UN yataka amani kunusuru maisha ya raia vita vya Israel, Palestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres
Muktasari:
- Katibu Mkuu Guterres ameeleza kusikitishwa na hali ya Gaza na kuomba misaada ya kibinadamu huku akilaani vitendo vyote vya vurugu na kuonya Israel kuhusu sheria za kimataifa. Amesisitiza umuhimu wa amani na suluhisho baina ya serikali mbili.
Geneva. Umoja wa Mataifa (UN) umetaka kufanyika kwa mazungumzo katika mgogoro wa kivita unaoendelea kati ya Israel na Palestina ili kupatikana kwa amani hususan kwa wananchi wanaoendelea kupoteza maisha bila hatia.
Katibu Mkuu wa UN, António Guterres amesema anasikitishwa na amri ya Israel ya kuzingirwa kikamilifu kwa Gaza na kukata umeme, kuzuia misaada ya chakula na mafuta katika eneo hilo lenye wakazi wengi.
Pia amelaani mashambulizi ya makombora katika hospitali na makazi katika Ukanda wa Gaza, akiomba Umoja wa Mataifa uruhusiwe kuingia kutoa misaada ya kibinadamu.
Guterres ambaye alizungumza na vyombo vya habari jana baada ya kukutana na viongozi wakuu, pia akilaani kitendo cha Hamas kuwateka raia na wanajeshi na pia alielezea wasiwasi wake juu ya ripoti za zaidi ya Wapalestina 500 waliouawa huko Gaza.
Ameiambia Israel kwamba operesheni za kijeshi lazima zifanywe kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Amesema watu 137,000 wamehifadhiwa katika makazi ya Umoja wa Mataifa huko Gaza idadi ambayo amebainisha kwamba inatarajiwa kuongezeka.
"Ni wakati wa kumaliza mzunguko huu mbaya wa umwagaji damu, chuki na ubaguzi," amesema.
"Ni amani tu ambayo itatimiza matarajio halali ya kitaifa ya Wapalestina na Waisraeli, pamoja na usalama wao sawa na maono ya muda mrefu ya suluhisho la serikali mbili.