Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tope lafukia Reli ya Tazara Morogoro, abiria wakwama

Reli ya Tazara eneo la Kijiji cha Lumumwe, Kata ya Mlimba ikiwa imefukiwa na tope baada ya mvua kubwa kunyesha jana. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

Abiria wa treni ya Tazara wameshindwa kuendelea na safari baada ya reli kufukiwa na kifusi

Mlimba. Abiria 400 wakiwamo watu wawili wenye ulemavu na mgonjwa mmoja waliokuwa wakisafiri kwa treni ya Tazara kutoka Makambako kwenda Kidatu wameshindwa kuendelea na safari baada ya reli kufukiwa na kifusi cha tope kutokana na  mvua zinazoendelea kunyesha.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 2, 2024, Mkuu wa Stesheni ya Mlimba, Alex Mhiri amesema abiria hao wamekwama katikati ya Stesheni ya Lumumwe na Mlimba kwa zaidi ya saa 12.

Amesema  tayari jitihada za kuwaondoa katika eneo hilo kwa kutumia helkopta zimeanza ili kuwasogeza Stesheni ya Lumumwe kwa ajili ya kuwasafirisha kwa kutumia viberenge hadi Stesheni ya Ifakara.

"Treni hii ilikuwa inaitwa Udzungwa na imekuwa ikifanya safari kutoka Makambako hadi Kidatu; ilipofika katikati ya Stesheni ya Lumumwe na Mlimba ilikuta reli imefukiwa na kifusi cha udongo; dereva alipoamua kurudi nyuma alikutana tena na kifusi kingine, hivyo hawa abiria walijikuta wako katikati, mbele hawaendi wala nyuma hawarudi," amesema Mhiri.

Reli ya Tazara eneo la Kijiji cha Lumumwe, Kata ya Mlimba ikiwa imefukiwa na tope baada ya mvua kubwa kunyesha jana. Picha Hamida Shariff

"Baada ya kupata taarifa hizi tulianza kuwasiliana na viongozi na ilipofika jioni abiria 202 waliamua kutembea kwa miguu umbali wa kilometa 2 kwenda Stesheni ya Lumumwe kwa ajili ya kuona namna wanavyoweza kuendelea na safari.

“Wengine zaidi ya 50 wakiwamo wenye ulemavu wa macho, mwingine miguu pamoja na mgonjwa mmoja walibaki eneo la tukio kutokana na kushindwa kutembea," amesema Mhiri.

Pia, amesema abiria waliojinasua na kutembea hadi Stesheni ya Lumumwe, uongozi wa Tazara uliamua kuwasafirisha kwa kutumia viberenge hadi Ifakara na wale waliokwama waliendelea kusaidiwa chakula na maji kupitia kantini zilizopo ndani ya treni.

“Hali ya hewa bado sio nzuri kwa kuwa mvua inanyesha na udongo unaendelea kuporomoka, mpaka sasa kuna maeneo manane yenye vifusi na magogo ya miti yaliyofukia reli," amesema Mhiri.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amesema kwa sasa yuko njiani kuelekea Mlimba kwa ajili ya kuona namna ambavyo abiria hao wanaweza kuokolewa katika eneo hilo.

"Mwandishi nipo njiani naelekea huko kwenye eneo la tukio, lakini tayari jitihada wa kuwanasua hao waliokwama zinaendelea kupitia kikosi chetu cha maokozi, mvua kubwa inanyesha na hata barabara nayo kuelekea Mlimba imekuwa korofi, hivyo nikifika na kuona hali halisi nitatoa taarifa kamili. Kwa sasa naomba ifahamike hakuna vifo wala majeruhi abiria wote wako salama," amesema Kyobya.