Chadema yataja mambo matatu furaha 2022

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ataja mambo matatu ambayo chama hicho, kimefurahishwa nayo kwa mwaka 2022 huku akisisitiza umuhimu wa mikutano ya hadhara na kwamba wapo mbioni kuifanya.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema mwaka 2022 kimefurahishwa na mambo matatu huku kikiendelea kupiga debe kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara ili vyama vitekeleze majukumu yao.

  

Mambo hayo ni pamoja na kuachiliwa huru kwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuanza mazungumzo na Serikali kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo mchakato wa Katiba mpya, maridhiano ya kisiasa na tume huru ya uchaguzi na kufanyika kwa kikao cha baraza kuu la chama hicho.

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameeleza hayo leo Jumapili Disemba 4, 2022 wakati akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu kuhusu masuala mbalimbali yaliyojitokeza mwaka 2022 na mwelekeo wa chama hicho kwa mwaka 2023.

“Jambo zuri kwa mwaka huu ni kuachiliwa kwa mwenyekiti wetu (Mbowe), aliyekuwa gerezani mkoani Dar es Salaam kwa miezi nane,” amesema Mnyika ambaye ni mbunge wa zamani wa majimbo ya Ubungo na Kibamba mkoani Dar es Salaam.


Machi 4, 2022, Mbowe na wenzake watatu, walifutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.


Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani nchini na wenzake walikuwa wanakabiliwa na kesi ya ugaidi na uhujumu uchumi, waliachiliwa huru baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.

Mbali na hilo, Mnyika amesema Chadema kimefurahishwa na kuanza kwa mazungumzo kati ya chama hicho na Serikali yanayoendelea kufanyika kwa nyakati yanayojadili masuala mbalimbali.

Kwa mara kwanza mazungumzo hayo yalianza Mei 22, 2022, kwa viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, miongoni mwa walioiwakilisha Chadema iliwakilishwa na Mnyika wakili Jeremiah Mtobesya aliyekuwa akimtetea Mbowe na wenzake watatu waliokuwa wakishtakiwa kwa ugaidi na uhujumu uchumi.

Wengine ni Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Catherine Ruge, Mjumbe wa Kamati Kuu, John Heche, Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Mohamed Issa, wakili Jonathan Mndeme, Reginald Munisi.

Upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alikuwapo Rais Samia, Makamu Mwenyekiti (Bara), Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.

Pia, kulikuwa na baadhi ya viongozi wa Serikali waliohudhuria mkutano huo, wakiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi.

Hata hivyo, Novemba 29, 2022, makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu anayeishi Ubeligiji alisema Chadema, kitaamua kama kiendelee mazungumzo na CCM au la ifikapo mwezi ujao kwa kuwa mambo mengi wanayolalamikia hayatekelezwi.

Mbali na hilo, Mnyika amesema mwaka huu Chadema wamefanikiwa kufanya kikao cha baraza kuu la chama hicho, kwa kishindo na kupitisha mipango mbalimbali ikiwemo Chadema Digital na ujenzi wa chama kuanzia ngazi za vijiji, vitongoji na  kata.

Pia, leo Jumapili katika mazungumzo yake na Mnyika amesema suala la kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa mwaka 2016 ili vyama kufanya shughuli za kisiasa limeendelea kuwa baya kwa upande wao pamoja kutoanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.

“Matokeo yake sasa kumekuwa na matatizo mbalimbali ikiwemo suala uhaba wa maji, wananchi wameshindwa kupata sauti mbadala ya kusemewa changamoto hii, kufanya mikutano na wanahabari pekee haitoshi.

“Tunahitaji kuzungumza na wananchi moja kwa moja kupitia mikutano ya hadhara ili tupaze sauti zao kuhusu changamoto hizi,” amesema Mnyika.

Hata hivyo, Mnyika amesema chama hicho kipo katika hatua ya mwisho ya maandalizi ya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali, akisema hivi sasa wanasubiri mrejesho kutoka kwa viongozi wao ngazi ya chini.

“Lini tutaanza tutawaambia, lakini tupo katika maandalizi ya mchakato.Suala la upatikanaji wa Katiba Mpya bado tunalipigia kelele,”amesema Mnyika aliyekuwa kuwa naibu katibu mkuu wa Chadema bara kabla ya kushika wadhifa wa sasa.

Mwezi uliopita mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, John Heche alisema Desemba haitaisha bila kufanya mikutano ya hadhara aliyosema ni haki kikatiba na kisheria kwa vyama vyote vya siasa.