261 wafariki, wengine 650 kujeruhiwa treni tatu zikigongana

Wananchi wakiwa katika eneo ilipotokea ajali ya treni huko jimbo la Odisha,India. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Watu 50 wamefariki huku zaidi ya 350 wakijeruhiwa kufuatia ajali iliyohusisha treni tatu nchini India huku vifo zaidi vikihofiwa.
India. Zaidi ya watu 261 wamefariki dunia na wengine 650 kujeruhiwa baada ya treni mbili za abiria na moja ya mizigo kugongana katika Jimbo la Odisha mashariki mwa India usiku wa kuamkia leo.
Takribani magari 50 ya wagonjwa yamepelekwa katika eneo la tukio Wilaya ya Balasore, Katibu Mkuu wa jimbo hilo, Pradeep Jena amethibitisha.
Jena amewaambia wanahabari kwamba timu za NDRF na SDRF ziko eneo la ajali na waokoaji kati ya 600 hadi 700 wametumwa kwa ajili ya shughuli ya uokoaji.
Ofisi ya Kamishna wa Misaada Maalum (SRC) ilituma timu zao kwenye eneo la ajali kwa shughuli ya utafutaji na uokoaji. Mtendaji Mkuu wa Odisha Naveen Patnaik amemuagiza waziri wa Usimamizi wa Maafa wa jimbo hilo Pramila Mallik na maafisa wakuu wa SRC pamoja na huduma za zimamoto kusimamia operesheni hiyo.
Moja ya treni zilizohusika katika ajali hiyo ni Shalimar-Chennai Coromandel Express, maafisa wamesema.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi amesema amesikitishwa na tukio hilo huku akitoa salamu za pole kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.
"Operesheni za uokoaji zinaendelea katika eneo la ajali na usaidizi wote unaowezekana unatolewa kwa wale walioathiriwa," Modi ameandika katika mtandao wa Twitter.