Vifo vyafikia 330 vita Sudan

Muktasari:
- Idadi ya vifo nchini Sudan imefikia 330 kufuatia vita vilivyozuka nchini humo mapema wiki hii, huku maelfu wakiukimbia mji mkuu Khartoum ambao ndio kitovu cha mapigano.
Sudan. Idadi ya vifo nchini Sudan kufuatia athari za vita vilivyozuka nchini humo kati ya wanajeshi wa Serikali na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) wakipigania udhibiti wa taifa hilo vimefikia 330 huku madhara zaidi yakitarajiwa.
Ahmed Al-Mandhari wa Shirika la Afya Ulimwenguni amesema jana Alhamisi kwamba karibu watu 330 wamekufa na karibu 3,200 zaidi wamejeruhiwa huko Khartoum, Mkoa wa Darfur Magharibi na majimbo mengine.
"Tunatamani mapigano yasitishwe wakati wa Sikukuu ya Eid ambayo itaanza Ijumaa kuadhimisha mwisho wa Ramadhani, Mwezi Mtukufu,” alisema Abdalla, mkazi wa Kusini mwa Khartoum.
Karibu na mji mkuu na kwingineko, wapiganaji wa RSF wakiwa juu ya magari ya kivita na lori ya kubebea mizigo yaliyokuwa na bunduki wameingia mitaani.
Wengi wameweka vizuizi ili kupekua magari yaliyokuwa yamewabeba raia wanaojaribu kutoroka maeneo mabaya zaidi ya mapigano ya Khartoum hadi maeneo salama katika mji mkuu na maeneo mengine.
Mapigano yameharibu majengo ya makazi na biashara, na raia wanaojificha katika nyumba zao wanazidi kukata tamaa.
Kufikia Jumanne, maelfu ya Wasudan walikuwa wameukimbia mji mkuu, huku wengi wakisema wameona maiti zikiwa zimezagaa mitaani walipokuwa wakielekea maeneo mengine nje ya mji mkuu.