Zaidi ya 260,000 waachwa bila makazi Gaza, vifo vikifikia 2,100
Gaza/Israel. Taarifa rasmi ya Umoja wa Mataifa (UN) imesema hadi leo Jumatano Oktoba 11, 2023 zaidi ya watu 260,000 wamelazimika kuyahama makazi yao katika ukanda wa Gaza huku jeshi la Israel likiendelea kushambulia eneo la Palestina.
Kwa mujibu wa UN, idadi hiyo ni kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao tangu kuongezeka kwa siku 50 kwa uhasama mnamo 2014 huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka zaidi.
Kwa mujibu wa BBC, ukanda wa Gaza ni nyumbani kwa takriban watu milioni 2.3 na una moja ya msongamano mkubwa zaidi wa watu ulimwenguni.
Mabomu katika siku za hivi karibuni yameharibu zaidi ya nyumba 1,000, UN imesema huku ikiongeza kuwa imekuwa ngumj kukidhi mahitaji ya kimsingi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la NBC idadi ya watu waliouawa Israel katika mashambulizi ya Hamas imeongezeka hadi 1,200 huku maafisa wakipata miili zaidi, msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel amesema leo Jumatano.
Zaidi ya Waisraeli wengine 2,700 wamejeruhiwa, Luteni Kanali Jonathan Conricus amesema.
Conricus amesema wanajeshi wa nchi kavu wametumwa katika maeneo yanayozunguka Gaza, na tayari wako karibu na Ukanda wa Gaza wakijitayarisha kutekeleza jukumu ambalo wamepewa.
"Hiyo ni kuhakikisha kuwa Hamas, mwishoni mwa vita hivi, haitakuwa na uwezo wowote wa kijeshi ambao wanaweza kutishia au kuua raia wa Israeli. Hilo ndilo lengo letu la kijeshi,” amesema.
Conricus pia amesema kuwa Hamas ina ofisi zake na mali nyingine katika majengo ya raia huko Gaza na kwamba ni malengo halali ya kijeshi kwa mashambulizi ya anga.
Wizara ya Afya ya Palestina imesema leo kuwa watu wasiopungua 900 wameuawa huko Gaza tu na kwamba 4,500 wamejeruhiwa.
(Imeandaliwa kwa msaada wa mtandao)