Serikali na mikakati ya kufufua viwanda nchini

Kiwanda cha ngozi kilichopo Morogoro, ambacho kinahitaji uwekezaji mkubwa ili kuzalisha zaidi. Picha na Juma Mtanda
Muktasari:
Viwanda hivyo vilikuwa vinafanya kazi katika awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, lakini sasa vimekufa kutokana na uzembe na kuridisha nyuma sekta ya viwanda nchini.
VIWANDA vya uzalishaji ambavyo vipo nchini Tanzania vinaweza kuinua uchumi wa taifa kama Serikali na sekta binafsi zitaanzisha mpango kabambe wa kufufua baadhi ya viwanda vilivyokufa.
Tanzania kuna malighafi za kutosha ambazo zinaweza kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali na kuuzwa ndani na hata nje ya nchi, lakini tatizo hakuna viwanda vya kutosha vya kusindika na kutengeneza bidhaaa mbalimbali.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuna viwanda vingi ambavyo havifanyi kazi, kutokana na ukosefu wa mitambo imara na hivyo kusababisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kuwa chini.
Lakini si hayo tu bali kuna tatizo la kutumia ardhi yetu yenye rutuba ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha mazao mbalimbali ambayo kama yakisindikwa, yangesaidia kuinua pato la taifa.
‘Viwanda vingi vimekufa’
Kuna baadhi ya viwanda vilivyokuwa vikifanya kazi miaka ya nyuma hasa katika serikali ya awamu ya kwanza naya pili, lakini sasa havipo tena baada ya watu waliokabidhiwa kushindwa kuviendeleza.
Baadhi ya viwanda hivyo ni kama kiwanda cha nguo cha Urafiki Garments kilichopo ubungo, Tanzania Dairies limited ambacho kilikuwa cha maziwa, Ubungo Spining mill, pamoja na cha Zana za kilimo (UFI) ambacho kilikuwa maalum kwa ajili ya kutengeneza zana za kilimo. Vingine ni Tanzania Sewing Thread na Poly Sacks. Viwanda hivyo hivi sasa havifanyi kazi.
Viwanda hivyo vilikuwa vinafanya kazi katika awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere, lakini sasa vimekufa kutokana na uzembe na kuridisha nyuma sekta ya viwanda nchini.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda, alitoa ripoti inayoonyesha jinsi hali ya viwanda ilivyo barani Afrika.
Ripoti hiyo ilijikita zaidi kwa nchi ya Tanzania ikionyesha jinsi viwanda vyake vilivyodorora.
Kigoda anaelezea kwamba ripoti hiyo imejikita zaidi kutatua matatizo mbalimbali ambayo yameikumba sekta ya viwanda.
Anasema wanajipanga jinsi ya kutatua matatizo yaliopo kwenye sekta hiyo ili kufufua viwanda na kuleta maendeleo nchini.
Dk Kigoda anasema Serkali itaweka mazingira bora kwa ajili ya kuvutia wawekezaji, kuboresha na kulegeza masharti kwa wawekezaji, kuboresha miundo mbinu, na kupambana pamoja na urasimu.
“Ripoti hii imejikita zaidi jinsi ya kutatua matatizo mbalimbali zinazoikumba sekta ya viwanda nchini, naamini kwa kufanya hivi sekta ya viwanda itainuka upya,” anasema Kigoda.
Dk Kigoda:Tufufue viwanda vyetu
Kutokana na hali hiyo Serikali na sekta binafsi zinatakiwa kuungana ili kufufua uchumi kupitia viwanda na siyo kutegemea kilimo tu kama uti wa mgongo wa taifa.
“Mageuzi ya fikra zetu yanahitajika kuitazama upya sekta ya viwanda na kuacha kusema kwamba kilimo pekee ndio uti wa mgongo wa taifa letu kwani hata nchi zilizoendelea zinathamini viwanda pia,” anasema Kigoda.
Waziri huyo anafafanua kwamba vitendo vinahitajika zaidi kufufua sekta ya viwanda.
“Lazima tuondokane na nadharia na kujikita kwenye vitendo ili Wizara ya Viwanda na biashara ipanue soko la ndani na nje, lakini hili litafanikiwa baada serikali na sekta binafsi kuungana pamoja,”anasema Kigoda.
Anabainisha kwamba tatizo kubwa linaloikumba sekta ya viwanda nchini ni ukosefu wa mitaji na tatizo la kupatikana kwa soko la uhakika la kuuza bidhaa za viwandani.
Anafafanua kwamba matatizo hayo yanasababisha kudorora kwa biashara katika nchi za Afrika.
“Ukosefu wa mtaji kwa wafanyabiashara ni changamoto kuu inayowafanya washindwe kuwekeza kwenye viwanda, hadi kufikia biashara katika nchi.
Kutokana na kuwapo kwa tatizo hilo biashara imedorora kwa sababu imekuwa ikifanyika kwa asilimia 10 tu ukulinganisha na nchi nyingine duniani.
Viwanda vinatumia mitambo duni
Katika hatua nyingine wizara husika kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), imeandaa ripoti ambayo imechambuliwa kiundani kuhusu maendeleo ya viwanda Tanzania ili kuonyesha matatizo yanayokabili viwanda nchini.
Mmoja wa waandaji wa ripoti hiyo Falicia Massak anasema viwanda havijatengeneza ajira kwa Watanzania hasa vijana kwa sababu hakuna viwanda vikubwa vinavyotumia mitambo ya kisasa.
Massak anasema hali hiyo Anaeleza kwamba Tanzania hatuna viwanda vikubwa ambavyo vinatumia mitambo ya kisasa kwa ajili ya kugeuza malighafi kuwa bidhaa.
“Hapa kwetu, Tanzania iko nyuma kiviwanda, tunahitaji kuwa na viwanda vikubwa venye mitambo ya kisasa tena ambavyo vimesambaa nchi nzima kwa sababu viwanda vingi vipo Dar es Salaam na vichache Arusha ambavyo vipo nyuma kimaendeleo.
“Serikali na sekta binafsi zinatakiwa ziungane kwa pamoja ili kufufua sekta ya viwanda upya,”anasisitiza Massak.
Katika hatua nyingine anasema bidhaa za Tanzania hazijapata soko la uhakika duniani, na kusababisha kutegemea zaidi soko la ndani.
Massak anasema ujuzi wa wafanyakazi viwandani hauridhishi kwa sababu hakuna mahusiano mazuri kati ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda.
Anabainisha kwamba mazingira hayo yanasababisha viwanda vingi nchini kuzalisha bidhaa duni ambazo zinakosa soko duniani.
Mshiriki katika maandalizi ya ripoti hiyo Neema Rutatina anasema sera ya viwanda inatakiwa iangaliwe kwa undani zaidi kabla ya viwanda hivyo kufufuliwa ili visirudi tena nyuma kama awali.
Bajeti ya viwanda
Kwa mujibu wa Rutina anasema Serikali inatakiwa kuongeza bajeti kwenye viwanda pamoja na kuongeza wawekezaji kwenye sekta ya viwanda ili kufikia lengo kuinua uchumi kupitia sekta ya viwanda.
“Serikali inapaswa kuweka bajeti zaidi kwenye sekta ya viwanda na kuongeza wawekezaji ili kukuza uchumi,” anasema Rutatina.