Rais afanya mabadiliko madogo baraza la mawaziri, amrejesha Kairuki amuondoa Mulamula

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha wawili, kumuondoa mmoja na kumrejesha Angella Kairuki bungeni na kumteua kuwa waziri.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha wawili, kumuondoa mmoja na kumrejesha Angella Kairuki bungeni na kumteua kuwa waziri.

Mabadiliko hayo yametangazwa usiku wa leo Jumapili, Oktoba 2, 2022 na Zuhuru Yunus, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ya Tanzania.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua Kairuki kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania kisha kumteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kairuki aliyewahi kuwa waziri katika wizara mbalimbali katika utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete na ya tano ya Hayati John Magufuli zikiwemo madini na ile ya uwekezaji, anachukua nafasi ya Innocent Bashungwa.

Anarejea tena bungeni na kwenye baraza la mawaziri, baada ya kushindwa katika mchakato wa kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwani ubunge wa Same Magharibi, Mkoa wa Kilimanjaro.

Kairuki aliyezaliwa Septemba 10, 1976, amekuwa mbunge wa viti maalum kuanzia mwaka 2010 hadi 2020 alipojitosa jimboni na kushindwa.

Bashungwa aliyekuwa Waziri wa Tamisemi yeye amehamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuchukua nafasi ya Dk Stergomena Tax.

Katika mabadiliko hayo, Rais Samia amemweka kando, Balozi Liberata Mulamula aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na nafasi yake akimteua Dk Tax.

Balozi Mulamula amehudumu katika wizara hiyo kuanzia Machi 31, 2021 alipomteua kuwa Mbunge kisha kumteua kuwa waziri wa mambo ya nje kuchukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi.

Dk Tax, aliyehudumu nafasi ya Katibu Mtendaji Jumuiya ya Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia mwaka 2013 hadi 2021 alipomaliza muda wake, alikuwa mwanamke wa kwanza, kuongoza wizara ya ulinzi.

Rais Samia alimteua Dk Tax kuwa mbunge na waziri wa ulinzi, Septemba 12, 2021 akichukua nafasi ya Elias Kwandikwaa mbaye alifariki dunia Agosti 3, 2021 jijini Dar es Salaam.