Absa Tanzania kupeleka Sh120 milioni kampeni ya huduma kidigitali
Mkurugenzi wa Huduma za Wateja Binafsi wa Benki ya Absa Tanzania, Ndabu Swere (Katikati), akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuhusu uzinduzi wa kampeni ya Ujanja ni Kuswipe na Kadi ya Absa, yenye lengo la kuhamasisisha wateja kutumia huduma za kidigitali katika kufanya miamala ya kifedha. Wengine ni wafanyakazi wa benki hiyo na Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Judith Wililo (kulia).
Muktasari:
- Kampeni hiyo imezinduliwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni, imepewa jina la “Ujanja ni Kuswipe na Kadi ya Absa.”
Dar es Salaam. Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wengi zaidi, Benki ya Absa Tanzania imezindua kampeni maalumu inayohamasisha matumizi ya huduma za kidigitali na kadi za benki, huku ikitenga jumla ya Sh120 milioni kwa ajili ya zawadi kwa wateja.
Kampeni hiyo, iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam hivi karibuni, imepewa jina la “Ujanja ni Kuswipe na Kadi ya Absa.”
Lengo lake kuu ni kuhimiza watanzania kutumia zaidi njia za malipo salama, rahisi na za kisasa badala ya kubeba fedha taslimu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Huduma za Wateja Binafsi wa Absa Tanzania, Ndabu Swere, alisema huduma za kidigitali za benki hiyo zimebuniwa kwa ajili ya kuongeza usalama na urahisi kwa wateja.
“Ukitembea na fedha taslimu unajiweka kwenye hatari ya kuangukia mikononi mwa wezi na wajanja wengine. Kupitia kampeni hii tunawahamasisha wateja kutumia zaidi kadi za Debit na Credit za Absa pamoja na huduma za benki mtandaoni, simu na mawakala,” amese,a Ndabu.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo ni kielelezo cha dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kuwazawadia wateja wake na kusherehekea uaminifu wao.
Kwa upande wake, Aron Luhanga Mkuu wa Masoko na Uhusiano wa Umma wa Absa Tanzania, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa dhumuni kuu la benki hiyo la “Kuiwezesha Afrika ya kesho, hatua moja baada ya nyingine.”
“Kila muamala wa mteja ni stori ya ukuaji na urahisi. Kupitia kampeni hii tunasherehekea stori hizo kwa kuwazawadia wateja wanaoichagua Absa kama mshirika wao wa kifedha,” amesema Luhanga.
Aidha, Meneja wa Bidhaa za Kadi na Malipo wa benki hiyo, Erica Mwaipopo amesema zawadi mbalimbali zimetengwa kwa washindi watakaoshiriki kampeni hiyo.
“Kila wiki kutakuwa na washindi sita ambao kila mmoja atajinyakulia Sh500,000. Zaidi ya hapo, kila mwezi kutakuwa na washindi watatu watakaopata zawadi za Sh3 milioni, Sh5 milioni na Sh10 milioni. Mwisho wa kampeni mshindi mmoja ataondoka na zawadi kuu ya Sh30 milioni,” amesema.