochezi na matumizi ya lugha za kifedhuli na kutukana viongozi”.
Lakini kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema kinachofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya wanasheria na wanaharakati hao ni “kuzuia uhuru wa wananchi kujieleza na kutoa maoni yao juu ya rasilimali zao, kitendo ambacho ni kinyume cha Katiba ya Tanzania”.
Wakati wawili hao wakisema hivyo, Wakili David Shillatu ambaye pia ni kiongozi wa chama cha mawakili nchini (TLS) kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga, ameshauri matamshi ya mawakili na wanaharakati waliopewa wito wa polisi, yatazamwe kama maoni yao binafsi.
Miongoni mwa walioitwa na Polisi ni mawakili Dk Rugemeleza Nshala, Tundu Lissu waliowahi kuwa Rais wa chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi pamoja na mwanaharakati Mdude Nyagali.
Dk Nshalla na Lissu bado hawajahojiwa kwa kuwa wako nje ya nchi, wakati Mwabukusi na Mdude wamehojiwa na wako nje kwa dhamana.
Ingawa kukamatwa kwa Wakili Peter Madeleka jijini Arusha baada ya makubaliano yake ya kukiri kosa aliyoingia na DPP kufutwa na mahakama hayana uhusiano na sakata hilo la bandari, wanaharakati na mijadala katika mitandao wanahusianisha masuala hayo mawili.
Mara tu baada ya makubaliano hayo kufutwa ili kesi yake isikilizwe upya kama ilivyoamuriwa na Mahakama Kuu Julai 18, Madeleka alitiwa nguvuni na akafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa makosa ya uhujumu uchumi yenye maudhui yanayofanana na aliyokuwa amekubaliana na DPP.
Kati ya mwaka 2016 na mwaka 2017 wakati wa Serikali ya awamu ya tano, Lissu alifunguliwa kesi tano za jinai zote zikihusu makosa ya uchochezi na baadaye zote zilifutwa.
Maagizo ya Masauni
Akihojiwa na gazeti hili jana, DCI Kingai alisema jeshi hilo linatekeleza maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi aliyetaka watu wote wanaotumia vibaya uhuru wa maoni kuhatarisha amani na utulivu wachukuliwe hatua za kisheria.
“Sisi hatujawaita watu kuwahoji kwa ajili ya mkataba, umma ukae ukielewa hivyo, isipokuwa tunatekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa uhuru kweli wa kutoa maoni, lakini hakuna mtu ambaye anaruhusiwa kuvuka mipaka,” alisema DCI Kingai.
"Uhuru wako unaanzia pale wa mwenzako unapoishia, sisi tunachowaitia watu ni kitu tofauti na mkataba. Watu wazungumze wanachozungumza lakini sisi tunasimamia sheria kwa vile vitu vinavyohatarisha amani.
“Ndicho ambacho tunakiangalia na si wote wameitwa, mbona waliotoa maoni kuhusu huo mkataba ni wengi sana. Watu wajiulize kwa nini waitwe hawa wachache tu,” alihoji Kingai, akiwalenga mawakili hao watatu pamoja na Mdude.
“Tunachowaitia ni mambo ambayo tunaona kabisa yana element (viashiria) za kijinai na ambazo tunapaswa kuwahoji na kupata maelezo yao kuona na kupima kama kuna hatua za kisheria tunaweza kuzichukua,” alisisitiza Kingai.
DCI Kingai alisema umma uelewe kuwa wanaitwa kwa sababu za kijinai ambazo jeshi hilo limeona, kwamba kuna lugha wamekuwa wakizitoa na wengine (wanazitoa) ilimradi waonekane wanazungumza.
"Watu wanaongea lugha za kiuchochezi, za kifedhuli, lugha ambazo ni za matusi na lugha nyingine ambazo tunapaswa kuwaita. Kwa mfano, wanatukana viongozi, sisi tukiwa watu tunaosimamia sheria tukikaa kimya tutakuwa hatujafanya sawasawa,” alisema.
Kingai alifafanua kuwa pale wanapoona mtu anavuka mpaka, tofauti na sheria inavyotaka, ni lazima wamuite kumhoji na kuona kama kuna haja ya kuchukua hatua za kisheria pale wanapokusanya ushahidi usioacha shaka.
Alisema wito wa polisi ni wa kisheria na watu hawapaswi kuwa na taharuki, isipokuwa wanataka kujiridhisha na maneno wanayoyazungumza.
Kiongozi huyo namba moja katika upelelezi wa jinai nchini, alisema “jeshi linataka watu wawe na uhuru wa kuzungumza na wazingatie staha, si kutukana viongozi kwa sababu katika mkataba ule hakuna kitu kinaitwa matusi wala uchochezi”.
Alipoulizwa kama kuna watu wengine ambao Jeshi hilo lina mpango wa kuwaita kuwahoji, alisema hiyo ni siri yao na hawawezi kuweka wazi lakini “waliotoa lugha za kifedhuli ni lazima wataitwa kuhojiwa”.
Alipoulizwa iwapo Dk Nshala aliitikia wito baada ya kupewa taarifa, Kingai alisema kwanza walipata taarifa kwamba hakuwepo nchini, kwa hiyo wanamsubiri kwa kuwa wana uhakika wito huo umekwishamfikia.
"Wito wa polisi ni wa kisheria, ukiangalia kifungu cha 10 (2) (A) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai kinatoa mamlaka kwa polisi kumuita mtu ambaye wanajua kabisa kuna jambo na huyo mtu analifahamu kwa ajili ya ushahidi,” alisema DCI Kingai.
Pia alisema wamepewa mamlaka ya kumuita mtu iwapo watabaini kuna kitu kinaweza kutumika kama kielelezo kwa shauri la jinai lililopo polisi na akakiwasilisha na kikatumika na asipofanya hivyo anaweza kushtakiwa.
Kuminya uhuru
Mkurugenzi wa Jukata, Bob Wangwe alisema katika ufafanuzi wake kuwa kinachofanywa na jeshi hilo ni kuzuia uhuru wa wananchi kujieleza na kutoa maoni juu ya rasilimali zao.
“Ungetarajia kuona nguvu ya kujibu hoja zao (wakosoaji wa mkataba) ikitumika, lakini imekuwa kinyume chake, kwamba inatumika hoja ya nguvu, kitu ambacho kinaenda kinyume na kinachoitwa zile 4R za Rais Samia Suluhu Hassan,” alidai.
Alisema hali hiyo inaonyesha kwamba nguvu kubwa inatumika katika kuziba hoja au kuwazuia wananchi kutumia haki zao za kikatiba katika kutoa maoni juu ya mustakabali wa rasilimali zao.
"Waziri (Masauni) alichokifanya ni kutumia hoja ya nguvu badala ya kutumia nguvu ya hoja kujibu yale ambayo watu wanaokamatwa wanayafanya," alisema.
Kwa upande wake, Shillatu alisema mjadala mkali unaoendelea nchini kuhusiana na DP World na bandari za Tanzania, ni mjadala ambao kama Taifa hatujaushuhudia kwa muda mrefu baada ya kashfa ya Richmond.
“Bahati mbaya mjadala huu unaanzia kwenye makosa ya kawaida. Tuliposhindwa au tulipotoa taarifa ya muda mfupi ya kukusanya maoni ya wananchi kwa jambo linalohusu rasilimali za nchi, ndipo mgogoro ulipoanzia,” alisema.
“Lugha kali zinazotumika kwa sasa kuelezea hisia za Watanzania, wakiwemo mawakili, ni jambo ambalo wakati fulani ni vigumu kulidhibiti kwa kuwa kila mmoja ana emotions (hisia) zake na hivyo ni ngumu kudhibiti kile anachotaka kukisema katika wakati fulani,” alisema Shillatu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Taarifa, John Kitoka alisema mchakato unaofanywa na Jeshi la Polisi ni kutaka kuwatisha watu wasiendelee kutoa maoni yao.
"Ukishughulika na wanaojua kujenga hoja na ni maarufu, manake hata watu wa kawaida watakaa kimya hawawezi kuzungumza kwa kuhofia kukamatwa," alisema.
Kitoka alieleza athari za kufanya hivyo kuwa kuna uwezekano wa kuibuka wajenga hoja wengine ambao hawatakuwa na hofu tena na watashindwa kutumia majukwaa ya kawaida kama vyombo vya habari kutoa maoni yao.
“Watu wataanza kukengeuka na kutumia njia ambayo si nzuri na Serikali italazimika kutumia gharama kubwa kudhibiti hali hiyo kuliko ambavyo ingetumia kwa kuruhusu maoni huru," alisema.
Akijadili suala hilo, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Tobias Swai alikuwa na mitazamo miwili, kwanza akidai inawezekana Jeshi la Polisi linahitaji kujua kiundani maoni yao au kufahamu mambo wanayoyatilia shaka wakiwa ana kwa ana.
"Nafikiri tulichukulie kwa nia njema kwa kuwa ni chombo cha usalama ambacho kinahusika na ulinzi wa raia na mali zao," alisema.
Hata hivyo, alidai kama itakuwa ni njia ya kutengeneza vitisho kwa watu wanaojenga hoja badala ya kujibiwa, tafsiri yake ni kwamba wameanza kufunga milango ya demokrasia ya watu kutoa maoni juu ya rasilimali zao.
"Lakini ninachotaka kukiondoa katika uelewa wangu, kama itakuwa njia ya kuanza kuleta vitisho kwa watu wanaojenga hoja katika mfumo wa kidemokrasia, maana yake wanafunga milango ya watu wasitoe tena maoni," alisema.
Hata hivyo, Ali Makame, mchambuzi wa Siasa za Zanzibar aliipongeza hatua ya Serikali kuwahoji watu hao ikiwa wakizungumza mambo ambayo yanakwenda kinyume na sheria za nchi.
"Kuzungumza nako kuna mipaka, kama wameitwa wanapaswa kwenda kusikiliza wito na kuonyesha ushirikiano kwa kile watakachohojiwa," alisema.
Kukosoa si kubaya
Katika hatua nyingine, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema kukosoa si kubaya lakini maneno yanayotumika si sahihi.
Alisema alikuwa akisikiliza mjadala wa Lissu akikosoa mawazo ya Rais ya kuwajumlisha watu wanaokosoa kwenye mchakato wa kuboresha mambo kwa kusema mawazo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni matope (presidential rubbish).
Nape alisema Rais Samia ni mstaarabu, ametoa jukwaa la watu kuongea huku akisema kwa miaka miwili au mitatu iliyopita hali isingekuwa hivyo.
“Katoa fursa ya kuongea, lakini mjomba wangu kaenda kuchanganya mambo anasema Rais anataka watu waende kutoa mawazo kwenye bandari, Rais anasema waje kwenye tume ya Mipango, ukiacha kuwa Rais huyu ni mama wa Kitanzania,” alisema.
Alisema kitendo cha mtu mzima kutukana hadharani inajenga jamii ambayo leo ametukanwa Rais na siku zinazofuata itakuwa ni wazazi wengine.
“Tunataka hao watoto waamini kuwa mzazi wako unaweza kumuambia akili (kauli) yako ya matope, ndipo jamii tunataka kuipeleka,” alihoji.
Alisema Rais huyu wa sasa ndiye kiongozi pekee wa ngazi ya juu aliyefunga safari kwenda kumuona Lissu na kumpa pole alipokuwa amepigwa risasi, lakini hata akiwa Rais alienda Ubelgiji kumuona, kumpa pole na kumuomba arudi nyumbani na aliondoa zuio la kufanya mikutano.