Uongozi Dar es Salaam watakiwa kudhibiti malori kwenye makazi

Muktasari:
- Serikali imeutaka uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha unadhibiti malori yanayoegeshwa kiholela ili kupunguza adha inayoepukika
Pwani. Huenda foleni ya malori ndani ya Jiji la Dar es Salaam ikawa inaelekea ukingoni baada ya bandari ya Kwala kuanza kuhudumia mizigo inayoshushwa bandari.
Kutokana na hilo, Serikali imeutaka uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha unadhibiti malori yanayoegeshwa kiholela ili kupunguza adha inayoepukika.

Hiyo ni baada ya kontena 700 kuwa tayari zimehudumiwa katika bandari hiyo huku idadi yake ikikadiriwa kuongezeka zaidi pindi bandari hiyo itakapounganishwa na reli ya kisasa (SGR) hivi karibuni.
Bandari hiyo kavu inatarajiwa kuhudumia kontena 823 kwa siku zikiwamo zinazokwenda nchi jirani ikiwa ni sawa na kontena 300,395 kwa mwaka sawa na asilimia 30 ya kontena zinazohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.

Hayo yamesemwa leo Jumapili, Machi 16, 2025 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na wanahabari baada ya kutembelea mradi wa kongani ya viwanda mkoani Pwani sambamba na bandari kavu ya Kwala iliyojengwa chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
“Hivyo lengo la bandari hii la Kwala ni wafanyabiashara waje kuchukulia mizigo hapa kwa sababu hata wao foleni inawakera,” amesema Msigwa.
Mbali na kuchukulia mizigo bandari hiyo pia, amesema katika hatua nyingine ya kupunguza msongamano Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa barabara ya mzunguko Dar es Salaam ili malori ambayo yatalazimika kuingia katikati ya mji yapitie huko.
Kauli hii inakuja wakati ambao kumekuwapo na malalamiko ya foleni kubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam inayosababishwa na malori huku baadhi ya wakazi wakitaka zitengwe siku maalumu za magari hayo kuingia mjini.
Mbali na foleni inayosababishwa na magari hayo pia uegeshaji holela unaofanywa na madereva umekuwa ukifanya watumiaji wa barabara kushindwa kutumia hata njia za dharura pindi linapotokea tatizo na kuwafanya wakae barabarani muda mrefu.
“Kwa yale yanayopaki katika makazi ya watu ni jukumu la Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa na kuondoa kero kwa wakazi,” amesema.
Kufuatua changamoto hii, Februari 4, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alitangaza operesheni maalumu ya kukamata malori yanayopaki katika njia za dharura kinyume na taratibu huku akiwataka madereva na wamiliki kutumia maeneo maalumu yaliyopangwa.
Chalamila amesema barabara hizo za dharura siyo za wamiliki wa malori bali kwa ajili ya matumizi ya Watanzania, huku akieleza kwa msongamano uliopo ndani ya Jiji la Dar es Salaam si vyema barabara hizo zikazibwa.
"Hizi njia nazo zikijaa itafika wakati ambao mgonjwa anatakiwa kuwahishwa hospitali, tuna majambazi wamevamia mahali tunahitaji kuwakamata kwa foleni hizi na malori kuegesha ovyoovyo itafika kipindi tutashindwa," amesema Chalamila.
Mbali na kushindwa kutoa usaidizi wa dharura unapohitajika, pia amesema kuendelea kuwapo katika eneo hilo kunaweza kutumika kama maficho ya watu wenye nia ovu.
Alipoulizwa juu ya kile kilichosemwa na mkuu wa mkoa, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Issa John amesema mara nyingi wanaegesha malori katika maeneo hayo kwa ajili ya kusubiri kushusha mizigo jambo ambalo hawalipendi kwa sababu linawaongezea gharama.
"Sasa hivi wengi wanalazimisha kuegesha katika maeneo yenye bandari kavu, sehemu za kawaida hakuna; na kesho tutakuwa na mkutano na idara zote za Serikali zinazohusika nasi ikiwemo Latra tutakapozungumza huko tutapata majibu mazuri," amesema John.
Akiendelea kuzungumza, Msigwa amesema mbali na kupunguza msongamano malori ndani ya Jiji la Dar es Salaam, pia Bandari ya Kwala inalenga kutatua msongamano wa shehena bandarini.
Msongamano huo unatokana na ongezeko la mizigo inayoshushwa bandarini huku kukiwa na maeneo finyu ya kushushia mizigo.
“Katika Jiji la Dar es Salaam kulikuwa na jumla ya bandari kavu 11 zenye uwezo wa kuhifadhi kontena 24,300 kwa wakati mmoja. Kati ya hizo, pia kulikuwa na Bandari Kavu tisa zenye uwezo wa kuhifahi jumla ya magari 19,100 kwa wakati mmoja ambazo zilionekana kutokidhi mahitaji makubwa kwa wakati huo,” amesema Msigwa.
Jambo hilo ndiyo lilifanya kufikiwa uamuzi wa kujengwa bandari hiyo ili kusaidia kuongeza idadi ya mizigo inayohudumiwa na mapato ya Serikali.
“Pia, itapunguza gharama za uendeshaji, hivyo kuvutia wateja kutumia Bandari ya Dar es salaam jambo litakaloongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kikanda ukizingatia uwekezaji wa bandari za nchi jirani katika bandari kavu,” amesema.
Hiyo pia itaimarisha shughuli za kiuchumi na biashara za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa kupunguza msongamano wa magari uliopo sasa.
“Pia, tutaimarisha usalama barabarani kwa kuwa idadi kubwa ya shehena ya Bandari ya Dar es salaam itatumia usafiri wa reli, hii itaongeza maisha marefu ya miundombinu ya barabara za mikoa ya Dar es salaam na Pwani, utaongeza ajira kwa wakazi wanaoizunguka Bandari Kavu ya Kwala na Taifa kwa jumla,” amesema.
Mpaka sasa ujenzi wa mradi wa Bandari Kavu ya Kwala umetumia Sh83.246 bilioni na kazi zilizofanyika ni ujenzi wa ukuta katika eneo la hekta 60.
Hilo limeenda sambamba na kujenga Yadi yenye ukubwa wa hekta tano kwa kiwango cha zege ambao tayari imekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya Sh36.67 bilioni.