Sababu tatu viwanda kudorora Tanga,  wananchi wapinga dhana ya uvivu

Mwoneknao wa mji wa Tanga. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Kati ya mwaka 1960 hadi 2000, Tanga ni miongoni mwa mikoa iliyokuwa ikisifika kuwa na viwanda vingi vilivyochochea ukuaji wa uchumi nchini, lakini baadaye vingi vilifungwa, kufa au kusitisha uzalishaji na kuathiri uchumi na ajira kwa wananchi.

Tanga. Nini kimesababisha mkoa wa Tanga kuporomoka katika sekta ya viwanda? Hili ndilo swali linagonga vichwa vya Watanzania wengi, huku  baadhi wakitaja sababu tatu kuwa ndio kiini, na kupinga dhana kuwa wao ni wavivu.

Kati ya mwaka 1960 hadi 2000, Tanga ni miongoni mwa mikoa iliyokuwa ikisifika kwa kuwa na viwanda vingi vilivyochochea ukuaji wa uchumi, lakini baadaye vingi vilifungwa, kufa au kusitisha uzalishaji, hali iliyochangia kuathiri  uchumi wa mkoa na ajira kwa wananchi wake na wale wa maeneo mengine ndani na nje ya nchi.

Katika sensa ya uzalishaji viwandani kwa Tanzania Bara kwa mwaka 2013, Tanga ilishika nafasi ya tisa kwa kuwa na viwanda 48, huku mkoa wa Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na viwanda 389 kati ya viwanda 1,322 vilivyokuwepo.

Taarifa ya takwimu hizo iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mbali na Dar es Salaam, mikoa mingine iliyoingia katika tano bora ni Arusha iliyokuwa na viwanda 87, Kagera (74), Mwanza (54) na mikoa ya Mbeya na Kilimanjaro ikiwa na viwanda 48.

Licha ya kuwepo sababu za msingi za kuporomoka kwa sifa ya Tanga kuwa na viwanda vingi ukiondoa Dar es Salaam, kuliibuka dhana kuwa tabia ya uvivu ya baadhi ya wenyeji wa mkoa huo pengine imechangia kukosekana nguvu kazi.


Walichosema wananchi

Baadhi ya wananchi ya mkoa wa Tanga wameeleza sababu iliyofanya viwanda vyake kutofanya kazi, huku wakishauri nini kifanyike ili kuvirejesha na kuanza kufanya kazi upya na kupinga vikali kuwa uvivu wa wananchi kuwa sababu.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema zipo sababu kuu tatu a wanazozifahamu kuwa kiini cha viwanda vingi visifanye kazi kwa muda mrefu ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi.

Juma Hamisi (56), amesema sababu ya kwanza iliyochangia viwanda kuacha kufanya kazi ni kodi iliyokuwa inatozwa ambayo iliwashinda wafanyabiashara na kuamua kuacha kuendesha viwanda hivyo, kwani hawakupata faida.

Ametaja sababu ya pili ni baada ya wananchi wengi hasa wenyeji kuacha kwenda kufanya kazi kwenye viwanda kutokana na kulipwa mshahara mdogo, hivyo walirudi kwenye kilimo ambacho waliona kina faida kwao.

"Viwanda vimekufa baada ya kufuatiliwa sana na mfumo kodi kuwa kubwa, wawekezaji wakaona faida wanayopata ni ndogo kuliko wanachotoa. Pia wazawa walianza kulipwa mshahara mdogo, hivyo wengi waliacha kazi,” amesema.

Hamisi ameongeza kuwa kutokana na hilo, wageni ndio walibaki kwenye viwanda, hivyo nguvu kazi ikapungua. “Hilo nalo lilisababisha uzalishaji kushuka, hali iliyochangia baadhi ya wamiliki viwanda kuacha uzalishaji,” amesema.

Hata hivyo, Salimu Kihiyo, amesema viwanda Tanga havijafa, ila vimehamishiwa na kupelekwa mikoa mingine, ikiwemo Dar es Salaam ambako vinaendelea kufanya kazi kama kawaida, huku  akitolea mfano kiwanda cha Nondo kimetolewa Tanga na sasa kipo Dar es Salaam.

Kihiyo ameongeza kuwa sababu inayotajwa kuhamishwa na kufungwa viwanda kwa mkoa wa Tanga ni  uvivu wa wananchi wake, jambo analolipinga akisema changamoto ni ujira mdogo ambao haukidhi mahitaji yao ya kifamilia.

"Tukaambiwa Tanga wavivu hatutaki kazi, vijana wanakaa masikani tu hawataki kazi, maana yake sisi hatuna shida na hela, tunatamani kulala tu, kitu ambacho sio kweli, wamehamisha viwanda kwa sababu zao binafsi,” amesema.

Kwa upande wake, Mwanahamis Juma (44), amesema viwanda hivyo vikifufuliwa, huenda tatizo la ajira kwa vijana wa mkoa wa Tanga lisingekuwa kubwa kama ilivyo sasa.

“Mimi wakati nakua nilikuwa nawashuhudia kaka zangu na ndugu wengine wakifanya vibarua viwandani, sikumbuki majina ila nilikuwa nawaona wanaamka asubuhi wanasema wanaenda kazi viwandani, ilikuwa nadra kuwakuta vijana wamekaa vijiweni,” amesema Mwanahamis.

Kauli ya TCCIA

Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara (TCCIA) Mkoa wa Tanga, Rashid Mwanyoka amesema viwanda vya mkoa huo havijakufa, shida walionunua kwa ajili ya kuwekeza hawajafanya hivyo na badala yake wamevifunga na kuondoka.

Amesema wanatafuta jukwaa maalumu la kuzungumza na wafanyabiashara kuwa ni hatua gani wachukue itakayosaidia kuvifufua viwanda hivyo na watakaoshindwa, chemba ifuatilie kuona itafanya nini, ili viwanda vifufuliwe na vianze kufanya kazi.

Naye rais wa TCCIA Tanzania, Vicent Minja amekiri viwanda vingi Tanga vimepewa watu wanaotakiwa kuanza kuvifanyia kazi, ili kuvifufua ila hawajafanya hivyo kwa muda mrefu kama walivyokubaliana.

Minja amesema kuna taratibu pia zinatakiwa kufanyika baina yao na Serikali ya mkoa, ili kuleta wawekezaji wapya kwenye baadhi ya viwanda na kurudisha hali kama ya awali ya mkoa huo uliovuma kwa kuwa na viwanda vingi miaka ya nyuma.

RC Matilda, Brela wafunguka

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema wamekubaliana kama Serikali ya mkoa, kuitisha kikao na wafanyabiashara walionunua viwanda hivyo, ili kufahamu kwa nini havifanyi kazi na kuwekeana muda wa kuvifungua.

"Tumekubaliana tutaitisha kikao cha pamoja na wale walionunua viwanda vyetu hapa Tanga kujua wamejipangaje na tuwawekee kabisa muda wa kuhakikisha kuna kitu kinaendelea vinginevyo wabadilishe huduma,” amesema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, kubadilisha huduma na matumizi ya viwanda hivyo itasaidia Tanga kuondokana na magofu kwenye sehemu ambazo watu wengine wanataka kuwekeza na wengine wamehodhi maeneo.

Kuhusu viwanda vilivyo kufa, Balozi Batilda amewataka wahusika waangalie ni taratibu gani watazitumia ili vifufuliwe na kufanya akazi.

“Vikifufuliwa vitasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, lakini pia maeneo ambayo sasa hayatumiki kwa sababu yamehodhiwa na viwanda hivyo mfu,” amesema.

Kwa upande wake, ofisa leseni mwandamizi kutoka Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (Brela), Rehema Kionaomela, amesema  Tanga kuna wafanyabiashara wanaohuisha leseni zao kila mwaka zikiwamo za viwanda.

Amesema kwa mwaka jana pekee, asilimia 97 ya wafanyabiashara wamefanya hivyo na kuashiria zipo biashara zinafanyika na waliohuisha ni wafanyabiashara wa kundi A wanaojihusisha na biashara za kusafirisha bidhaa ndani na nje ya nchi.

“Hii ina maana wapo wafanyabiashara wanaotumia viwanda hivyo ama kwa kuhifadhi bidhaa zao na kuzisafirisha nje ya nchi au vinginevyo, ndiyo maana wanahuisha leseni zao,” amesema Rehema.