Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanajeshi 200 wauawa Burkina Faso, al-Qaeda yatajwa

Muktasari:

  • Mashambulizi hayo ya kushtukiza ya JNIM, yalifanywaa wakati ambao Rais Ibrahim Traoré alipokuwa ziarani nchini Russia, huku akitumia ziara hiyo kuomba msaada zaidi wa mafunzo na silaha kutoka kwa Rais Vladimir Putin ili kupambana na makundi hayo.

Ouagadogou. Kundi moja la wapiganaji linalofungamana na kundi la al-Qaeda, huko Afrika Magharibi limesema kuwa mashambulizi yake yamewaua wanajeshi 200 wa Burkina Faso katika kambi moja ya kijeshi nchini humo.

Al Jazeera imeripoti leo Ijumaa Mei 16, 2025, kuwa kundi hilo maarufu kama Jama'a Nusrat ul-Islam wa al-Muslimin, (JNIM) limefanya mashambulizi hayo kwa nyakati tofauti wiki hii.

Awali jana, kundi JNIM lenye ushirika na kundi la Al-Qaeda, lilisema kwamba limewauwa wanajeshi 60 na idadi hiyo imeongeza na kufikia takriban 200.

Hata hivyo, Al Jazeera haikuthibitisha taarifa ya kundi hilo. Mamlaka za Burkina Faso zilipotafutwa kuzungumzia madai hayo hazikujibu chochote.

Ingawa hakujatolewa taarifa rasmi na Serikali, lakini wakazi watatu wa mji wa Kaskazini wa Djibo uliovamiwa, wameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa wanajeshi na raia wa Burkina Faso wameuawa.

Tangu kutokea tukio hilo, kundi la JNIM limefunga njia ya kuelekea katika kambi ya kijeshi ya Djibo.

Mbali na kambi ya jeshi iliyopo Djibo, Shirika la Marekani la Site Intelligence Group linalojihusisha na uchunguzi wa matukio ya uhalifu, limetoa taarifa kuwa kundi hilo linadaiwa pia kulenga maeneo ya masoko na vituo vya polisi.

Pia, chanzo cha habari kutoka ndani ya Jeshi la Burkina Faso kiliiambia Al Jazeera kuwa kuna uwezekano wa wapiganaji hao kuwa wamesababisha athari zaidi.

“Operesheni hii inakuja wakati huu ambao shughuli za JNIM zimeongezeka nchini Burkina Faso mwezi uliopita na kusababisha vifo kadhaa,” imesema Site.

Shirika hilo hapo awali lilisema kuwa Kiongozi JNIM nchini Burkina Faso, Ousmane Dicko ameonekana katika video akiwaomba wakazi wa Djibo waondoke katika mji huo kwa usalama wao binafsi.

Akiripoti kutoka Dakar, Senegal, Mwandishi wa Al Jazeera, Nicolas Haque alisema kuwa shambulio hilo lilipangwa na kutekelezwa kwa siku kadhaa kuanzia Jumapili iliyopita.

“Mojawapo ya kambi kuu za kijeshi zilizopaswa kulinda mji huu wenye takribani watu 200,000 iliteketezwa kabisa, kutokana na nguvu wanamgambo hawa,” amesema Nicolas Haque wa Al Jazeera akiwa jijini Dakar.

“Hili ni mojawapo ya mashambulizi makali zaidi nchini Burkina Faso, wakati ambapo Ibrahim Traore ambaye ni kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso amekuwa akidai kuwa nchi imefanikiwa kurejesha hali ya amani,” amesema Haque.

Video inayodaiwa kusambazwa mitandaoni na tawi hilo la Al-Qaeda inawaonyesha wapiganaji hao wakiwataka raia kuondoka kwenye makazi yao na kutangaza kuwa litateka maeneo zaidi.

“Tunaona mabadiliko makubwa hapa makundi haya ya wanamgambo ambayo kwa kawaida hushambulia vijiji sasa yanajaribu kuteka miji. Hii ni pigo kubwa kwa jeshi la Burkina Faso,” amesema Haque.

Mwandishi huyo aliieleza Al Jazeera kuwa mashambulizi mengi ya wapiganaji hao yalitekelezwa wakati ambao Rais Traoré alipokuwa ziarani nchini Russia, huku akitumia ziara hiyo kuomba msaada zaidi wa mafunzo na silaha kutoka kwa Rais Vladimir Putin ili kupambana na makundi hayo.

Kwa mujibu wa Shirika la SITE, kundi la JNIM pia limedai kuhusika na shambulio jingine wiki hii dhidi ya kituo cha kijeshi katika mkoa wa kaskazini wa Loroum, ambapo linasema wanajeshi 60 waliuawa.

Mashambulizi hayo yanaonyesha changamoto kubwa ambazo mataifa matatu ya Sahel, Burkina Faso, Mali na Niger, yanayokumbwa nazo katika kudhibiti makundi ya kigaidi, huku yote yakiwa chini ya utawala wa kijeshi.

Mamlaka za Burkina Faso hazijatoa maoni kuhusu mashambulizi hayo.

Shambulio jingine kubwa lilitokea katika mji wa Sole nchini Burkina Faso, ambapo wapiganaji wa JNIM walivamia kituo cha jeshi na kuwaua wanajeshi.

Serikali ya kijeshi chini ya Kapteni Traoré, ilichukua madaraka nchini Burkina Faso mwaka 2022, lakini imeshindwa kwa kiasi kikubwa kuleta utulivu, kwani zaidi ya asilimia 60 ya nchi inakadiriwa kuwa nje ya udhibiti wa Serikali.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.