Mama mbaroni akituhumiwa kuua wanawe wawili

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga.
Muktasari:
- Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga amesema uchunguzi wa awali umeonyesha mwanamke alikuwa na msongo wa mawazo
Mbeya. Jeshi la Polisi Mbeya linamshikilia Dainess Mwashambo (30) mkazi wa Kijiji cha Mashese Wilaya ya Mbeya kwa tuhuma za kuwaua watoto wake wawili kwa kuwanywesha sumu ya kuulia magugu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga ameiambia Mwananchi Digital leo Jumamosi Machi 9, 2024, kuwa chanzo ni msongo wa mawazo baada ya kutuhumiwa kuhusika na wizi kwenye ofisi ya Serikali ya mtaa.
Kamanda Kuzaga amesema tukio hilo lilitokea Machi 5, 2024 wakati mtuhumiwa alipokuwa nyumbani kwake Kijiji cha Mashese aliwanywesha sumu ya kuulia magugu watoto wake na kusababisha vifo vyao baada ya kufikishwa Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
“Mtuhumiwa baada ya kuwanywesha sumu watoto wake naye alikunywa kwa lengo la kutaka kujiua, lakini wote walikimbizwa Hosptali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na kwa bahati mbaya watoto hao walifariki,” amesema.
Kamanda Kuzaga amesema kuwa miili ya watoto hao inafanyiwa uchunguzi na madaktari kabla ya kutoa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi huku mtuhumiwa akiwa katika ulinzi mkali wa.
Hata hivyo, Kamanda Kuzaga ameonya na kuwataka wananchi wanapokuwa katika hali ya msongo wa mawazo ni vyema kutoa taarifa ili kupatiwa msaada wa kisaikolojia na kutafuta msaada wa kisheria.
“Nitoe rai kwa wananchi kuachana na uamuzi mgumu pindi wanapokuwa na changamoto badala yake watafute ushauri au kufuatia sheria inavyoelekeza ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwamo kukatisha ndoto za malaika wasio na hatia,” amesema.
Wakati huo huo msaidizi wa dawati wa jinsia na watoto wa Jeshi la Polisi, Loveness Mtemi ameitaka jamii kuwa na hofu ya Mungu kwa kuachana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wasio na hatia.
“Inapotokea changamoto kwenye maisha, wanawake na wanaume zungumzeni ili kuepuka vitendo vya ukatili ikiwamo mauaji kwa kuwa ninyi ndio mlikubaliana kupata familia ili kuwatua mzigo watoto wasio na hatia,” amesema Loveness.