Prime
‘Lambalamba’ wazua taharuki Kigoma

Kigoma. Taharuki imeibuka mkoani Kigoma, baada ya kundi la watu wanaojiita waganga wa kienyeji maarufu kama Kamchape au Lambalamba kuibuka mkoani humo na kutangaza kuwa na uwezo wa kutoa uchawi.
Watu hao ambao hufika katika vijiji vya mkoa huo na kuunda vikundi vidogo vidogo, kisha kuzunguka katika miji ya watu kuwashawishi kutoa uchawi kwa kuwatoza Sh5,000 kwa kila kaya ili kukamilisha kazi ya kutoa uchawi kutoka kwenye nyumba za watu.
Kutokana na sababu kadhaa ikiwemo maradhi, kukosa tiba sahihi hospitalini na ugumu wa maisha, baadhi ya wananchi wakiwemo viongozi wa Serikali za mitaa huwapokea na kuruhusu kufanyika shughuli hiyo.
Watu kadhaa wamepata madhara ya kupoteza mali, kuchomewa nyumba na hata kushambuliwa kutokana na kazi za waganga hao kama ilivyoshuhudiwa katika tukio la Septemba 12, mwaka huu ambapo kwa ushauri na maelekezo ya Lambalamba, kundi la wananchi wa Kijiji cha Mahembe Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma lilivamia nyumba ya mfanyabiashara, Khalid Mwela maarufu “Osama” na kuiteketeza kwa moto na kuharibu mali.
Uvamizi huo ulifanyika baada ya mfanyabiashara huyo kugoma kumruhusu Lambalamba kuingia nyumbani kwake ‘kutoa uchawi’ uliodaiwa kuwepo.
Mke wa mfanyabiashara huyo, Rehema Khalidi alisema siku hiyo mchana, kundi hilo la Kamchape lilifika katika mlango wake mkubwa wa nyumba yao uliokuwa umefungwa na kuanza kupiga ngoma na walipoona mlango haufunguliwi walianza kuchimba chini na kuweka vitu vinavyodaiwa kuwa ni dawa.
Alisema baada ya muda, kundi hilo walikuwa wamefika nyumba ya tano kutoka kwake, askari walifika eneo hilo na kuanza kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi.
Rehema alisema baada ya wananchi kutawanyika, ghafla walirudi na kusimama katika mlango wa nyumba yao na kusema wabomoe nyumba na kuichoma moto, jambo ambalo lilimshtua.
“Kama ingekuwa ni uchawi wangetoa na kwenda zao, sikuona sababu ya kufanya uharibifu wa mali na kuchoma nyumba moto, kwani wamechoma kila kitu kilichokuwa ndani, hali iliyosababisha watoto kushindwa kwenda shule.
“Hakuna kitu tulichookoa kwenye nyumba, nguo tulizovaa ndio hizi tulizobakia nazo. Pia kulikuwa na mazao ndani kama maharage na mahindi yote yameteketea kwa moto,” alisema Khalid.
Alisema wanaomba Serikali ifanye uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo na iwakamate watu wote waliohusika bila kufumbia macho na hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Mdogo wa mfanyabiasha huyo, Yusuf Ali alisema siku moja kabla ya tukio alishusha mzigo wa mahindi gunia 70 nyumbani kwa kaka yake ambako ni eneo analohifadhi kila mara, kwa ajili ya kwenda kuyauza kama ilivyo kawaida yake.
Alisema siku ya tukio hakuwepo nyumbani, alikwenda kwenye shughuli zake nyingine na aliporudi usiku alikuta watu wengi nyumbani na kuona uharibifu wa mali ikiwemo kuungua kwa nyumba.
“Nilikwenda kuangalia magunia yangu ya mahindi, lakini sikuyakuta yote. Nilikuta magunia saba kati ya 70 niliyokuwa nimeacha nyumbani,” alisema Ali.
Ali alisema magunia waliyochukua yana thamani ya Sh7 milioni na ndio ulikuwa mtaji wa biashara yake na kwa sasa hajui ataishije kwa kuwa biashara hiyo ndio ilikuwa inamsadia kuendesha maisha yake.
Jirani na shuhuda wa tukio hilo, Omary Juma alisema kundi hilo linafanya kazi ya kutapeli baadhi ya wananchi kutokana na uelewa mdogo walionao, kwani kuna baadhi ya nyumba wanaingia na kusema wamekuta uchawi na kumtaka alipe faini ya fedha na kama hana wanachukua vitu vyake vya ndani ikiwemo kupiga mnada mazao yake.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mahembe Kati, Dunia Ngali alisema kundi hilo lilitawanywa na polisi kwa kutumia mabomu ya machozi na kwamba wao kama Serikali ya kijiji wanalaani tukio la baadhi ya wananchi kuchoma nyumba ya mwanakijiji mwenzao na kufanya uharibifu wa mali.
Jeshi la Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu aliwaonya wananchi kuacha si tu imani za kishirikina, bali pia kushiriki matukio ya uvunjifu wa amani na usalama kwa sababu watawajibishwa kisheria.
“Hadi sasa watu zaidi ya 100 wameshakamatwa na kuhojiwa kuhusiana na tukio la kuchomba nyumba katika Kijiji cha Mahembe Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, wote ambao upelelezi utathibitisha kuhusika watafikishwa mahakamani,’’ alisema Kamanda Makungu.
RC atahadharisha
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye aliwaonya wananchi kujihadhari na kujiepusha na watu wanaofika kwenye maeneo yao kujitangaza kuwa na uwezo wa kutoa uchawi, akisema ni matapeli wenye nia ya kutumia matatizo ya watu kujipatia fedha.
“Watu hawa wanachezea saikolojia na imani za watu, wanapaswa si tu kupuuzwa, bali pia kuripotiwa kwenye vyombo vya dola, ili hatua za kisheria zichukuliwe kabla ya madhara kama tulivyoshuhudia katika Kijiji cha Mahembe Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,’’ alisema Andengenye.
Alisema kuna ushahidi wa vitendo vya kitapeli vilivyowahi kufanywa na kundi la wanaojiita waganga wa kienyeji wenye uwezo wa kutoa uchawi ikiwemo kukutwa na mali wanazochukua kutoka kwenye nyumba za wanaodai kuwa ni wachawi.