Walioambukizwa kipindupindu Mwanza wafikia 58

Muktasari:
- Uwepo wa kipindupindu mkoani Mwanza ulitangazwa rasmi Januari 9, mwaka huu, zikiwa zimepita siku tano tangu watu watano waripotiwe kuugua ugonjwa huo uliolipuka katika eneo la mji mdogo wa Kagonga mkoani Shinyanga, huku watu 13 wakilazwa na 452 waliochangamana nao wakifuatiliwa.
Mwanza. Idadi ya walioambukizwa ugonjwa wa kipindupindu mkoani Mwanza imeongezeka kutoka watu 34 na kufikia 58.
Januari 10, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk Thomas Rutachunzibwa wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao cha wajumbe wa kamati ya huduma ya afya ya msingi mkoani humo, walisema watu 34 walikuwa wamethibitika kuwa na maambukizo ya ugonjwa huo.
Takwimu za ongezeko la wagonjwa hao mkoani Mwanza zilitolewa jana Jumapili Januari 14, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani humo, Hassan Masala alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya maji taka.
Masala alisema takwimu zinaonyesha wilaya zilizoathiriwa na maambukizo ni Magu, Ilemela na Nyamagana huku akisema baadhi ya waliokutwa na maambukizo tayari wametibiwa na kuruhusiwa kujumuika na familia zao.
“Takwimu za wataalam wetu zinaonyesha mpaka kufikia leo (jana) tulikuwa tumepokea wagonjwa kama 58, wapo ambao wamepata tiba wameruhusiwa na ambao wanaendelea kupokelewa, maeneo ambayo yamepata athari kubwa ni Magu, Ilemela na Nyamagana,” alisema Masala.
Alisema juzi Januari 13, mwaka huu ofisi yake ilipokea malalamiko ya kuwepo utiririshwaji holela wa maji taka katika mitaro ya eneo la Kirumba, jambo linalotajwa huenda likachangia mlipuko huo kuwapata baadhi ya wakazi wa maeneo hayo.
“Tulikuwa na kazi kukagua miundombinu ya masoko ambako wananchi wanapata huduma, ni ratiba ya kawaida, lakini sasa hivi tumebidi tuongeze nguvu kwa sababu ya changamoto ya kipindupindu ambayo mkoa tunakabiliana nayo, lengo ni kusisitiza suala usafi na tahadhari za kuchukua kwa wananchi na wateja wanaopata huduma kwenye hayo maeneo,” alisema.
Masala aliitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) kufanya ufuatiliaji wa chemba zilizounganishwa kiholela na mifumo ya maji taka sambamba na kufanya uchunguzi wa hali ya uchafunzi na vimelea kwenye maji yanayopita maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
“Niwaombe Mwauwasa, mfanye ufuatiliaji wa maeneo ambayo yanavujisha maji taka maeneo mbalimbali, hili tatizo siyo la jana ama juzi, sasa likionekana halijafanyiwa kazi inaleta tafsiri ya kutojali wakati ni wajibu kulinda afya za watu wetu,” alisisitiza.
Kaimu Meneja wa Mwauwasa Wilaya ya Ilemela mkoani humo, Robert Lukoja alisema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo ni pamoja na wananchi kuunganisha mifumo ya maji ya mvua kwenye mifumo ya maji taka inayosimamiwa na mamlaka hiyo.
“Tutapita nyumba kwa nyumba kubaini nyumba zote ambazo zimeunganisha mfumo wa maji ya mvua kuingia kwenye mfumo wetu wa maji taka, ili kuzuia maji ya mvua yasiingie kwenye vituo vyetu. Hata waliofungulia maji kwenda kwenye mifumo ya maji taka waanze kuiondoa wenyewe,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Magomeni Kata ya Kirumba wilayani Ilemela mkoani humo, Abdallah Suleimani alisema baada ya mlipuko huo kutokea, mtaa wake uliathirika kutokana na kuwa na wagonjwa wengi (bila kutaja idadi) walioko hospitalini.
“Mpaka sasahivi tuna wagonjwa wengi hospitalini, lakini kwa mfumo uliokuwepo wa injini moja hauwezi kutusaidia Mwauwasa, ukiangalia sasahivi kwenye majumba yetu yamejaa kinyesi hadi juu, Mwauwasa wajitahidi wafunge injini mpya ili kusukuma maji taka,” alisema Suleimani.
Naye Mama lishe katika mtaa wa Kaluta jijini Mwanza, Aisha Mohammed alisema kwa kutambua uwepo wa mlipuko wa ugonjwa huo, amelazimika kuchemsha maji wakati wote kwa ajili ya kunywa na kunawa mikono kwa wateja wake ili kuwalinda wasipate maambukizi hayo.
“Hatuna namna kwa sababu tunategemea biashara hii kuhudumia familia zetu, kwa kuwa maofisa afya wameshatupatia elimu ya namna ya kujikinga ndiyo maana tumeweka miundombinu na tunawahimiza wateja kunawa kabla ya kula chakula,” alisema Aisha.