Afande Sele alivyokwama kufanya mtihani, atua mtaani kusaka maisha -2

Afande Sele akiwa na watoto wake Tunda (kulia) na Asantesanaa. Picha na mtandao
Morogoro. Anasema akaendelea na maisha ya mtaani yasiyo na uangalizi baada ya shule. “Baadaye nilikwenda Moshi, nikafanya shughuli kwa mjomba, kisha nikafanya kazi za ulinzi, ujenzi na kuanza kujitegemea na baada ya miaka kadhaa nilipata nafasi ya kujiunga na jeshi, kisha muziki na kuwa kwenye mahusiano yaliyonipa familia yenye upendo, ingawa nilipambana hasa. “Maisha yale ndio yamenisukuma kuwaongoza wanangu, sio tu wa kuwazaa hadi wengine wanaonisikiliza, huwa napenda kuongeza upungufu na ubora wangu katika kuwafunza wengine, ukiangalia makuzi yangu na niliyowapa wanangu ni tofauti, wao wamepata malezi na ukaribu wangu na ndugu wengine ambao mimi sikuyapata.
“Hiyo imenipa uzoefu na ujasiri mkubwa wa kuwaelimisha, binti zangu nawategulia mitego ambayo kama mimi baba yao nisingeishi hivyo huenda wasingelijua,” anasema.
Anasema, alijikuta ameingia kwenye kuimba akiwa mtaani, Morogoro japo hakuwa maarufu hadi alipokutana na Joseph Mbilinyi (Sugu). “Sugu aliniona naimba, akapenda kipaji changu, nikawa naye hadi nilipoweza kusimama. “Iliniumiza, mzazi mmoja yupo lakini hujawahi kupata mapenzi yake, japo wakati mwingine nasema mitihani niliyopitia ndiyo imefanya niwe hapa nilipo, kabla ya muziki niliwahi kujiunga na jeshi ila kutokana na mambo ya ujana nilifukuzwa.
“Lile jambo pia liliniumiza, sikufahamu kesho yangu itakuwaje, kwani tayari nilishaingia kwenye mfumo na kuanza kulipwa hadi mshahara, lakini katika mazingira ya kidunia nilipoteza ile nafasi, ilikuwa ni bahati mbaya, sio kila kitu ni uzembe au makusudi, hasa sisi ambao tunapitia makuzi ya bila mwongozo wa wazazi.
“Nilikengeuka tu na sikujua hatima yangu baada ya tukio hilo, muziki ulitokea tu, ni karama ilikuja, lakini jeshi ni taaluma ambayo nilikwenda depo kule Zanzibar kujifunza, liliniumiza nilipofukuzwa, najilaumu mwenyewe kwa tukio lile, ilikuwa ni ujana tu na kukengeuka, nilijutia sana japo baadaye nikaja kuwa mwanamuziki.”
Anasema changamoto kubwa kwenye muziki wakati huo jamii haikuwa na uelewa na Bongofleva, wengi walilioshiriki walionekana kama waasi kwenye familia zao. “Kipindi kile ndio muziki tuliofanya ulikuwa unaingia ingia nchini, tena ilikuwa ni ku-rap, sio huu wa kuimba, moja kwa moja ulijumuishwa na uhuni, kipindi hicho miaka ya 1990 kulikuwa na kuuana, ndipo yalifanyika mauaji ya 2PAC na sisi tukaupokea hivyo.”
Anasema ili waeleweke kwenye jamii, walilazimika kuimba nyimbo za kukemea na kutishia, ingawa baadaye wakaingiza meseji zenye mafunzo, japo walionekana kana kwamba ndiyo wameshapotea.
“Tulianza kutunga nyimbo ili watu watuelewe, hata wakitusikiliza pamoja na kwamba tunaonekana wahuni, lakini wajihoji mbona wanaongea vitu vya msingi, haikuwa rahisi eti mtu tu kanywa pombe kalewa anaenda studio, ilikuwa lazima ukae na watu upate historia au ujisomee vitabu ndipo uandike mistari. “Changamoto nyingine ikawa ni studio, zilikuwa MJ Records na Bongo Records tu, hivyo unaweza kwenda siku hiyo kumbe sio zamu yako.
Anasema masilahi kwenye muziki nayo ilikuwa kidogo, japo waliutengenezea njia lakini haukuwalipa, kwani pesa wao walipata kwenye matamasha. “Tulikuwa tunaanda tamasha tunakaa wenyewe mlangoni kukusanya kiingilio, pesa inayopatikana tunagawana, muziki haukuwa na maslahi makubwa. Ingawa hatukukubali jamii ituone kuwa sisi tuliofanya muziki wakati huo ni kama waasi, tulilazimisha kuandika muziki wenye ujumbe mzito ili jamii ituamini na kutuona hatufanyi uhuni,” anasema na kuongeza; “Wanamuziki wa zamani hatukupata pesa, lakini tulijenga heshima kwenye muziki, nyimbo zetu zilijikita kufikisha ujumbe na kufanya muziki ukubalike, tulitengeneza njia hadi leo ‘watoto’ wanaimba hata matusi wanapata pesa, tunaona mzazi anatoa pesa kumlipia mwanaye ili akarekodi, wakati wetu hayo hayakuwepo,” anasema.
Maisha yake ya sasa
Mwaka 2004, ndipo mwimbaji huyo ambaye sasa ni balozi wa mazingira na mkewe Asha walinunua eneo huko Modeko, Kata ya Mazimbu, mjini Morogoro ambalo walikubaliana kuwa hapo ndipo yatakuwa makazi yao ya kudumu na familia yao.
Katika eneo hilo, Afande Sele ametengeneza kempu tofauti alizozipa majina, kuna Magufuli Site ambayo imewekewa eneo la kupumzika, ina urembo wa chupa mbili za asili, moja ina rangi ya bendera ya taifa na nyingine ina rangi nyekundu, njano na kijani (alama inayotumiwa na marasta). Kwenye eneo hilo pia kuna picha ya Simba, ambayo anasema Simba ni mnyama shujaa, naye alimuona Magufuli kama mnyama Simba. Eneo jingine ni Samia Site, ambalo amempa heshima Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anamtaja kama mwanamke jasiri ambaye aliwatoa Watanzania kwenye simanzi baada ya kifo cha Magufuli. “Binafsi nilikuwa nawaza itakuwaje baada ya kifo cha Magufuli, lakini tumeona namna Rais Samia alivyoiongoza nchi, kwenye eneo hili ni mahususi kwa ajili ya kufanya usuluhishi wa jambo fulani kama kaka na kioo cha jamii wanaomzunguka wakiwa na ugomvi humfuata na hutumia hilo eneo kuwasuluhisha,” anasema. Pia kuna eneo la Nyerere Site, Karume, Sokoine, Dk Remmy na Asantesanaa Site, yote yakiwa na maana, Nyerere ambaye ni baba wa Taifa, Karume Rais wa kwanza wa Zanzibar na Sokoine, Waziri Mkuu wa zamani ambao wote wametangulia mbele za haki na mwanangu ambaye jina lake lilitokana na shukrani zangu kwenye sanaa,” anasema.
Itaendelea kesho