Huduma treni ya Tazara sasa kwa simu ya mkononi

Muktasari:
Mfumo huo uitwao “Freight Management and information systems",amezindua leo Mei 8, 2018
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amezindua mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji shughuli za usafirishaji katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), ambao mteja ataweza kufuatilia shughuli za usafirishaji za mamlaka hiyo kwa kutumia simu yake ya kiganjani.
Mfumo huo uitwao “Freight Management and information systems",amezindua leo Mei 8, 2018 na utaanza kufanya kazi rasmi, ikiwamo kufuatilia mapato na matumizi ya uendeshaji wa treni kutoka Dar es salaam hadi Kapirimposhi (Zambia).
Akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa shughuli za usafirishaji kupitia mifumo huo katika kilomita 1,860 za reli hiyo, meneja mkuu wa Mkoa wa Tazara-Tanzania, Fuadi Abdallah amesema mfumo huo utatoa huduma kwa wateja na watumiaji wa huduma za Tazara kupitia programu ya Tazara.
"Kupitia mifumo huo unaweza kuangalia uendeshaji wa treni, ukusanyaji wa mapato ya usafirishaji, utaona njia yote ni treni gani imekwama, utaona taarifa za vituo vyote hadi mwisho wa safari. Itasaidia sana mifumo hii ambayo tumetumia miaka miwili kuandaa na watalaamu wetu, ni wa kwanza Afrika Mashariki,” amesema Abdallah.