Zelenskyy amteua waziri mpya wa ulinzi wa Ukraine, ataka mikakati mipya

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii Reznikov ambaye utuzi wake umetenguliwa
Muktasari:
- Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy jana Jumapili Septemba 3, 2023 alitangaza kufanya mabadiliko katika nafasi ya Waziri wa Ulinzi huku akimtoa Oleksiy Reznikov na nafasi yake kuchukuliwa na Rustem Umyerov.
Ukraine. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy jana Jumapili Septemba 3, 2023 alitangaza kufanya mabadiliko katika nafasi ya Waziri wa Ulinzi huku akimtoa Oleksiy Reznikov na nafasi yake kuchukuliwa na Rustem Umyerov.
Zelenskyy amechukua uamuzi huo ikiwa ni miezi 18 ipite tangu nchi hiyo iingie katika vita na Russia.
Akitaja sababu ya mabadiliko hayo, Rais huyo amesema anahitaji mbinu mpya na mikakati katika wizara hiyo hasa wakati huu wa vita.
“Reznikov alipitia zaidi ya siku 550 za vita. Ninaamini kwamba Wizara inahitaji mbinu mpya na miundo mingine ya mwingiliano na jeshi na jamii kwa ujumla," Zelenskyy ameandika kwenye Telegram.
Zelenskyy amesema kuwa anatarajia bunge la Ukraine kuidhinisha uamuzi huo wiki hii.
Uamuzi huo ulikuja chini ya mwezi mmoja baada ya Zelenskyy kuwafuta kazi maafisa wanaosimamia uandikishaji jeshi katika kila eneo la nchi, akitaja tuhuma za ufisadi ambazo alisema zinaweza kuwa uhaini.
"Mfumo huu unapaswa kuendeshwa na watu ambao wanajua hasa vita ni nini na kwa nini wasiwasi na rushwa wakati wa vita ni uhaini mkubwa," ameandika kwenye mtandao wa kijamii wakati huo.