Afande Sele aeleza anavyoishi na wanawe baada ya mkewe kufariki-3

Muktasari:
- Katika toleo la jana tuliona jinsi Afande Sele alivyowekeza maisha yake eneo la Modeko mjini Morogoro, akiunda kambi za kumpumzikia, moja inayoitwa Magufuli site na nyingine Samia site. Leo pamoja na mengine anaelezea watoto wake Tunda na Asantesanaa walipo. Endelea
Tunda ambaye wakati mama yake anafariki Agosti 2014, Afande Sele anasema alikuwa kidato cha pili Shule ya Wasichana Kunduchi, sasa ni mwalimu anayejitolea kwenye moja ya chuo mjini Morogoro baada ya kuhitimu shahada yake ya kwanza chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA).
“Ni kudra za Mungu, mapenzi yake mwenyewe kwenye malezi ya binti zangu, mama Tunda alifariki Asantesanaa akiwa na mwaka mmoja na miezi kama tisa hivi, nilisema nitawalea mwenyewe, niliwafanya kuwa rafiki zangu.
“Niliwaongoza kuwa na hofu ya Mungu bila kuwalazimisha kuwa kwenye imani fulani, imenisaidia na nilipowafanya kuwa marafiki zangu na kuwa wazi kwangu katika majaribu yote wanayoyaona na kukutana nayo kuwa wananishirikisha, ilinisaidia katika malezi yao nikipewa sapoti kubwa na bibi yao upande wa mama yao na mama zao wadogo,” anasema.
Anasema katika malezi yote ya binti zake hadi sasa, hakutaka wafuate nyayo zake za muziki, japo Tunda anajua kuimba ila kama watapenda kuingia huko ni baada ya kuwa na maisha yao na kujitegemea.
Nyumbani kwa Afande Sele, Tunda ndiye mwenye nyumba japo muda mwingi anakuwa kazini na mdogo wake anakuwa shuleni.
“Tunda akija ananiambia Sele mbona hapa hujasafisha hata mama yao walikuwa wakimuita Asha tulizoeana hivyo, hawaniiti baba wananiita jina langu.
“Tundajema amehitimu SUA shahada yake ya kwanza alikuwa anasoma mambo ya sayansi, sasa anafundisha (alitaja moja ya vyuo maarufu mjini Morogoro) tangu Septemba mwaka jana, lakini ana malengo mengine, Asantesanaa yupo darasa la sita Shule ya Msingi Nguzo.
Akimzungumzia baba yake, Tundajema anasema, “alitulea kama marafiki mbali na ile ya kuwa baba na binti zake, yeye ndiye rafiki yetu wa kwanza.
“Baada ya mama kufariki, nakumbuka shida zangu zote nilimueleza yeye, hata nilipokuwa mbali na nyumbani shuleni, na tatizo mtu wa kwanza kumwambia alikuwa yeye, nampigia simu, hayo ndiyo maisha yetu hadi sasa,” anasema.
Anasema japo kuna wakati baba yao huwabadilikia na kuwakanya pale walipokosea na hata wakati mwingine kuwaadhibu, lakini asilimia kubwa alikuwa karibu nao wakijadiliana mambo mbalimbali kama marafiki.
“Mdogo wangu huanzia kwanza kwangu kunieleza changamoto zake na mimi huangalia kama nimshirikishe baba au nitafute mtu mwingine wa karibu wa kumueleza, tuliishi hivyo hadi sasa najitambua na nimekuwa kama mama wa familia yetu.
“Ule upweke wa mama unakuwepo, kwani mimi nimeishi naye muda mrefu kuliko mdogo wangu, lakini niliamini baba yupo na alitujengea misingi ya ukaribu na urafiki na kumcha Mungu ambao unatuongoza hadi sasa,” anasema Tundajema.
Hakutaka kuoa
Afande tangu kuondokewa na mkewe mpenzi Asha (Mama Tunda), anasema hakutaka kuwatafutia wanaye mama mwingine kwa kuhofu mambo mengi.
“Ni kweli hakuna maisha ya peke yako, lakini ningesema nitafute rafiki niishi naye, kina Tunda wakae na mama mwingine japo nilitamani iwe hivyo, changamoto ni mazingira ya sasa, nilikuwa na hofu ukiingia kwenye mahusiano maana umependa huwezi gawanya upendo wa watoto na mke mwingine.
“Nikasema nitakomaa nao mwenyewe, nitaishi hivi hivi, niliwashawishi wanangu wajue mimi na mama yao tulikuwa na malengo mazuri tu, lakini Mungu amempenda zaidi mama yao,” anasema.
Anasema wanae wana zamu ya kumpigia simu kila siku, asubuhi Tunda atamuuliza ameamkaje, jioni Asantesanaa ambaye Jumatatu hadi Ijumaa anakuwa kwa bibi yake mzaa mama kwa ajili ya shule anampigia kumtakia usiku mwema na wikiendi wanakuwa pamoja.
“Wakiwa nyumbani, kama baba ni jukumu langu kuwapikia, wao watanisadia kufua na kuosha vyombo na usafi wa nyumba, lakini wanangu chakula chao nawapikia mwenyewe na nilijifunza kupika nilipokuwa najilea mwenyewe wakati huo,” anasema.
Licha ya kuwa staa, Afande Sele anasema yeye si mtu wa starehe na kwenda klabu, maisha yake ni nyumbani, akitoka anakwenda kwenye majukumu ya msingi.
“Siwezi kutoka usiku eti nikanywe pombe na marafiki, huo muda sina, siko hivyo kabisa, hata marafiki zangu wanalifahamu hilo, aliye na shida na mimi huja nyumbani,” anasema.
Kuhusu muziki kwa sasa
Licha ya kutofanya kwa kiwango kikubwa, Afande Sele anasema, “bado naimba japo si kwa kiwango kikubwa, kwani muda mwingi sasa najishughulisha na kilimo na kazi zangu za mazingira, nilipewa hilo jukumu na Rais pale Kigamboni, hivyo ni majukumu juu ya majukumu.”
Anasema japo muziki si umri bali ni maarifa ambayo mtu anazaliwa nayo na hakuna kustaafu, bado anafanya mara moja moja ingawa muda hautoshi kutokana na majukumu kuongezeka.
“Japo ule muziki wetu wa kutulia na kuandika mashairi si huu wa sasa, lakini tunaamini watu bado wanauhitaji huo na mimi naufanya bado ingawa si sana. Mwaka 2021 nilitoa wimbo unaitwa ‘Hauna hatia’, mwaka jana (2022) nikafanya mwingine unaitwa ‘Bila Marekani’, Basata walinipigia simu wakasema niutoe, niliongea na mwanasheria kausikiliza akasema hauna tatizo, sikuutoa,” anasema.
“Baada ya wiki mbili, Ubalozi wa Marekani waliposti kwenye mtandao wao wa kijamii wakasema wameusikia hata kama unawagusa, lakini hauna tatizo lolote, ni wimbo ambao ulipata mafanikio, kusikilizwa na ubalozi wa nchi kubwa kama Marekani tena ukiwa kwa lugha ya Kiswahili na ni audio kwangu ilikuwa ni mafanikio, tunaendelea kufanya muziki kwa kutuheshimisha,” anasema.
Amsamehe mama, aongoza mazishi yake
Pamoja na changamoto alizopitia zilizosababishwa na kuachwa na mama yake, Afande Sele anasema alimsamehe baadaye alipofahamu ukweli uliomfanya mzazi huyo kumuacha.
“Japo niliteseka, nilipambana na dunia, lakini nilipofahamu ukweli wa kilichomuondoa mama yangu na kuniacha bila kujua naishije hata baada ya baba kufariki, nilimsamehe.
“Mama alipitia changamoto ya kubaguliwa na familia ya baba, alitoka kwenye ukristo, jambo ambalo upande wa baba hawakukubaliana nalo, walimtenga pale nyumbani, walikuwa wakimnyanyapaa kwanza ni mkristo, lakini pia mchaga, hilo lilipelekea kutokuwa na sapoti yoyote akalazimika kuondoka na kwenda kuanza maisha yake mengine.
“Aliolewa kwingine na kuzaa watoto watatu, ndugu zangu hao tuliochangia mama, nilikuja kuonana nao nikiwa mkubwa, aliponieleza sababu za kuondoka kwa baba yangu iliniumiza sana, nilimuonea huruma na kuona kabisa hakuwa na hatia, mazingira yalimlazimisha.
“Hata alipofariki, kama kijana wake mkubwa niliongoza mazishi yake kule Moshi mwaka jana, nilirudisha upendo wangu kwake na kusahau yote yalitonitokea.” Anasema alipitia yote hayo kwa chuki tu za shangazi yake ambaye ni kama alitaka kumharibia maisha, na hata wimbo wake wa ‘Mkuki moyoni’ aliutunga mahususi kwa kwa ajili ya shangazi yake huyo.
“Mkuki moyoni ilikuwa ni kwa ajili yake, asilimia 90 huo wimbo umeyagusa maisha yangu halisi niliyopitia na mlengwa ni shangazi yangu.
“Yeye alijimilikisha kila kitu cha familia, alikuwa mkatili, japo sitaki kujuta kwa ajili yake, lakini naamini hakufanya vizuri, alikosea, basi hakutaka kunilea, kwanini asingeniacha Moshi baada ya kukutana na mama na wajomba zangu, kama haitoshi ni yeye huyo huyo aliniambia mama yangu alikufa kumbe si kweli,” anasema.