Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo sita yanayoipa thamani kazi ya ufundi

Muktasari:

  • Ufundi anaouzungumziwa ni shughuli kama ujenzi, useremala, ushonaji wa nguo, na kazi nyingine zote zinazofanywa kwa mikono na kuwaingizia wananchi kipato.

Dar es Salaam. Mkurugenzi na mwanzilishi wa Fundi Smart, Fredy Herbert amesema ili kuiongezea thamani shughuli ya ufundi ni kuhakikisha wanaojihusisha na kazi hiyo wanapewa uelewa wa mambo sita muhimu.

Ametaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni elimu ya afya, utunzaji wa fedha na maandalizi ya dharura ili mafundi waweze kuona tija ya kazi wanazofanya.

Ufundi anaouzungumzia Herbert unahusisha shughuli kama ujenzi, useremala, ushonaji wa nguo, na kazi nyingine zote zinazofanywa kwa mikono na kuwaingizia wananchi kipato.

Katika kutekeleza azma hiyo, amesema yeye na wenzake wameanzisha programu ya Fundi Smart ambayo wanaamini itabeba ndoto hiyo na kufanikisha malengo yote.

Herbert aliyazungumza hayo hivi karibuni alipofanya mahojiano na Mwananchi Digital jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa kutokana na kada ya ufundi kutothaminiwa ipasavyo, wameona kuanzishwa kwa programu hiyo kutaiinua na kuipa hadhi stahiki.

“Tunapozungumzia maisha, ni ufundi. Lakini je, jamii inawachukuliaje mafundi? Mtu akisema yeye ni fundi, anachukuliwa kawaida. Hiyo ndiyo sababu tumekuja na Fundi Smart,” amesema.

Amesema programu hiyo inahusisha vipengele sita ambavyo ni msingi wa mafanikio ya fundi na vinamwezesha kulinda afya yake na kunufaika zaidi na kazi.

Miongoni mwa vipengele hivyo, ni elimu ya afya kwa mafundi wote hasa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya kinga wakati wa kazi zao.

Amesema wamekuwa wakitoa elimu hiyo baada ya kubaini kuwa mafundi wengi hukwama mara tu wanapopatwa na maradhi.

“Fundi akiacha kufanya kazi, kipato kinakata. Maisha yake ya kila siku yanategemea sana kazi. Kwa hiyo tunawapa elimu ya afya ili kuepuka hali hiyo,” amesema.

Jambo lingine amesema ni elimu ya fedha, kuwasaidia mafundi kupanga matumizi yao sambamba na kiwango wanachowatoza wateja wao.

Katika mazingira ya sasa, amesema mafundi wengi hasa wa ujenzi hufanya kazi kwa miaka mingi lakini hawana makazi yao binafsi.

“Kuna mambo mengi katika sekta ya fedha. Wengine hawaweki akiba, au wanatumia fedha vibaya kwa imani kwamba kila siku watapata,” amesema.

Aidha, amesema Fundi Smart inatoa pia elimu ya sheria za kazi ili mafundi waweze kufanya shughuli zao bila kuvunja taratibu za kisheria.

“Unakuta fundi anakubaliana na mteja, anapokea malipo ya awali lakini haendelei na kazi. Mambo haya yanatokea kwa sababu hawajui sheria,” amesema.

Kutokana na mapungufu hayo, amesema mafundi wengi wamejikuta wakipelekwa mahabusu au hata kufungwa jela.

Vilevile, amesema mafundi wanaelimishwa kuhusu maandalizi ya dharura na namna ya kukabiliana na matukio ya ghafla.

Kuhusu huduma kwa wateja, amesema ni kipengele kingine muhimu wanachofundisha ili mafundi waweze kutoa huduma kwa lugha na mwenendo unaofaa.

“Tunawafundisha kutumia lugha nzuri kwa wateja wao. Kama wao wanavyopiga simu na kuhudumiwa vizuri, basi nao wanatakiwa kutoa huduma kwa namna hiyohiyo,” amesema.

Jambo la sita, amesema ni matumizi ya teknolojia, ili kurahisisha kazi zao na kuongeza ufanisi.

Ameeleza kuwa lengo kuu la Fundi Smart ni kuwabadilisha mafundi kutoka kuwa wa kawaida hadi kuwa smart yaani wenye maarifa, nidhamu na mwonekano wa kitaalamu.

Amesema mafundi watajiunga bure, na wamekuwa wakifanya makongamano mbalimbali nchini kutoa elimu hiyo.

Aprili 29, mwaka huu, wanatarajia kufanya kongamano la mafundi mkoani Mbeya, ambapo mafundi wa ujenzi, ushonaji, useremala na wengine watakutanishwa.

Kongamano hilo litafanyika Ukumbi wa Tugimbe, eneo la Mafyati, na ushiriki hautakuwa na gharama yoyote.

Herbert amesema wanatarajia washiriki kati ya 1,500 hadi 2,000 katika kongamano hilo na baada ya Mbeya, makongamano yataendelea katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa ratiba ya mikoa mingine itaandaliwa ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata mafunzo kupitia programu hiyo.

Amesema shughuli hizi wanafanya kwa kushirikiana na Taasisi ya Ufundi Stadi (Veta), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha).

Pamoja na taasisi hizo za umma, pia wameshirikiana na taasisi binafsi zinazosaidia kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Fundi Smart.