Polisi Njombe yamsaka aliyemjeruhi mpangaji wake, kisa wivu wa mapenzi
Kamanda wa polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga.
Muktasari:
- Shuhuda Happiness Mwinuka alidai mama mwenye nyumba alimuita mpangaji wake nje kuzungumzia tuhuma za uhusiano na mume wake.
Njombe. Jeshi la Polisi mkoani Njombe linamtafuta Leonola Madilo, mkazi wa Mtaa wa Lunyanywi, kwa tuhuma za kumjeruhi mpangaji wake, Yusta Mbilinyi (21), kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kisha kutoroka.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, ambapo Leonola anamshuku Yusta kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wake, Noel Ngole.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 4, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amesema jeshi hilo linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa ili achukuliwe hatua za kisheria.
Kamanda Banga amesema tukio hilo lilitokea Juni 1, 2026, saa tatu usiku katika Mtaa wa Lunyanywi, ambapo Yusta Mbilinyi alijeruhiwa kwa kitu chenye ncha kali kwenye mkono na mguu wa kushoto.
Amesema baada ya kutekeleza tukio hilo, mtuhumiwa alitoroka na hadi sasa Jeshi la Polisi linaendelea na msako ili akamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kujibu tuhuma zinazomkabili.
"Sababu ni mtuhumiwa kumtuhumu Yusta ambaye ni majeruhi kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mume wake, kwa hiyo sababu kubwa ni wivu wa mapenzi," amesema Banga.
Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Lunyanywi, Aida Mwaka amesema baada ya kupata taarifa kuhusu tukio hilo walifika nyumbani hapo na kutoa msaada kwa msichana huyo kwa kumpeleka hospitali.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Happiness Mwinuka amesema mama mwenye nyumba alimuita mpangaji wake nje na kumuuliza juu ya uhusiano na mume wake lakini, baada ya muda mfupi wakaona mama huyo anarudisha panga jikoni na kuondoka.