Wagombea 16 wajitokeza kupambana na Putin

Muktasari:
- Rais Vladimir Putin anatarajiwa kugombea nafasi hiyo kwa muhula wa tano.
Russia. Wagombea 16 wamewasilisha maombi ya kugombea urais wa Russia mwaka 2024.
Maofisa wa Tume ya Uchaguzi wamesema hayo leo Desemba 20, 2023, ambapo Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin anatarajiwa kugombea kwa muhula wa tano.
“Tumepokea maombi kutoka kwa wagombea 16 katika uchaguzi wa Rais,” Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (CEC), Ella Pamfilova amenukuliwa na Shirika la Habari la Serikali la Ria Novosti.
Akiwa kwenye mkutano na maveterani wa kijeshi mapema mwezi huu, Putin aliweka bayana kuwa atashiriki katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2024.
Uchaguzi huo utafanyika kwa siku tatu kuanzia Machi 15, mwakani.
CEC imesema kura pia zitapigwa katika mikoa minne ya Ukraine iliyokaliwa kwa sehemu na vikosi vya Russia na katika rasi ya Crimea, iliyochukuliwa kutoka Ukraine mwaka 2014.
Chama rafiki kwa Serikali ya Russia cha Liberal Democratic wiki hii kilimteua msuluhishi wa zamani wa mgogo wa Ukraine, Leonid Slutsky, kuwa mgombea wake.
Amesema kugombea kwake “hakutaondoa kura” kutoka kwa Putin.
Wagombea lazima wawasilishe maombi ya kushiriki katika uchaguzi wa Machi ifikapo Desemba 27,2023 kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
Baada ya hapo watahitaji kukusanya maelfu ya saini kutoka kwa wafuasi wao ili kupata nafasi kwenye uchaguzi.
Igor Girkin, mtu mwenye msimamo mkali na mkosoaji mkubwa wa Kremlin ambaye yuko kizuizini akisubiri kufunguliwa mashtaka kwa tuhuma za itikadi kali, amesema alitaka kumpinga Putin kwenye uchaguzi huo.
Mwanasiasa wa upinzani aliyefungwa, Alexei Navalny alizuiwa kugombea katika uchaguzi wa mwaka 2018 kutokana na mashtaka ya zamani ya udanganyifu ambayo washirika wake walisema ni ya kisiasa.