Ukweli kuhusu kifafa

Muktasari:
Wengi wanaamini ni ugonjwa unaoambukiza na pia unatokana na mapepo. Watu milioni moja wanaugua ugonjwa huo Tanzania
Si ugonjwa unaoambukiza, lakini uzoefu unaonyesha wagonjwa wake wamekuwa wakikosa ukaribu kutoka kwa wanajamii wengine.
Hawa ni wagonjwa wa kifafa, ugonjwa ambao wataalamu wanasema unatokana na hitilafu au jeraha katika ubongo linalosababisha mgonjwa kuanguka, kukakamaa, kuzimia na wakati mwingine kutoa povu mdomoni.
Hali huwa ngumu zaidi pale wagonjwa hao wanapoanguka; jamii inayowazunguka imekuwa ikishindwa kuwasaidia kwa wakati kwa kudhani ni mapepo.
“Jambo hili limefanya asilimia 75 ya wagonjwa wa kifafa Tanzania kupelekwa kutafuta tiba kwa waganga wa kienyeji na baadhi ya viongozi wa kidini wakiamini kuwa mgonjwa amevamiwa na mapepo mabaya au mashetani,” anasema Dk Edward Kija ambaye ni bingwa wa mfumo wa fahamu na ubongo kwa watoto wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Mbali na hilo pia asilimia 50 ya wanajamii bado wanaamini kuwa kifafa ni ugonjwa wa kuambukiza, hivyo huwanyanyapaa wagonjwa na kuwasababishia msongo wa mawazo.
“Hali hii hutokea pale mgonjwa anapopata degedege na kudondoka, wengi hufikiri kuwa ukigusa povu analotoa mdomoni au akitoa hewa chafu na ukanusa basi nawe utapata ugonjwa huo,” anasema na kuongeza: “Hali hii imekuwa ikifanya wananchi kushindwa kuwapeleka wagonjwa hospitali waweze kupatiwa tiba, kwa sababu ya imani kwamba wamerogwa au wameingiwa na mashetani.”
Huduma kwa mgonjwa wa kifafa
Anasema jamii inapaswa kutambua kuwa mtu anapokuwa katika hali hiyo anahitaji msaada wa haraka ikiwamo kwa kuangalia degedege hilo limetokea katika sehemu gani ili athari zaidi zisitokee.
“Watu wanaomzunguka mgonjwa huyu wanatakiwa kuangalia hali hiyo ikiwa imetokea katika sehemu ambayo huweza kumsababishia madhara zaidi kama kuangukia katika moto au maji, ni lazima aondolewe katika eneo hilo.
Wananchi wasiogope kumgusa mgonjwa aliyepata kifafa hawataambukizwa, wamtoe na wamuweke sehemu salama,” anasema.
Anasema pia kuna watu wenye hofu kuwa mgonjwa huyo anapodondoka atang’ata ulimi, hivyo humuwekea kijiko, kidole au kijiti, kitendo anachosema hakifai.
“Unapoweka kitu mdomoni, unaweza kusababisha njia ya hewa kuziba na hali ikiwa hivyo unaweza kuhatarisha maisha ya mgonjwa,” anasema Dk Kija
Anasema wakati huo pia mgonjwa hutakiwa kutolewa nguo au vitu vinavyombana mwilini mwake au kulegezwa na baada ya hapo anapaswa kulazwa kwa kutumia ubavu wa kushoto hadi pale atakapoamka.
“Hivyo kama unyanyapaa utaendelea kuwepo ni vigumu watu hawa kupata usaidizi wa haraka pale unapohitajika kutokana na watu kuona kama wataambukizwa,” anasema.
Tahadhari kwa wenye kifafa
Mwakilishi wa Chama cha wenye Kifafa Tanzania (Tea), Jane Mwenda anasema jamii inapaswa kutambua pia mtu aliye na ugonjwa wa kifafa hatakiwi kufanya kazi katika jua kali hata kama ni mwanafunzi.
“Tumeshafanya kampeni nyingi kwa sababu kuna walimu mtoto akikosa anamwambia apige magoti juani, lile ni kosa ndiyo maana siku hizi watoto walio na vifafa wana alama nyekundu katika bega ili kuwatambulisha wasifanyishwe kazi ngumu.”
“Lakini watu hawa pia hawaruhusiwi kuvuka barabara peke yao bila msaada wa mtu kwa sababu wanaweza kudondoka katikati ya barabara na watu wakamkimbia wakidhani kuwa ana mashetani,” anasema.
Anasema kwa wale wanaopatwa na kifafa usiku wanatakiwa kuwekewa magodoro yao chini ili wasidondoke.
Takwimu zinasemaje?
Wakati unyanyapaa ukitajwa kama moja ya kitu kinachofanya wagonjwa wa kifafa kukosa matibabu sahihi, takwimu zinaonyesha kuwa watu wanaoishi na kifafa ni zaidi ya milioni 60 duniani kote huku Afrika ikiwa ni bara ambalo limeathirika zaidi na tatizo hilo.
Kwa upande wa Afrika takwimu zinaonyesha kuwa katika kila watu 1000 basi 20 hadi 50 kati yao wanaishi na tatizo hilo.
Lakini pia kati ya wagonjwa milioni 60 wanaopatikana duniani asilimia 80 kati yake hutokea katika nchi zinazoendelea.
Kwa upande wa Tanzania zaidi ya watu milioni moja ni wagonjwa wa kifafa huku hali ikionekana kuwa mbaya zaidi katika mkoa wa Morogoro kijiji cha Mahenge kutokana na aina ya wadudu wanaopatikana huko.
Wadudu hawa mithili ya nzi waitwao ‘Simulium fly’ wanapatikana katika mito iliyopo maeneo hayo.
Nzi hawa wanapowang’ata watu huwaachia virusi vya ‘Oncocerca volvus’ ambavyo husababisha ugonjwa wa ‘Onchocerciasis’ ambao baadaye huwafanya kupata kifafa
“Jambo hilo liliifanya Serikali kuanza kuwapatia dawa za kuzuia ugonjwa huo mara mbili kila mwaka tangu mwaka 2007,” anasema Dk Mnacho Mohammed ambaye ni daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Muhimbili.
Imani potofu
Hapa nchini zaidi ya asilimia 36 ya watu bado wanaamini kuwa ugonjwa wa kifafa unatokana na nguvu za giza.
“Lakini asilimia 60 ya wagonjwa wanaofika kupatiwa matibabu hospitalini hufika mwaka mmoja baada ya kupata tatizo huku wengi wanoishi na kifafa Tanzania ni cha kiwango cha juu,” anasema Dk Mohammed.
Anaongeza: “Ni asilimia tano hadi 10 ya wagonjwa wa kifafa Tanzania ndiyo hupatiwa matibabu hospitalini.”
Dalili za mgonjwa wa kifafa
Wagonjwa wa kifafa huweza kuwa na dalili za aina mbili tofauti ikiwamo kutopoteza fahamu ila anakuwa hajui anachokifanya, kutetemeka kwa sehemu moja ya mwili kama kidole, mkono wote, upande mmoja wa mkono na mguu au upande mmoja wa uso.
Wakati mwingine kama hitilafu itatokea katika ubongo unaoendesha hisia kama harufu au usikivu dalili zake zinaweza kuwa ni kusikia harufu au kelele ambazo kiuhalisia hazipo.
Kama hitilafu itatokea katika ubongo unaoendesha kufikiri au kuongea, mgonjwa huyo ataanza kuongea ovyo, kucheka ovyo au kubadilika kwa hali na mapigo ya moyo.
Sehemu ya pili ya dalili za ugonjwa wa kifafa hutokea pale sehemu mbili za ubongo zinapopata hitilafu mgonjwa huweza kupoteza fahamu, kuanguka na kugeuza macho juu, kutetemeka mwili mzima na wengine hutoa povu mdomoni.
Pia kuanguka na kujigonga usoni hasa kwa watoto au kuzubaa na kuacha anachokifanya.