‘Wahimizeni watoto kusoma sayansi ili kuzalisha wataalamu wa sayansi’

Muktasari:
- Shirika la Wanawake Waelimishaji Afrika (Fawe) limezindua mpango mkakati wa miaka mitano (2024-2028), unaolenga kuwawezesha watoto wa kike na wa kiume kusoma masomo ya sayansi, ili kuziba pengo la kitaaluma na kuzalisha wataalamu zaidi nchini.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha watoto wakike bila kusahau wa kiume wanapata elimu hasa masomo ya Sayansi wadau wa maendeleo wamekuja na mpango mkakati kufanikisha hilo.
Wadau hao ambao ni Shirika la Wanawake Waelimishaji Afrika (Fawe) wamejitosa kupitia mpango mkakati wa kutowaacha nyuma wavulana kwa wasichana.
Hayo yamebainishwa kwenye hafla ya uzinduzi wa mpango mkakati huo wa Fawe wa miaka mitano unaoanza mwaka 2024 hadi 2028 hii leo Ijumaa ya Novemba 29, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mpango huo wenye kauli mbiu isemayo: kuwezesha kila mwanafunzi kuziba mapengo ili kujenga siku zijazo, utahakikisha jamii inashirikiana na wadau hao pamoja na Serikali kuwahimiza kundi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo Mratibu wa Taifa wa Fawe Tanzania, Neema Kitundu amesema sababu ya kuja na mpango huo ni kutokana na baadhi ya mila na desturi zinazowakandamiza kundi hilo.
"Pia, utaendelea kuleta tija na maendeleo ya elimu na tuna malengo kadhaa ambayo tutayafikia kupitia ushirikishwaji wa jamii," amesema.
Amesema jamii itashirikishwa katika mpango huo kupitia elimu inayohusu umuhimu wa watoto wa kike bila kusahau wa kiume.
"Aidha, Fawe inashirikiana na Serikali kuhakikisha watoto hao wanaacha kunyanyasika katika maendeleo ya kielimu.
Kwa upande wake Profesa wa Hisabati, Verdiana Masanja miongoni mwa waanzilishi wa Fawe amesema mabinti lazima wapate elimu nchini.
"Mkakati huu matokeo yake yatahakikisha wasichana na wavulana hawaachwi nyuma kwenye elimu," amesema Profesa huyo mstaafu.
Aidha mgeni rasmi wa hafla hiyo Zahara Rashid ambaye ni Ofisa Mdhibiti Ubora wa Shule Kanda ya Dar es Salaam amesema anaamini kwa kushirikiana na Fawe wataendeleza mabadiliko ikiwemo kushirikiaha jamii inayozunguka shule.
"Ushirikiano ni muhimu katika kuhakikisha wanaongeza nguvu kwa pamoja kufika walipokusudia," amesema.