Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika yatakiwa kuja na bunifu za kiteknolojia kuendana na mazingira

Mtaalamu wa teknolojia ya Akili Mnemba (AI) kutoka Sweeden, Alexander Morad katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Komputa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM) na kukutanisha wadau mbalimbali wa teknolojia.

Muktasari:

  • Wabunifu wa masuala ya teknolojia nchini, wamehimizwa kutumia utaalamu walio nao kubuni mfumo wa Akili Mnemba (AI) utakaokuwa katika lugha, mazingira, maadili na data za Kiafrika.

Dar es Salaam. Wabunifu wa masuala ya teknolojia nchini wamehimizwa kutumia utaalamu walio nao kubuni mfumo wa Akili Mnemba (AI) utakaokuwa katika lugha, mazingira, maadili na data za Kiafrika.

Wito huo umetolewa leo Aprili 22, 2025 jijini Dar es Salaam na mtaalamu wa teknolojia ya Akili Mnemba (AI) kutoka Sweden, Alexander Morad katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM) na kukutanisha wadau mbalimbali wa teknolojia.

Morad ambaye pia ni mwanzilishi wa taasisi ya masuala ya teknolojia ya Bright Mind Agencies, amesema mfumo huo ukibuniwa utakuwa wa kwanza utakaokuwa na data za Kiafrika kwa kiasi kikubwa.

Ametolea mfano wa zana ya kidigitali ya Akili Mnemba ya Chat GPT, ambayo ni asilimia moja tu ya data zake imetokana na data za Kiafrika.

"Marekani wana ChatGPT, China wameunda DeepSeek, Ufaransa wameunda yao, watu wengi wanatengeneza mifumo yao ya lugha na aina mbalimbali za injini za AI, lakini bado hatujatengeneza hata mfumo wa kwanza wa Kiafrika," amesema.

Pia ametumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania wanaochukulia teknolojia kama tishio la ajira zao, bali wanatakiwa kuongeza ubunifu ili kuendana na kasi mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Amesema kuwa ukiweka ubunifu katika matumizi ya AI unaweza kutengeneza fedha kutokana na fursa lukuki zilizopo ndani yake.

Miongoni mwa fursa alizobainisha ni pamoja na kutoa mafunzo ya matumizi ya AI, kutoa huduma ya maudhui kwa kutumia AI, kufanya chambuzi za takwimu na hata uhariri wa maudhui kutoka ndani na nje ya nchi

"Unaweza kupata wateja kutoka Ujerumani, Marekani, Uswidi, na nchi nyingine ukawasaidia kutatua changamoto zao na kuwapatia huduma mbalimbali kwa kutumia AI kwa bei ambayo kwao ni nafuu sana, lakini kwako ni hela nyingi,” amesema na kuongeza;

"Kwa mfano, kama mtu angeniambia, naweza kuhariri podcast yako, unipe tu dola 150,” ningekubali. Siwezi kumpata mtu Sweden anayefanya hivyo kwa kiasi hicho. Ukipata wateja 10, tayari unapata dola 1,500 kwa mwezi, wakati kama nimeelewa vizuri, mshahara wa wastani hapa ni kama dola 230 hadi 300.

Kwa upande wake, Felician Nyanda, Mkurugenzi kutoka kampuni ya BFI anasema namna matumizi ya teknolojia ya AI yanavyorahisisha kazi, yanamfanya mtumiaji kuweza kuhudumia watu wengi zaidi na kuongeza kipato.

Nyanda ametolea mfano wa namna àkili mnemba, inavyoweza kutengeneza tovuti ndani ya muda mchache.

"Kutokana na inavyorahisisha kazi mtumiaji anaweza kuongeza kipato kupitia kazi anayoifanya kwa msaada wa AI," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Komputa cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM), Leticia Ndongole amesema wao kama taasisi inayojishughulisha na masuala ya teknolojia wamekuwa wakihakikisha Watanzania hawawi nyuma katika masuala ya teknolojia.

"Hatutaki mtu aachwe nyuma na hiyo ndiyo sababu tumekuwa tukiendelea kutoa elimu na semina kwa watu, katika kada mbalimbali kutumia teknolojia katika kurahisisha kazi zao," amesema.

Ameongeza kuwa kuna haja sasa ya elimu kuhusu matumizi sahihi ya akili mnemba (AI) kuingizwa katika mtaala ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa mstari wa mbele katika masuala ya teknolojia.

Pia kwa wale wenye hofu kuwa matumizi ya AI yatakwenda kuondoa ajira zao, Ndongole amewataka kuachana na dhana hiyo kwani mfumo huo umekuja kwa ajili ya kurahisisisha ufanyaji wa kazi na siyo kuharibu ajira ya mtu.

"Msiichukulie teknolojia kama inakuja kuua ajira zenu, mnapaswa kutafakari kwa kina kuja na ubunifu ambao utaitumia hiyo teknolojia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi," amesema.