ACT Wazalendo yatia neno Siku ya Moyo Duniani

Muktasari:
- Maadhimisho ya siku ya moyo yamefanyika nchini huku Chama cha ACT Wazalendo kikiitaka Serikali kuipa kipaumbele suala la matibabu na mfumo wa ugharamiaji wa afya ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo.
Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo, kimeitaka Serikali kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila kikwazo chochote, kupitia bima ya Afya inayotokana na Hifadhi ya Jamii.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya wa chama hicho Ruqayya Nasssir alipotembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) baada ya kuwaona watoto wanaopatiwa huduma ya moyo kwenye taasisi hiyo.
Tamko la ACT Wazalendo ni sehemu ya kudhimisha Siku ya Moyo Duniani sherehe ambayo hufanyika kila mwaka Septemba 29, mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ‘Utumie moyo, utambue moyo’.
“Tunashuhudia kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya Watanzania wanaokabiliwa na matatizo ya moyo na kwa upande mwingine tunaona ukubwa wa gharama za kiafya hasa suala la matibabu nchini,” amesema.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa leo Septemba 29, 2023 na chama hicho kimesisitiza Serikali kuimarisha huduma za afya ya msingi kwa watu wenye magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Hatua hiyo ni kupitia kuweka kipaumbele kwenye matatizo ya upungufu wa miundombinu, ukosefu wa dawa, wafanyakazi wa afya katika ngazi ya afya ya msingi yaani zahanati na vituo vya afya, wenye mafunzo ya kuzuia, kutambua na kuwasaidia watu wenye magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza.
“Serikali iweke mkazo kutoa elimu ya afya kwenye ngazi ya jamii, kupitia zahanati na vituo vya afya,”amesema.
Sababu na dalili za tatizo la moyo
Matumizi ya tumbaku, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, chumvi nyingi, lehemu nyingi na kutokula mbogamboga na matunda ya kutosha.
Pia, unywaji wa pombe, uzito uliozidi au unene uliokithiri, kutokufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara na kuwa na shinikizo kubwa la damu ni visababishi vya tatizo la moyo.
Kwa upande wa dalili, kwa mtu mwenye tatizo la moyo hupata maumivu ya kifua ambayo hutokea zaidi mtu anapojitahidi kujishughulisha na kutoweka anapopumzika, moyo kwenda haraka, uchovu na kukosa nguvu ya kufanya kazi na moyo hushindwa kabisa kufanya kazi.
Kukabili maradhi ya moyo inashauriwa ufanyaji mazoezi walau kwa dakika 150 kwa wiki, kupunguza matumizi ya chumvi sukari na mafuta.