Mtoto wa miaka minane auawa na fisi

Muktasari:
Mtoto Pendo Philipo mwenye umri wa miaka minane amefariki dunia baada ya kushambuliwa na fisi wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Mwanza. Mtoto Pendo Philipo mwenye umri wa miaka minane amefariki dunia baada ya kushambuliwa na fisi wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 26 katika Kata ya Mantare wakati mtoto huyo alipokuwa na wenzake watatu wakiokota kuni porini.
Alisema Pendo alisema anasoma darasa la kwanza Shule ya Msingi Ishingisha wilayani Kwimba.
“Fisi huyo aliwafukuza na kumkamata mtoto huyo kisha kumjeruhi na kumsababishia kifo,” alisema Kamanda Muliro
Alisema polisi kwa kushirikiana na idara ya wanyamapori na vyombo vingine vya usalama vinafanya jitihada kumsaka na kumdhibiti fisi huyo ili asilete madhara mengine. Tukio kama hilo lilitokea mwaka jana, mtoto mwenye umri wa miaka saba aliyekuwa anasoma darasa la kwanza Shule ya Msingi Mwaniko wilayani Misungwi aliuawa na fisi majira ya jioni alipotoka nje ajisaidia.
Hata hivyo, katika tukio hilo, waliuliwa fisi 23 baada ya vikundi vya jadi kutoka vijiji vitatu vya Sumbugu, Igongwa na Nduhwa kushirikiana kuwasaka wanyama hao.