'Ukiona 2x3 haimaanishi unywe dawa asubuhi, mchana na usiku'

Mfanyakazi wa FCC akitoa maelezo kwa baadhi ya wananchi waliohuduria maonyesho yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) katika viwanja vya Mlimani City.
Muktasari:
- Ili kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya dawa na bidhaa feki TMDA na FCC, zimetoa elimu kwa wananchi.
Dar es Salaam. Wananchi wapewa elimu juu ya utambuzi wa bidhaa feki, kumalizika kwa muda wa matumizi pamoja na utumiaji sahihi wa dawa na uteketezaji wake.
Elimu hiyo imetolewa katika viwanja vya Mlimani City katika maonyesho yaliyoandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
Akizungumza na Mwananchi Online, Ofisa Mkaguzi wa alama za bidhaa Tume ya Ushindani (FCC), Grasiana Gallet amewataka wananchi kutembelea maonyesho hayo kwa ajili ya kupewa elimu kuhusu bidhaa feki.
Amesema kuna bidhaa nyingi feki ambazo zinauzwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu huku wakikopi kutoka kwenye kampuni nyingine.
Gallet amesema kutokana na ongezeko la bidhaa hizo wameona kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi wote waliopata fursa ya kutembelea katika banda lao na kuwaonyesha baadhi ya bidhaa kwa kuona utofauti wake.
"Tumekuwa na utaratibu wa kupita katika maduka kukagua bidhaa feki kwa kushirikiana na mamlaka husika kwa ajili ya kuteketeza bidhaa hizo zisiendelee kuingia katika mipaka ya nchi," amesema Gallet.
Pia amezungumzia kuhusu umuhimu wa kufahamu masuala ya uwekezaji kwenye taasisi kwa kufuata utaratibu ikiwepo uingiaji wa mikataba ya pande zote mbili ili kuepukana na migogoro isiyokuwa na tija.
Kwa upande wake, Ofisa Mahusiano wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba, Scholastica Njozi amesema kukosekana kwa elimu ya matumizi sahihi ya dawa na uteketezaji kunasababisha athari za kiafya.
"Tukiona dawa imeandikwa 2×3 haimaanishi kunywa dawa asubuhi, mchana na usiku bali kutumia mbili kila baada ya saa nane ili kuipa nafasi dawa kufanyakazi kwa usahihi na ndiyo maana tupo hapa kwa ajili ya kutoa elimu hiyo,"alisema Njozi.
Pia amesema wanaelekeza wananchi namna ya kuteketeza dawa ambazo zimepitwa na wakati baada ya kutumika kwani wengi wao wanazitupa kwenye takataka bila kufuata maelekezo.
"Baada ya matumizi dawa zinazobaki majumbani zinatakiwa kukusanywa na kupelekwa katika vituo vya afya kwa ajili ya kuteketeza kwa kuwa dawa hizo ni kemikali na tunazozitupanovyo zinatuletea madhara,"alisema.
Amesema wananchi wanatakiwa kuwa na utaratibu wa kuangalia muda wa matumizi ya dawa kama upo sahihi ili kuepuka na madhara pia kuangalia muhuri uliogongwa kwenye makasha ya dawa yaliyohifadhiwa.
Pia amewaomba Watanzania kuwa na utaratibu wa kupima na kupata ushauri wa madaktari kabla ya kunywa dawa ili kutibu ugonjwa sahihi na si kuhisia na kwenda kununua dawa kwenye maduka.
Haroub Kilonge Mkazi wa Mwenge amesema elimu hiyo isiishie kwenye maonyesho bali uwepo utaratibu mwingine ambao utasaidia kuwafikia watu wengi kwa kuwa si watu wote wanaofika katika eneo hilo.
"Wamefanya jambo la muhimu kuweka maonyesho hayo kwa kushirikisha wadau lakini wakiweza waende na sehemu nyingine ikiwepo mikoani ambako kunachangamoto za matumizi ya vitu feki itawasaidia.
Naye Doreen Shayo amesema aeona kuna umuhimu wa elimu kwenye upande wa vinywaji baada ya kutembelea banda la Fcc ili wananchi kutambua vinywaji wanavyotumia ni sahihi au feki.
"Nimepita hapa nimeonyeshwa vinywaji na mafuta ambavyo kwa mtu wa kawaida hawezi kutambua hadi elimishwe na wataalamu kutoka mamlaka husika,"amesema Doreen.