Abdulla akemea wapotoshaji Muungano

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na wanalushoto mkoaninTanga. Picha na Raisa Said
Muktasari:
- Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema wanaojaribu kupotosha kuhusu Muungano, hawazungumzii kero zake isipokuwa kero binafsi za matumbo yao.
Lushoto. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amewakemea wapotoshaji kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwamba hawana nia njema kwani hawazungumzii kero za muungano bali ubinafsi wao.
Hayo ameyasema leo Oktoba 12, 2023 wakati wa mkutano wa ndani aliokuwa akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya tawi na mashine; wilayani Lushoto, mkoani Tanga.
Makamu huyo wa pili wa Rais amesema kuwa muunguno huo unafaida na mambo makubwa lakini wapo watu wanajaribu kupotosha na kuharibu dhana ya wasisi "Mzee wetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume."
"Niwaombe Watanzania tuendelee kuimarisha Muungano wetu, na kwa bahati njema sana kwa upande wa Zanzibari, ile mikutano ya muungano mie hushiriki na mwenyekiti wetu anakuwa ni Makamu wa Rais, na tukimaliza kamati zote za pande zote mbili tunapeleka taarifa kwa viongozi wetu, niwaambie tunakwenda vizuri sana," amesema.
Abdulla amesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha uongozi wa awamu ya sita Tanzania na awamu ya nane kule Zanzibar, zimetatuliwa kero nyingi za muungano nakusema zilizobaki ni nne na kwamba mwezi huu wanakutana tena.
Awali, Mwenyekiti wa chama hicho wilayani Lushoto, Ally Daffa alisema kuwa kutokana na jiografia ya Wilaya ya Lushoto ameomba waweze kupatiwa wilaya ya kichama katika halamshauri ya Bumbili iliyopo wilayani humo.
Ombi hilo, pia limeungwa mkono na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (Nec), kutoka Mkoa wa Tanga, Mohamed Ratco, ambapo amesema endapo watapata wilaya hiyo ya kichama, itasaidia kuondoa changamoto za hapa na pale.
Makamu huyo wa pili wa Rais wa Zanzibari yuko mkoani Tanga kwa ziara ya siku ya kuimarisha chama hicho ngazi ya tawi na shina, ambapo yeye ni mlezi wake kwa mkoa wa Tanga.