Adaiwa kumchinja mkewe mjamzito, amchana tumbo

Muktasari:
- Mtuhumiwa huyo pia anadaiwa kumuua mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili.
Tabora. Mkazi wa Kata ya Uyogo wilayani Urambo mkoani Tabora, Hamisi Kulwa (35) anashikiliwa na Polisi mkoani hapa akidaiwa kumuua mkewe na mtoto wake wa miaka miwili.
Taarifa za awali zinadai Hamisi alifanya tukio hilo Jumanne, Januari 30, 2024 kwa kumchinja mtoto wake na mkewe (majina hayajatambulika) aliyekuwa mjamzito, kisha kumchana tumbo na kuutoa ujauzito huo.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu leo Jumamosi, Februari, 3, 2024, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Richard Abwao, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Urambo mkoani humo.
Kamanda Ambwao amesema tukio hilo lilitokea Januari 30, 2024, saa 11 jioni na katika maelezo ya awali yanaonyesha tukio hilo linahusiana na imani za kishirikina.
"Hamisi alimuua mke wake na mtoto wake mwenye umri wa miaka miwili. Katika mahojiano ya awali alieleza alikuwa anaumwa, alikwenda kwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya matibabu.
“Amesema kuna dawa alipewa, alipotumia ikamjia hali ya ukatili akafanya hivyo.
"Baada ya kumchinja mkewe alimpasua tumboni na alimkata maziwa… alimuua kikatili, na huyo mke alikuwa na ujauzito, sasa kusema ulikuwa wa mapacha sina uhakika, lakini ni kweli alikuwa na ujauzito ambao aliutoa," amesema Abwao.
Kuhusu miili ya marehemu, Abwao amesema baada ya uchunguzi wa miili hiyo, imekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya maziko.
Akizungumzia tukio hilo, Askofu wa Kanisa la Calistmatic Episcopal Church Of Tanzania (CECT), Charles Sekelwa ametaja msongo wa mawazo katika jamii na kukosa hofu ya Mungu kuwa sababu zinazochangia matukio ya mauaji kutokea nchini.
Askofu Sekelwa amewashauri wanaopitia msongo wa mawazo kutafuta ushauri kwa watu wenye hekima, wanaowazidi umri na viongozi wa kiroho kabla hawajachukua uamuzi mgumu ikiwemo kusababisha mauaji.
"Kumekuwa na msongo mkubwa wa mawazo kwenye jamii yetu. Msongo wa mawazo unapomkamata binadamu na akashindwa kutafuta mahali ambapo anaweza kutatua tatizo lake, vitu kama hivyo (mauaji) ni kawaida kutokea.
"Mtu yeyote anayeamini na anajua Mungu yupi, imani itajengeka ndani yake, hivyo itamuwia vigumu kutoa uhai wa mtu mwingine akijua kwamba uhai wa mtu anayeutoa na wa kwake vyote viko mikononi mwa Mungu, kwa hiyo hilo ni jambo la kiimani," amesema Sekelwa.
Kwa upande wake, Mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza, Ladislaus Sorwa amewaomba viongozi wa dini kuongeza mafundisho ya kiimani katika jamii ikiwemo kuwahusia waumini kumuogopa Mungu.
"Changamoto za maisha zinawafanya watu wengi kufikiria wanaweza kumaliza matatizo yao kwa njia za mkato, matokeo yake mtu anaweza kujikuta amefanya jambo la ajabu kama hilo," amesema Sorwa.