‘Serikali haitakuwa kikwazo kwa Azaki’
Muktasari:
- Asisitiza umuhimu wa elimu, uwekezaji, na nishati ya umeme kwa kukuza uchumi na kupunguza tatizo la ajira.
Arusha. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Serikali haitakuwa kikwazo kwa Asasi za Kiraia katika utekelezaji wa majukumu yao nchini.
Pia, amesisitiza kuwa kukuza uchumi wa Taifa kunahitaji kushughulikia mambo kadhaa, yakiwemo elimu, nishati ya umeme kwa viwanda na uwekezaji ambao utasaidia kupunguza tatizo la ajira.
Profesa Mkumbo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Septemba 9, 2024, wakati akizungumza na rais wa Taasisi ya Foundation For Civil Society (FCS), Dk Stigmata Tenga katika maadhimisho ya Wiki ya Azaki yanayofanyika jijini Arusha.
Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na asasi za kiraia na haitakuwa kikwazo katika kutekeleza shughuli zao.
"Niwahakikishie kuwa Serikali ya Tanzania haitakuwa kikwazo kwa shughuli za asasi za kiraia. Ni jukumu lenu kutafuta fursa," amesema.
Akizungumzia changamoto za kiuchumi, Profesa Mkumbo amesema cha msingi ni kufanya biashara na uwekezaji, ili kuongeza shughuli za kiuchumi na kutatua tatizo la ajira.
Ameeleza umuhimu wa kuwekeza katika elimu, akisisitiza uwekezaji wa kwanza wa nchi zilizopiga hatua duniani ni elimu na kila mtu anapaswa kuwa na uelewa wa msingi, kujua kusoma, kuandika na kupata maarifa.
Amesema uwekezaji katika elimu ya sekondari ni muhimu na kwamba Tanzania inakaribia kufikia asilimia 70 ya Watanzania wenye elimu ya angalau kidato cha nne.
Vilevile, amebainisha kuwa miundombinu ya umeme ni muhimu kwa kukuza uchumi wa viwanda, na ametoa mfano wa mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kama hatua ya kuongeza nishati.
Profesa Mkumbo amesisitiza umuhimu wa kuvutia wawekezaji wa ndani na kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara, ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, rais wa FCS, Dk Stigmata Tenga amesisitiza umuhimu wa mabadiliko kupitia ushirikishwaji wa wadau mbalimbali, ikiwemo asasi zinazosaidia makundi kama wanawake na watoto.
Amebainisha kuwa umaskini umeongezeka kutokana na changamoto kama elimu duni, kilimo na uzalishaji duni, miundombinu mibovu, na sera zisizo shirikishi.