Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipato cha mke kinavyoondoa ‘kichwa cha familia’

Muktasari:

  • Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanaume wanaopitia changamoto kwenye ndoa, Ernest Komba alisema kuwa hakuna tena kuheshimiana pale mke anapomzidi mumewe kipato.

Kuna wanaume wanaoishi na wake zao wenye kipato kikubwa kwa furaha, lakini kwa wengine ni mateso.

Na hili linatokana na ule usemi usemao “mwenye pesa ndiye mwenye sauti’, ikimaanisha kwamba kama huna pesa hata mawazo yao au ushauri hauna umuhimu.

Lakini hii ni tofauti na wanaume kwa wake zao kwa kuwa, imezoeleka katika jamii mbalimbali mwanamume ndiye kichwa cha familia kwa kuihudumia kutokana na kipato anachokipata ni kikubwa kuliko mkewe.

“Mke wangu ndiye ana sauti, imesababisha hata watoto hawanipi ile heshima tena, wanaona kama sina msaada kwao, asilimia kubwa ya mahitaji yao yanafanywa na mama yao,” anasema Paulo Joseph.

Mume huyo anasema kutokana na kipato chake kuwa kidogo, amegeuzwa kama mtumishi wa nyumbani kwa kuwa tu, mkewe ndiye ‘bosi’ kwenye familia.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanaume wanaopitia changamoto kwenye ndoa, Ernest Komba alisema kuwa hakuna tena kuheshimiana pale mke anapomzidi mumewe kipato.

“Wachache sana huwa na ustahimilivu, lakini ni mmoja kati ya 100, lakini wengi wao akiwa na kipato kukuzidi dharau inaongezeka,” alisema Komba.

Mwanamume mwingine ambaye mkewe kamzidi kipato aliyeomba hifadhi ya jina anasema amelazimika kuishi naye kwa akili tu na kujishusha ili mambo yake yaende.

“Mke wangu nilimkuta ana watoto na kipato kunizidi kutokana na biashara zake anazofanya, sipewi ile heshima ya baba, wakati mwingine mimi ndiyo natumwa sokoni mabinti zake wapo, hawaniheshimu, ndiyo hivyo nimejishusha ili mambo yangu yaende,” anasema mwanamume huyo ambaye hajabahatika kupata mtoto.

Mchambuzi wa masuala ya uhusiano, Deogratius Sukambi anasema kuna athari nyingi kwa mke kumpita mume kipato, athari inayoweza kuigharimu familia baadae.

“Kuna tofauti kati ya kuwa mwanamume na mume…mwanamume ni kiumbe na mume ni mamlaka, sasa inapotokea mamlaka imezidiwa kiuwezo na aliye chini ya mamlaka hiyo athari kubwa ya kwanza inamuondolea mume kujiamini,” anasema Sukambi.

Muktadha wa ndoa ukoje?

Akitolea mfano wa muktadha wa ndoa, anasema mume ndiye kiongozi, kichwa cha familia na anapaswa kumhudumia mkewe hata kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya nchi.

Sukambi anasema anapozidiwa kipato itamuondolea ujasiri wa kudili na mahitaji ya mkewe.

“Huyu mume anaweza kuwa na uwezo wa kumnunulia nguo ya gharama ya kawaida mkewe, lakini akashindwa kwa kuamini kwa uwezo wa mkewe hawezi kujinunulia nguo ya gharama hiyo, japo kufanya hivyo ni upendo lakini katika saikolojia ya mwanamume inamuondolea ule ujasiri wa kuona anamudu mahitaji ya mkewe,” anasema Sukambi.

Anasema kingine inamuondolea mamlaka ya kiuongozi kama mume, hivyo kuangaliwa kwa taswira hasi.

“Unapokuwa katika nafasi kama baba, utataka kutoa dira kwa familia yako, kuonyesha mnaelekea wapi na kufanya uamuzi wa msingi, ikiwamo kuamua watoto wasome shule gani, wavae mavazi gani na mambo kama hayo, hivyo unapokosa mamlaka hiyo sauti ya baba inakosekana,” anasema Sukambi.

Hali hiyo anasema inaweza kuathiri uhusiano wa mke na mume kwa kuwa baba akipoteza ujasiri wa kuongoza hakuwezi kuwa na mawasiliano mazuri na mkewe.

“Wakati mwingine mke anaweza kuhamasika kwa nia njema tu kufanya vitu, lakini mara nyingi kwa mume inatafsiri ya kudharauliwa.

“Wanaume wengi tunapenda kuthibitisha uanaume wetu kwa namna tunavyotaka na kwa nafasi tunayotaka, ikitokea mke akachelewa kwa sababu za msingi, wanaume wanatafsiri kudharauliwa kwa hisia za kuzidiwa kipato na hapo ndipo shida zinaanza,” anasema.


Watoto nao huathirika?

Sukambi anasema kama wazazi hawataruhusu hilo lisijionyeshe kwa watoto basi hakuna athari, kinyume na hapo, athari ni kubwa.

“Mama atakaporuhusu watoto walione hiyo ‘gap’ basi ni shida, kwani mambo hayo yanatokea chumbani, huko nje wazazi ndiyo wanaruhusu yaonekane na watoto kufahamu mhusika wa mahitaji yao ni mama.

“Athari za kisaikolojia kwa mtoto anayeona mama ndiye anahudumia mahitaji yake huwa mbaya kuliko tunavyofikiria, mfano kwa mtoto wa kiume ambaye amekuwa akiona mama ndiye anamlipia ada, mavazi, chakula na mahitaji yake mengine, huwa inamtengenezea fikra ya kwamba ni wajibu wa mwanamke kuhudumia familia,” anasema Sukambi.

“Hata siku mtoto akikua na kuwa mume hataona shida kumuachia mkewe kuhudumia familia hata kama yeye ana kipato kikubwa, ataona kama mama yake aliweza kwa nini mkewe asiwezi, hivyo tunatengeneza kizazi ambacho hawaoni shida kuhudumiwa na wake zao.”

Anasema kwa watoto wa kike inamtengenezea akili ya kuamini yeye ndiye ana wajibu kuhudumia familia, ndiyo sababu wadada wengi wanapambana kutafuta pesa na haoni shida kuingia kwenye uhusiano na mwanamume ambaye hajielewi wala hafahamu anaelekea wapi kiuchumi.

“Ataolewa na mtu ambaye hana hela, dira, mipango na mpaka mahari anampatia ili amuoe, wanaona kama vile sifa, lakini yote haya yalianzia huko nyuma, ndiyo sasa tunafikia mahali mwanamume anakosa mamlaka ya kuwa kichwa cha familia.

“Katika uhusiano inapaswa mambo yote ya nyumbani, chakula, mavazi, umeme, ada na mengineyo kuwa ni jukumu la baba, hatakiwi kuonewa huruma wala kuchukuliwa kuwa anahitaji msaada wa mkewe, kama mkewe ana kipato basi kitumike katika uwekezaji mwingine.

“Watoto na mke wanapaswa kumuona baba anawajibika kama kichwa cha familia, kipato chake ndicho kiamue watoto watavaa nini, watakula nini, watasoma shule gani na mahitaji mengine ya nyumbani.

Wasikie wanaume

Wanaume wengi wanasema hawapendi kuoa wake ambao wamewazidi kipato, wakihofia manyanyaso, huku wengi wao wakieleza licha ya kuwa mapenzi sio pesa, inapotokea mwanamume umezidiwa kipato na mkeo lazima ujinyenyekeze utake, usitake.

“Mimi siwezi kuruhusu mke wangu anipite kipato, ingawa nyumbani tumegawana majukumu, yeye anafanya kwa asilimia 30 wakati mwingine hadi 20 na mimi nafanya asilimia 70 mpaka 80,” anasema Kulwa Magwa.

Mwanamume mwingine, Haji Salum anasema kuna wakati aliyumba kiuchumi baada ya kuachishwa kazi, mkewe ambaye ni daktari akawa na kipato kumzidi, hapo ndipo ndoa yao ilipovunjika.

“Ndani nilionekana kama mdudu, japo nilipokuwa na kazi nilimhudumia kwa kila kitu, hakuweza kunivumilia kipindi kile cha mpito,” anasema Salum.

“Sasa nimepata kazi nyingine, lakini nilichojifunza mke kumzidi kipato mumewe ni mateso, wachache sana wanaoweza kulinda heshima ya waume zao.”

Wanawake wanasemaje?

Stela Aidan anasema kama alimpenda mumewe akiwa hana kipato, basi ataendelea kumpenda hivyo hivyo kwa kuwa alimchagua bila kuagalia kipato chake.

“Kama kipato kimekatikia njiani hapo sasa itategemea na yeye alikuwa akinichukulia vipi wakati huo akiwa na kipato, kama ilikuwa ni ubabe ubabe, basi na kwangu itakuwa hivyo hivyo,” anasema Stela.

“Wapo wanawake wanaoishi na waume wasio na kipato, lakini huwezi kujua hadi uambiwe kuwa mwanamke ndiye ‘bosi’, ni wanyenyekevu kwa waume zao, japo ni wachache, wengi akiwa na kipato kumzidi mwanamume huwa ni tatizo, ndiyo sababu wanaume wengi hawapendi kuoa wanawake wenye vipato kuwazidi.”

Ester Raphael anasema yeye hawezi kuishi na mwanamume ambaye ana kipato kidogo zaidi yake, akitolea mfano wanawake wanazaa kwa uchungu hivyo wanaume wanapaswa kukubali kula kwa jasho ili waendelee kupata heshima ya kuwa kichwa cha familia.


Kisaikolojia hiko hivi

Mtaalamu wa Saikolojia ambaye ni Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Patandi, Modesta Kimonga anasema katika historia, jamii inaamini mwanamume ndiye anapaswa kuwa na kipato zaidi ya mkewe.

“Ikitokea mume akazidiwa (kipato), basi ataonekana ndivyo sivyo, ile hali itamfanya ajisikie unyonge, kisaikolojia itamuathiri, muda mwingi atahisi labda kwa kuwa hana hela ndiyo sababu anafanyiwa kitu fulani na mkewe hata kama amepewa ushauri mzuri.

“Atajiona hana sauti, atashindwa kufanya hata majukumu yake mengine kama baba, ataendelea kutojiamini, ile dhana hana hela itamuathiri kisaikolojia,” anasema Kimonga.