Changamoto za kibiashara Kikwazo uchumi wa viwanda

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango
Muktasari:
Katika hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa bungeni Novemba 5, alisisitiza kuwa sekta ya viwanda ina jukumu kubwa la kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa viwanda.
Katika hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa bungeni Novemba 5, alisisitiza kuwa sekta ya viwanda ina jukumu kubwa la kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.
“Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano zitakuwa katika ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafananefanane na nchi ya kipato cha kati. Njia moja ya kutufikisha huko ni uendelezaji wa viwanda. Tutaanza na viwanda vilivyopo na kuhakikisha vinafanya kazi,” alisema Rais Magufuli.
Sekta ya viwanda inachangia asilimia nne ya Pato la Taifa, ikitoa ajira kwa Watanzania wengi wanaofanya kazi kwenye viwanda vidogo na vya kati. Sekta hii ina wajibu wa kukuza viwanda na kuleta mabadiliko ya kiuchumi kutoka kipato cha chini (kwa kutumia kilimo) hadi uchumi wa kati (kwa kutumia viwanda), hivyo Serikali haina budi kuboresha mazingira ya uwekezaji katika viwanda mbalimbali nchini.
Katika miaka ya hivi karibuni, sekta hii imekua kutokana na ukuaji wa viwanda vidogo kama vile viwanda vya nguo, viwanda vya ngozi na bidhaa zinazohusiana na ngozi, uchakataji, chakula, saruji, plastiki, uchapishaji, kuchomelea, utengenezaji samani na uhandisi kutokana na mazingira bora na marekebisho ya sera na mikakati iliyotayarishwa na wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Kiasi cha Sh107 trilioni zinahitajika kugharamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016 hadi 2021. Mpango huo utategemea sana makusanyo ya kodi na ukijikita katika kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda.
Alipowasilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alisema katika fedha hizo, Sh59 trilioni zitatolewa na Serikali, huku kiasi kilichobaki cha Sh48 trilioni zitachangiwa na sekta binafsi pamoja na mikopo na misaada kutoka nje.
Akitoa mchanganuo wa ugharamiaji mpango huo, Dk Mpango alisema kila mwaka Serikali itatoa Sh11.8 trilioni na kwamba katika kipindi cha miaka mitano ya mpango huo, Serikali itakuwa imetoa jumla ya Sh59 trilioni.
Alisema eneo la pili la gharama za mpango huo, litabebwa na sekta binafsi, mikopo na misaada kutoka nje na kuwa Serikali inaweka mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuwekeza katika miradi ya maendeleo.
Alisema nchi ikiwekeza kwenye ujenzi wa viwanda, huvutia misaada kutoka nje na hiyo imetokana na uzoefu wa nchi nyingine zilizoweka mikakati kwenye uwekezaji wa viwanda.
“Mantiki yetu ni kwamba nchi haina budi kuwa na mkakati mahususi wa kukusanya fedha kuwezesha utekelezaji wa mpango huu kwa ufanisi,” alisema Dk Mpango.
Dk Mpango alisema fedha za kugharamia mpango huo, watazipata kwenye makusanyo ya kodi na yale yasiyo ya kodi, ambapo Serikali imeainisha miradi mikubwa ya kielelezo kama ile ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na wa chuma wa Liganga.
Pia, eneo jingine ni ujenzi wa Reli ya Kati na kuboresha miundombinu ya usafiri. Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa mwaka 2016/17, umeweka vipaumbele vikuu vinne vilivyolenga ukuzaji viwanda kwa lengo la kuifanya nchi itimize malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Vipaumbele hivyo ni kuwa na viwanda vya kukuza uchumi, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na rasilimali watu, kuweka mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na kipaumbele cha nne ni kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
Katika vipaumbele hivyo, sekta zote zitaangaliwa na kuwekewa mikakati ya kuziboresha, ikiwamo viwanda, kilimo, afya, elimu, miundombinu, rasilimali watu kwa kuhakikisha nchi inafikia malengo yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Katika utekelezaji huo, viwanda vilivyokufa na vile visivyoendeshwa kwa tija vitafufuliwa na vingine kuanzishwa ili visaidie kuongeza uzalishaji wa mazao yenye thamani na kukuza kipato cha Watanzania na taifa kwa ujumla.
Dk Mpango alisema njia pekee ya uhakika ya kupata maendeleo endelevu ni kuwekeza kwenye viwanda na hiyo ndiyo njia inayotumiwa na nchi nyingi duniani na Tanzania imeamua kujipanga upya kiuchumi kufikia huko.
Changamoto
Sekta ya viwanda ndiyo hasa inayoshikilia ufunguo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kutokana na uwezo wake wa kutengeneza ajira nyingi.
Ripoti ya sekta ya viwanda katika ukanda wa mashariki mwa Afrika iliyotolewa mwaka jana inasema sekta hiyo si tu ni injini ya taifa katika kukuza uchumi, bali pia katika kubadili maisha ya wananchi.
Ripoti hiyo inasisitiza kuchochea matumizi ya teknolojia, uvumbuzi, uzalishaji pamoja na kuunganisha viwanda na sekta nyingine za uchumi.
Ripoti hiyo iliyozihusisha nchi za Tanzania, Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Shelisheli na Uganda, ni sehemu ya utafiti wa sekta ya viwanda uliodhaminiwa na Kituo cha Rasilimali Ukanda wa Mashariki mwa Afrika cha Benki ya Maendeleo ya Afrika. Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye alisema nchi yoyote inayotaka kujitegemea kwenye bajeti yake, lazima kwanza iimarishe uuzaji wa bidhaa zake zilizoongezewa thamani nje ya nchi.
“Nchi inayotumia bidhaa za nje kwa wingi kama Tanzania isitarajie kujitegemea kibajeti. Ili nchi yoyote iepuke misaada ya kibajeti kutoka kwa wahisani, lazima iimarishe mauzo ya nje,” alisema Simbeye.
Pamoja na umuhimu huo kwa uchumi na maisha bora ya jamii, sekta ya viwanda Tanzania bado inakabiliwa na changamoto nyingi kiasi cha kuchelewesha kufikia malengo yaliyokusudiwa. Kwa mujibu wa Simbeye, Tanzania haina sera madhubuti zinazolenga kuboresha na kuendeleza sekta ya viwanda. Sera zilizopo, alisema, zinawaruhusu wawekezaji kuja kufungua maduka nchini ili wauze bidhaa za nje badala ya kuzalisha hapa hapa.
“Kama Serikali yetu ingekuwa makini, ingewaruhusu wawekezaji wa maduka makubwa kuingiza bidhaa za nje kwa muda fulani kisha waanzishe viwanda,” alisema Simbeye.
Wakati ripoti hiyo ikionyesha kwamba sekta ya viwanda Tanzania imekuwa ikikua kwa asilimia tisa kwa mwaka, bado kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na malengo yaliyopo katika Dira ya Maendeleo-2025. Dira hiyo inataka kuona mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Tanzania unafikia asilimia 25, kama ilivyo katika nchi za Kusini Mashariki mwa bara la Asia ambazo zipo nusu ya safari kuelekea uchumi wa viwanda.
Ripoti hiyo inaonyesha kwamba kiwango kidogo cha biashara ya nje ya nchi pamoja na masuala kadhaa yanayohusu uanzishwaji na ufungaji wa kampuni kama sababu kubwa zinazokwamisha ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa biashara ya nje ya nchi ambayo hutengeneza mazingira ya kujifunza na kuongeza ujuzi, kudorora kwa biashara hiyo huchelewesha maendeleo ya haraka ya viwanda,” inasema ripoti hiyo.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa mwingiliano wa uzalishaji wa viwanda na sekta nyingine, ugumu katika uanzishwaji wa taasisi za biashara ni kikwazo kikubwa katika usambazaji wa bidhaa za viwandani,” kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Changamoto nyingine inatokana na kuwepo kwa miundombinu dhaifu ya kiuchumi ambayo ipo chini ya viwango vya kimataifa na hata vile vya bara la Afrika.
Umeme usiotosha ni mojawapo ya matatizo makubwa kabisa ya kimiundombinu Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa ukanda wa mashariki wa Afrika ndiyo una kiwango kidogo kabisa cha uzalishaji wa nishati na wadau wanasema kukatika ovyo kwa umeme pamoja na kuwepo kwa mitambo ghali ya kuzalishia, ndiyo vitu vinavyowaongezea gharama.
“Ukanda huu wa mashariki wa Afrika unazo barabara zinazoungana lakini ni duni, hali ambayo huongeza gharama za usafirishaji. Kukosekana kwa usafiri wa reli madhubuti kunaongezea matatizo ya usafirishaji wa nchi kavu. Kadhalika bandari za ukanda huu nazo bado zinafanya kazi chini ya viwango ikilinganishwa na washindani wao sehemu zingine.
“Suala la usimamizi wa usafishaji wa bidhaa huenda likabakia kama tatizo kubwa katika miundombinu linalokwamisha uendelezaji wa viwanda,” inasema ripoti hiyo.
Changamoto hizi ambazo zimetajwa katika ripoti, zinakwamisha maendeleo ya sekta ya viwanda nchini na iwapo hazitatatuliwa, wadau wanasema, hata malengo ya kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2020 yatakuwa safari ngumu.