‘Somo la afya ya akili liwepo shuleni’

Mkurugenzi wa Asasi ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY), Rustika Tembele akizungumza wakati wa mradi wa elimu ya akili katika shule ya sekondari Mashujaa jijini Dar es Salaam. Picha na Elizabeth Edward
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na taarifa za watoto na vijana kujiua nchini, imeshauriwa elimu ya afya ya akili ijumuishwe kwenye mitalaa na utoaji huduma za unasihi shuleni.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 700,000 hupoteza maisha kwa mwaka kutokana na kujiua.
Akizungumza juzi katika uzinduzi wa mradi wa elimu ya afya ya akili katika Shule ya Sekondari ya Mashujaa jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Asasi ya Tap Elderly Women’s Wisdom for Youth (TEWWY), Rustika Tembele alisema shule ni sehemu muhimu kwa elimu ya afya ya akili ili kuwanusuru watoto na vijana.
Mradi huo utatekelezwa na shirika hilo kwa kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi kuhusu afya ya akili na huduma za unasihi.
“Hali ni mbaya, tunashuhudia kila siku matukio ya watoto na vijana wadogo kukatisha uhai wao, ndiyo maana tumeona tuanze na shule, elimu ya afya ya akili itolewe huku chini kabisa.
“Tumeanza na Mashujaa sekondari, walimu watafundishwa kuhusu afya ya akili ili waweze kuwatambua kwa haraka watoto wenye matatizo ya afya ya akili,” alisema Tembele.
Pia, alisema zitatengenezwa kamati za wanafunzi watakaopewa elimu hiyo na kuandaliwa kuwasaidia wenye changamoto.
Ofisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Ubungo, Voster Mgina alisema tatizo la afya ya akili kwa wanafunzi lipo, hivyo mradi huo utasaidia kulipunguza.
“Athari za afya ya akili zinaonekana kwenye shule zetu na hii inatokana na mfumo wa maisha. Wapo wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, mapenzi katika umri mdogo, wanaopitia changamoto za ukatili na kuangukia kwenye msongo wa mawazo.
Msaikolojia tiba, Isack Lema alisema yapo mazingira tofauti yanayoweza kumsababishia mtoto kuwa na tatizo la afya ya akili na yanaweza kuchangiwa pia na mzazi.
Alitoa mfano ukali kupitiliza unaweza kumsababishia mtoto kupata ugonjwa wa wasiwasi uliopitiliza.