TPSF sasa shirikisho la sekta binafsi, yapanua wigo sekta mbalimbali

Mkurugenzi Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga akizungumza na waandishi wa habari na wahariri leo Alhamisi, Desemba 12, 2024, jijini Dar es Salaam kuhusu mabadiliko yalifanywa kwenye taasisi hiyo. Kushoti ni Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake nchini (TWCC), Mercy Sila. Picha na Aurea SImtowe
Muktasari:
Kuongezwa kwa uwakilishi ndani ya shirikisho hilo kunalenga kusaidia kupaza sauti zao katika utatuzi wa changamoto pale inapohitajika, tofauti na makundi hayo kusimama wenyewe kama ilivyokuwa awali.
Dar es Salaam. Wakati Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ikitanua wigo wa kuhudumia vyama vingi vya biashara na kuvipatia uwakilishi, imebadili jina na kuwa Shirikisho la Sekta binafsi Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Desemba 12, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TPSF, Raphael Maganga alipozungumza na waandishi wa habari na wahariri juu ya maazimio, maboresho na mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika kupitia kikao cha mwaka kilichofanyika mwishoni mwa Novemba.
Mganga amesema uamuzi wa kubadili jina hilo ni kuondoa mkanganyiko uliokuwepo kati ya wadau kwa kudhani TPSF ni shirika la kutoa misaada, badala kuwakilisha ya sekta binafsi.
“Sasa tunapoweka shirikisho linamaanisha kuwepo na umoja wa vyama vingi ili kuwa na sauti moja ya sekta binafsi, awali tulipokuwa tukitambulika kama taasisi tulikuwa tukipata maombi mengi ya kutoa misaada sasa tukaona uelekeo wa taasisi si huu kutoa misaada kwa mashirika mbalimbali,” amesema Maganga.
Amesema mtazamo huo ulikuwa ukikinzana na uelekeo wa TPSF ambao ni kujenga sauti moja ya wafanyabiashara wakati wanapozungumza na Serikali.
“Mabadiliko haya yanafanyika bila kuchukua madaraka wala mamlaka ya taasisi yeyote nchini, tutaendelea kuwa kama mwamvuli na vyama vitaendelea kufanya kazi zao kama kawaida na kufuata misingi ambayo wamejiwekea,” amesema Maganga.
Mabadiliko haya yanakwenda sambamba na mabadiliko katika safu ya uongozi ambapo kutakuwa na baraza la uongozi ambalo litashughulika na wanachama na changamoto zao na chini yake kutakuwa kamati tendaji itakayoongeza ufanisi katika utoaji wa uamuzi katika shughuli za shirikisho.
“Lengo la kufanya hivi ni kutenganisha uwakilishi wa wanachama na usimamizi wa taasisi,” amesema Maganga.
Hiyo ni tofauti na awali ambapo bodi ya TPSF ilikuwa inaunganisha majukumu ya uwakilishi na usimamizi ambayo ilileta mchanganyiko na sasa kila kitu kitasimama kivyake.
Kutokana na kutanuliwa kwa wigo huo, sasa shirikisho hilo limeongeza sekta ambazo zinakuwa chini yake ikiwemo wanawake, biashara za vijana, startups, ufugaji, uvuvi, afya, elimu, michezo, ubunifu, teknolojia na mawasiliano, uchumi wa kidigitali, pamoja na kuongeza uwakilishi kutoka Zanzibar.
Hilo linafanyika ili kuweka urahisi wa changamoto za makundi haya ambayo awali hayakuwapo ndani ya TPSF kupatiwa ufumbuzi, kwani wawakilishi wa kongani zake watakuwa miongoni mwa wajumbe wa katika katika Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).
Akizungumza katika mkutano huo, Maganga amesema hilo linafanyika ili kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na uwakilishi wao katika ngazi tofauti kwa kuboresha kuanzia ngazi za wilaya na mikoa na Taifa kwa ujumla.
“Mfano sekta ya afya haikuwapo, japokuwa tunatambua umuhimu na biashara yake nchini na hasa wakati huu ambapo tunasukuma sana utalii wa matibabu. Kwa hiyo tulikuwa na hospitali nyingi za binafsi, lakini hazipo katika mfumo,” amesema Maganga.
Kupitia mfumo huo mpya, sasa kutafanya jumla ya wawakilishi wa kongani kuwa 25 sawa na wale wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) badala ya konga 10 za awali.
Uundaji wa kongani hizo za biashara utatazamia sekta za kiuchumi, ili kuhakikisha kila sekta binafsi inawakilishwa ipasavyo na mapungufu yaliyokuwapo awali yanaisha miongoni mwa wadau na wanachama.
Akitolea mfano wa sekta uchumi, amesema anafahamu kuwa ndani yake kutakuwa na viwanda, lakini sasa kutakuwa na mgawanyo wa vile vikubwa na vidogo kwa mahitaji yao ni tofauti hivyo kufanya kila kundi kuwa na mwakilishi wake.
“Kila mmoja atakaa katika eneo lake, watajadili changamoto zinazoendana na eneo lao baada ya hapo zinangizwa katika baraza la uongozi. Hii itasaidia kuhakikisha kila mdau anashiriki kikamilifu na kupata majibu kwa wakati na uwazi pale inapohitajika,” amesema Maganga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzania Startups Association (TSA), Zahoro Muhaji amesema wakati sekta yao inaanza hakukuwa na kongani iliyokuwa ikiwawakilisha, hivyo walikuwa nje ya uwakilishi wa sekta binafsi jambo ambalo liliwafanya kushindwa kushiriki katika vikao muhimu.
Mabadiliko hayo yamewafanya kuwa sehemu ya sekta binafsi nchini wakati ambao uwekezaji wa unaofanywa katika mawazo bunifu unazidi kuongezeka.
“Katika kipindi cha miaka minne iliyopita kiasi cha fedha kilichowekezwa nchini kwetu kinafikia Dola milioni 300, taarifa za kimataifa zinasema kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu zaidi ya Sh100 bilioni zimewekezwa, ni sekta inayouzika na inawagusa vijana wengi wanaotoka vyuo na shuleni wanajiunga nayo,” amesema.